To Chat with me click here

Monday, December 10, 2012

MNYIKA ATAJA WANAOITAFUNA TANESCO



MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ametaja orodha ya watu waliohusika na uzembe katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), huku aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, William Mhando, akiongoza katika orodha hiyo.

Kwa mujibu wa Mnyika suala hilo aliloliita ufisadi, limechangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine.

Katika taarifa aliyotuma katika vyombo mbalimbali vya habari kupitia kwa msaidizi wake, mzigo wa ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu pamoja na ukiukwaji wa sheria za manunuzi ya umma, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema orodha za watuhumiwa wa ufisadi katika sekta ya nishati, zinatolewa kwa awamu zikigusa kwa kuanzia mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini na baadaye wizara yenyewe na hatimaye Serikali kwa ujumla.

Akitaja mikataba hiyo katika awamu ya kwanza na watu waliohusika, Mnyika moja kwa moja alianza kwa kumtaja Mhandisi Mhando kuwa alihusika na mikataba iliyozihusu Kampuni za M/S Santa Clara Supplies Company Limited pamoja na Kampuni ya M/S McDonald Live Line Techonology Limited.

Alisema Mhando ukiacha mkataba alioingia na kampuni ya Santa Clara, inayomilikiwa na familia yake kwa tenda namba PA/001/11/HQ/G/011 iliyopewa jukumu la kuleta vifaa vya ofisini, pia aliingia katika makubaliano yenye mgogoro na Donald George Mwakamele, ambaye ni Mkurugenzi na mwanahisa katika Kampuni ya McDonald.

Alisema Mhando ambaye alijifanya ni mfanyabiashara, alisaini makubaliano na kampuni kwa ajili ya kutafuta tenda, kununua, kujenga, kufanya matengenezo na kufanya miradi yote inayohusika na umeme kinyume na maadili ya TANESCO na sheria nyingine za nchi.

Mbali na Mhando, Mnyika aliwataja wahusika wengine wa ufisadi huo ndani ya Tanesco, kuwa ni pamoja na Ofisa Ugavi wa shirika hilo, Haruni Mitambo, Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kisanga na kwamba wote walihusika na kuruhusu na kuidhinisha malipo kwa kampuni tajwa.

Aliwataka wahusika wengine wa ufisadi huo kuwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Robert Shemhilu, France Mchalange, Naftari Kisiga, Sophia Msidai na Mhandisi Declain Mhaiki.

Wengine ni pamoja na Fatuma Chungo, Athanas Nangai, Elangwa Mgeni pamoja na wengine aliowataja kwa kifupi kwa majina ya S. Nkondola na N.Ntimba.

Mkurugenzi wa Kampuni ya MacDonald, Donald Mwakamele, alikana kuhusika na kuingia makubaliano na Mhando kwa ajili ya kazi yoyote ya shirika hilo na kuongeza kuwa, makubaliano aliyokuwa nao na Mhando ni kwa ajili ya kumsaidia kutafuta kazi nje ya nchi.

Alisema kitendo cha yeye kuhusishwa na Tanesco kinatokana na chuki binafsi kwake na Mhando zilizopo miongoni mwa baadhi ya watendaji wa shirika hilo (majina tunayo).

Aidha alisema, kwa mtu yeyote mwenye ushahidi wa makubaliano aliyoingia na Mhando akiwemo Mnyika ajitokeze na yupo tayari kumlipa kiasi cha Sh milioni 20.

No comments:

Post a Comment