Jeshi la
Polisi mkoani hapa limetumia magari yake kuziba barabara kwa lengo la
kumdhibiti Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufanya mkutano
wake wa hadhara, aliotarajia kuufanya katika Kijiji cha Mang’onyi.
Kufuataia hali hiyo, Lissu juzi alilazimika kubaki kijiji jirani na Mwau zaidi ya saa nne baada ya jeshi hilo ‘kupaki’ magari yake kwa ajili ya kufunga barabara ya kwenda eneo alilopanga kufanya mkutano huo.
Jeshi hilo lilipanga magari yake barabarani na askari wenye silaha umbali wa kilomita tano, kabla ya kuingia Kijiji cha Mang’onyi, eneo ambalo Lissu alipanga kufanya mkutano wa hadhara.
Hata hivyo, Lissu alilaani kitendo hicho, kwa madai kuwa kinawanyima wananchi haki ya kukutana na mbunge wao, kwa ajili ya kumweleza matatizo mbalimbali yanayowakabili.
Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Linus Sinzumswa, alisema hatua hiyo ilichukuliwa, baada ya Lissu kunyimwa kibali cha kufanyia mkutano katika Kijiji hicho, kutokana na sababu za usalama.
Sinzumwa alifafanua kuwa, licha ya mbunge huyo kuomba kibali cha kufanya mkutano wa hadhara, lakini alinyimwa kutokana na kuonyesha dalili za uwepo wa uvunjifu wa amani.
Kufuatia tukio hilo, Sinzumwa alisema kuwa Polisi inawashikilia watu watano kwa mahojiano zaidi kutokana na tuhuma za kujaribu kukusanyika eneo la mkutano usio na kibali.
Baadhi ya wananchi wamelalamikia jeshi la polisi kuanza kujihusisha na masuala ya siasa, badala ya kufanya kazi ya ulinzi ikiwemo kuulinda mkutano huo uweze kufanyika katika hali ya amani na utulivu, kuliko kumzuia mbunge wao bila sababu za msingi.
No comments:
Post a Comment