WAKATI
wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi
ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa wabunge wenye
tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na wawili upinzani.
Habari
zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka
katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi
zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea
mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.
Vyanzo vya habari hii vimefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa
sababu za kitaaluma.
Baadhi
ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa,
wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa siyo
wakati mwafaka.
Moto
wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita
Kawawa wa Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili
lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa
rushwa zivunjwe.
“Waheshimiwa
wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha
55 (3)f mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe.
Sasa naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.
Aliliomba
pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na
kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na
wabunge.
Baada
ya hoja hiyo kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali
hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.
Spika
Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza
kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka kwa
watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
"Ninakubali
kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye tuhuma
hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi tutapata mwongozo wa kamati
hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:
"Nasema
kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili. Wabunge mkae
vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku kujitafutia masilahi
binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"
Mbunge Zedi
Baada
ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya
Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na uamuzi huo na
anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge.
"Nimeshtushwa
sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya
Bunge," alisema Zedi.
Waziri Muhongo
Akihitimisha
hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi
vya Tanesco kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia
mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.
"Shirika
liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri, lakini
kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa Muhongo na
kuongeza;
“Hata
katika nguzo za umeme kuna biashara inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo
zinazalishwa Iringa na kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo
kwamba zimetoka Afrika Kusini."
Waziri
Muhongo alisema kuwa mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe
wa Kamati ya Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya magari
kwa bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora unaokubalika.
"Baadhi
ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco; niseme tu kuwa, hii siyo sahihi.
Lakini niombe kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu, tayari tumekabidhi suala
hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)" alisema
Waziri Muhongo.
Waziri
Muhongo pia alizungumzia jinsi baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia Tanesco
kupitia mita za Luku ambapo aliwataja watu hao kuwa ni pamoja na Shule za
St. Mary's zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la Tabata Matumbi
Sh13.8 milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo inayodaiwa Sh25.5
milioni.
Alisema
kuwa baada ya kubainika kwa wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na
utaratibu,wahusika wote walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi baada
ya kufanyika kwa uchunguzi.
“Baada
ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia
na kuisababishia Tanesco hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo
kuwafikisha polisi,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
“Inaonyesha
wazi kwamba wizi wa umeme wa Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na kwamba
baada ya kuwakamata hawa, uchunguzi utaendelea na wengine watakaobainika
watachukuliwa hatua za kisheria.”
Jenista Mhagama
Katibu
wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa masikitiko
taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo, lakini akasema namna
nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya dola kufanya uchunguzi makini
ili kujiridhisha na kisha hatua za kisheria kufuatwa.
"Ni
taarifa mbaya kwa kweli, lakini mimi niiombe Serikali itusaidie kufanya
uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua zichukuliwe," alisema Mhagama.
Mbunge
Silinde
Naye
Katibu wa Wabunge wa Chadema, David Silinde alisema: "Kwa kuwa tumesikia,
kama kambi tutafanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo. Tutakaa kikao cha kuamua
nini cha kufanya. Pia tutatoa tamko juu ya mwenendo mzima wa hizi tuhuma na
Bunge kwa ujumla.”
Zitto
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma ambayo imeunganishwa kwenye tuhuma
hizo, Zitto Kabwe, alisema tuhuma hizo anazisikia, lakini anaziona kama siasa
za majitaka kwa sababu zinarushwa bila ushahidi wowote.
"Hakuna
hata mbunge mmoja aliyesimama kusema nani amehongwa nini. Mimi binafsi
sijahongwa na mtu yeyote wala mimi sijamtetea mtu isipokuwa natetea taratibu
kufuatwa," alisema.
Zitto
alibainisha kuwa anaamini tuhuma hizo zimetokana na hasira za yeye kupinga
posho za wabunge na sasa wameona hilo ndilo eneo la kumkomoa.
