To Chat with me click here

Sunday, December 16, 2012

SERIKALI KUMSAKA ALIYESAMBAZA UJUMBE KUWAFELISHA WANAFUNZI

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo
Hatua  ya walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani Simiyu kusambaza ujumbe kwa njia ya simu wa kuwafelisha wanafunzi, serikali imesema itawasiliana na kampuni za simu kumjua mmiliki wa simu iliyotumika kusambaza ujumbe huo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, kusoma moja ya ujumbe huo wa kuwahamasisha walimu mkoani humo na nchini kwa ujumla kuwafelisha wanafunzi ikiwa ni njia moja wapo ya kuishinikiza serikali kuwatatulia matatizo yao.

Mabiti alisoma ujumbe huo kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru iliyoadhimishwa mkoani humo na kusema kwamba atachukua hatua kali.

Ujumbe huo ulisema “Mchina si mjinga kutengeneza vitu feki, sisi walimu wa Tanzania kwa sababu serikali haitaki kutulipa vizuri, na sisi tutengeneze wanafunzi feki”.

Ujumbe huo umeelezwa kuwa matokeo yake yanaweza kujitokeza kwenye matokeo ya mitihani ya darasa la saba na yale ya kidato cha nne ya mwaka huu.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alisema kuwa anapata kigugumizi kuamini kama kweli ujumbe huo umeandikwa na mwalimu mwenye akili timamu na aliyeajiriwa na serikali.

“Tutashirikiana na serikali ya mkoa wa Simiyu, kwanza kujua kama kweli ni mwalimu aliyeuandika, lakini pia moja ya hatua tutakazochukua za kujiridhisha, tutapeleka namba ya simu iliyotumika kusambaza ujumbe huo kwa kampuni za simu ili kuwenza kumbaini mmiliki wake,” alisema jana Naibu Waziri huyo.

Kwa mujibu wa Mulugo, mfumo wa vyama vingi vya siasa unatumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kwani upo uwezekano changamoto zinazowakabili walimu zikatumiwa na wanasiasa hao vibaya.

Miongoni mwa madai ya walimu nchini ni pamoja na ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 100, posho ya kufundishia ya asilimia 55 kwa walimu wa sayansi na asilimia 50 walimu wa sanaa na posho ya asilimia 39 ya mshahara kwa mazingira magumu.

Hata hivyo serikali ilitoa msimamo wake juu ya madai hayo ambapo Rais Jakaya kikwete alisema hayatekelezeki.

Rais Kikwete alitoa mchanganuo kwa madai hayo kuwa yatafikia fungu la mshahara kwa watumishi wa umma kwa sh. trilioni 6.874 kati ya mapato yote ya ndani ya serikali ya sh. trilioni 8.

Katika kushughulikia matatizo ya walimu nchini, Mulugo alisema serikali imekwisha unda Baraza la Usuluhishi ambalo litakutana na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mapema mwakani.

Alisema kabla ya baraza hilo kukutana na walimu, serikali itakutana na CWT kabla ya siku kuu ya krismas ili kupata mchanganuo wa changamoto zinazowakabili walimu.

No comments:

Post a Comment