Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) Kifungu cha 99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa Fedha wa 2012/2013.
Mheshimiwa
Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na
ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi
waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya
kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha
wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya
kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za kuhamasisha mabadiliko
katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni.
Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo
kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa
http://mnyika.blogspot.com tutaendelea nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA;
Maslahi ya Umma Kwanza.
Mheshimiwa
Spika; Sekta za Nishati na Madini zina umuhimu maalum katika uchumi wa nchi na
maisha ya wananchi katika kipindi cha sasa na muda mrefu ujao. Wakati nishati
ikiwa nyenzo ya kuendesha maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya wananchi na
nchi kwa ujumla; madini ni mtaji na ni kati ya mitaji mikubwa ya kuwezesha
maendeleo ya haraka ya taifa. Hata hivyo, pamoja na Tanzania kujaliwa
rasilimali hizi nyingi ikiwemo watu, ardhi yenye rutuba, maji (bahari, mito na
maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara na
maliasili, bado takwimu za hali ya uchumi kwa mwaka 2011 zinaonyesha sehemu
kubwa ya Watanzania wako kwenye lindi la umaskini.
Mheshimiwa
Spika, tunajadili sekta za nishati na madini wakati taifa likiwa kwa mara
nyingine tena kwenye tishio la mgawo wa umeme pamoja na serikali kukanusha
kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme. Tunajadili mapitio ya utekelezaji wa
bajeti ya mwaka 2011/2012 wakati kwa mara nyingine tena kukiwa na mvutano baina
ya watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiwa
katika mvutano ambao umeambatana na kutuhumiana hadharani kupitia vyombo vya
habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Tunajadili
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka
2012/2013 wakati kukiwa na tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha
kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji
na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asili huku viongozi wa dini wakiwa
wamezindua ripoti juu ya ukwepaji kodi na upotevu wa mapato kwa serikali
unaogusa pia makampuni kwenye sekta za nishati na madini (The One Billion
Dollar Question).
Mheshimiwa
Spika, namuomba kila mmoja wetu atafakari kwa ukweli wa nafsi na nafasi yake
tumefikaje hapa kama taifa na kwa pamoja tukubaliane kuwa wabunge tuwajibike
kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio yote ya bunge kuhusu sekta za nishati
na madini ya miaka mbalimbali yanatekelezwa kwa haraka na kwa ukamilifu. Naamini
iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond
Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008,
maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011
yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa
Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti
bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa
uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii
hii mara kwa mara. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inatoa mwito kwa bunge
kupitisha maazimio ya kutaka uwajibikaji wa serikali kwa kushindwa kutekeleza
maazimio ya bunge kwa ukamilifu na kwa wakati.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 52 (1) Waziri Mkuu ndiye mwenye
madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na
shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye kiongozi wa shughuli za
Serikali Bungeni. Ni muhimu basi, badala ya kupokea majibu ya Wizara ya Nishati
na Madini pekee ambayo imeendelea kugubikwa na lundo la tuhuma mbalimbali,
Waziri Mkuu atoe kauli bungeni kuhusu kujirudia rudia kwa madai ya ufisadi na
uzembe katika sekta za nishati na madini.
Aidha,
pamoja na mabadiliko ya Mawaziri, Manaibu waziri, Makatibu wakuu na Wakurugenzi
wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ya mara kwa mara, Rais ashauriwe
kutumia nguvu zake za kikatiba za ibara ya 33, 34, 35 na 36 kuwezesha hatua za
kisheria kuchukuliwa kwa wote waliotuhumiwa kwa ufisadi, uhujumu uchumi na
matumizi mabaya ya madaraka kwa mujibu wa maazimio ya bunge na taarifa
mbalimbali za serikali ili kurejesha misingi ya uadilifu na uwajibikaji katika
sekta za nishati na madini.
Mheshimiwa
Spika, hivyo kwa ujumla mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka
wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 ulenge katika kuliepusha taifa letu kuendelea
kutumbukia katika ‘laana ya rasilimali’ kama ilivyojitokeza katika mataifa
mengine. Tuhakikishe tunalinda uhuru wa taifa letu dhidi ya uporaji wa ardhi na
rasilimali zake yakiwemo madini, mafuta na gesi asili ulio katika tishio la
ubeberu mamboleo, ufisadi na udhaifu wa kimifumo. Aidha, kupitia mchakato wa
katiba mpya wananchi watoe maoni ya kuhakikisha kuwa rasilimali za muhimu ikiwa
ni pamoja na madini, mafuta na gesi zinawekewa mfumo wa kunufaisha watanzania
wote na pia mikataba kuhusu rasilimali hizo inaridhiwa na Bunge.