"Kwa
kuwa ‘my conscious is clear’, (dhamira yangu safi) sina mashaka, uzushi, uongo
na siasa za majitaka hizi zitaumbuliwa na ukweli. Hata hivyo, kwa kuwa tuhuma
hizo zinasemwa juu juu tu, tutataka vyombo vya dola vichunguze na ikithibitika
hatua zichukuliwe," alisema na kuongeza:
"Kwangu
mimi naona hizi ni siasa za urais na hasira za posho. Wenye kutaka urais wa
vyama vyote na wapambe wao, wameungana kunichafulia heshima yangu. Wabunge
wenye njaa ya posho, wameungana kunikomoa. Ukweli una tabia ya kutopenda
kupuuzwa. Mwalimu Nyerere (Julius) alisema katika andiko lake la
'Tujisahihishe'.”
Mbunge
huyo wa Kigoma Kaskazini(Chadema) alishauri pia Spika wa Bunge kutumia Kamati
ya Maadili kuchunguza tuhuma hizo kwa kuwa hazipaswi kuachwa zikapita hivihivi.
John Cheyo
Mwenyekiti
wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema anasikitika kuona Bunge
ambalo kimsingi ni kitovu cha uadilifu limeanza kuvamiwa na mafisadi.
"Very
unfortunate, (bahati mbaya sana) Bunge ambalo ni kilele cha uadilifu, nyumba ya
waheshimiwa, ambako kunatarajiwa high level of intergrity (uadilifu wa hali ya
juu), kuanza kutumika kama perpets (vibaraka) wa mafisadi," alisema.
Cheyo
aliongeza: "Ninalaani sana kitendo hicho, lakini niwaambie viongozi wapya
wa Wizara ya Nishati na Madini kuwa, waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na
nguvu yao ni wabunge wengi wema, ambao watawaunga mkono. Wasikate tama,"
alisema.
Mjadala ya wabunge
Mbunge
wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda aliliomba Bunge kufanya uchunguzi
ili kuwabaini wabunge wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema
baadhi ya wabunge wanatumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya
rushwa ili kuiyumbisha Serikali.
“Namwomba
Spika na timu yake yote ikaona kuna haja ya kufanya uchunguzi kwa wabunge ili
kuweza kuwabaini wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kujihusisha na vitendo vya
rushwa ilikuiyumbisha Serikali ,” alisema Shibuda
Mbuge Kangi
Naye
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alitaka Waziri wa Nishati na Madini awataje
wabunge aliowatuhumu ili kuonyesha usawa hasa baada ya kuwataja kwa majina
watuhumiwa wengine katika ufisadi wa Tanesco na wale wanaoliibia umeme shirika
hilo la umma.
"Tunaomba
waziri asema kwa nini asiwataje hao wengine wakati tayari ametutajia kina
Freddy na Veronica William Mhando na taasisi za St Mary? " alihoji.
Hoja
hiyo ya Lugora ilitupwa na Spika wa Bunge Anne Makinda aliyesema kuwa jambo
hilo lina taratibu zake.
Kamata
Vicky
Kimata (Viti Maalumu) nusura amwage machozi bungeni juzi jioni, alipozungumza
kwa uchungu kupinga hatua ya wabunge hao kujihusisha na ufisadi, huku akieleza
kuwa nchi imefika pabaya.
'Watanzania
tumefikia hapo! Watu wanatengeneza mgawo wa umeme ili kujipatia hela,
Jamani...jamani.. Hammwogopi hata Mungu!"
Said
Mussa Zuberi alipendekeza itungwe sheria ya kuwanyonga mafisadi na wahujumu
uchumi kwa kuwa matendo hayo pia ni uuaji.
"Katika
taifa letu tuna wadudu sijui tuwaite mchwa ambao wanaharibu yaliyotengenezwa
kwa maslahi yao. Nawashauri wananchi kwa kuwa sasa tuko kwenye suala la Katiba,
wasisahau kupitisha sheria ili watu wahujumu uchumi tuwaue, tena kwa
risasi.
No comments:
Post a Comment