Tuchangie
mjadala wa sekta hizi nyeti tukikumbuka maneno ya hayati Mwalimu Nyerere katika
kitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962, nanukuu: “Lakini woga unaweza
kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote
tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu
kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio
wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi
tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni
ubinafsi mbaya sana”
MAPITIO
YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012
Mheshimiwa
Spika, tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2010/2011 na
makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha
2011/2012. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali
imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi serikali haikuyazingatia
pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi. Hivyo kupitia
mapitio haya ya utekelezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze
hatua ilizochukua juu ya maoni hayo ambayo baadhi yalijitokeza pia kwenye maoni
ya Kamati za Kudumu za Bunge na michango ya wabunge kwa nyakati mbalimbali.
Hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kutoa na kujadili maoni mapya ikiwa hakuna
mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa
ukamilifu.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipitia kitabu cha pili cha matumizi ya kawaida
ya Wizara ya Nishati na Madini (Volume II Supply Votes) Fungu la 58 kwa mwaka
wa fedha 2011/2012 na kubaini kwamba ilikuwa ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho
na ufujaji ya zaidi ya shilingi bilioni 7.9 ya posho na matumizi mengine yasiyo
ya lazima. Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka serikali ifanye marekebisho kwenye
bajeti ili fedha hizo zipunguzwe na kuelekezwa kwenye kuongeza ujenzi wa
miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na kuongeza kiwango cha fedha katika
mfuko wawachimbaji wadogo wa madini. Aidha, yako matumizi mengine ya ujenzi wa
maofisi na gharama kubwa za kisheria yaliyopaswa kuhamishiwa katika miradi
muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini. Kwa kuwa Wizara iliahidi
kuufanyia kazi ushauri wa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kiwango cha fedha kilichookolewa kutokana
na kutekeleza ushauri huo na kutoa pia maelezo ni kwanini katika makadirio ya
mwaka 2012/2013 pamejitokeza kwa mara nyingine tena matumizi yasiyokuwa ya
lazima.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati
na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze kuzingatiwa kwa uzito
unaostahili: Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili
kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha.
Hatua hizo ziambatane na kuwekeza katika Bomba la Gesi, pamoja na ujenzi wa
mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika
kwenye magari, viwandani na majumbani; kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme
kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na
kumaliza tatizo la mgawo wa umeme na mwisho kutenga fedha za kutosha kwa ajili
ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa
uchumi vijijini.
Kusuasua kwa utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme
Mheshimiwa
Spika, ili kushinikiza nyongeza hiyo ya bajeti na utekelezaji wa vipaumbele
hivyo, Kambi Rasmi Bungeni ilipendekeza bunge kupitisha azimio la kutangaza
kwamba ukosefu wa nishati ni janga la taifa na kupitisha mpango wa dharura na
maamuzi ya hatua za haraka ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji
wa pamoja. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo
yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda
kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika
bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.
Mheshimiwa
Spika, hata hivyo inaelekea ahadi hiyo ilikuwa hewa kwani tarehe 13 Agosti 2011
Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika
serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya
bilioni 400. Pamoja na kuikumbusha serikali bungeni kutekeleza ahadi hiyo ya
Waziri Mkuu, serikali ilipuuzia ushauri uliotolewa. Matokeo yake mpaka sasa
Shirika la Umeme (TANESCO) halikuwezeshwa kupata kiwango cha fedha
kilichopangwa na utekelezaji wa mipango husika kusuasua.
Mheshimiwa
Spika, ikumbukwe kwamba Mpango wa Dharuraulipowasilishwa bungeni tarehe 13
Agosti 2011 serikali ilieleza kuwa imepanga kuongeza MW 572 ifikapo mwezi
Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina
ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50
Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011. Kimsingi, kauli iliyotolewa
bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli. Hivyo, ahadi ya
kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo
imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani
kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote,
walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond
Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa
mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi
hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana na taifa limerejea kwenye utegemezi wa
mitambo ya kukodi ya gharama kubwa ya umeme kwa sababu ya udhaifu na uzembe wa
kiutendaji. Hivyo, si kweli kwamba mpango wa dharura wa umeme umetekelezwa kwa
mafanikio ya asilimia 64.5 kama inavyodaiwa na Serikali kwa kupunguza lengo
lilopitishwa bungeni, bali mpaka sasa umetekelezwa kwa asilimia 47.6 tu; katika
muktadha huo, serikali inabidi ieleze kwa ukweli ni kwa vipi mgawo wa umeme
utaepukwa kwa kuzingatia pia barua ya Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO kwa Rais
yenye kueleza uwepo wa tishio la mgawo wa umeme.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine upungufu wa umeme unaojirudia rudia matokeo ya
serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa kuweka mitambo ya MW 100
Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato (Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango
wa umeme wa mwaka 2009 ambao ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya
mwaka fedha 2010/2011 Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi
kukamilisha uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Hata hivyo pamoja na
miradi hiyo kuingizwa kwenye mpango wa dharura tarehe 13 Agosti 2011 hakukuwa
na usimamizi thabiti wa kufanya ikamilike kwa wakati. Kuzinduliwa kwa mtambo wa
MW 100 Ubungo katika mwaka wa fedha 2012/2013 ni hatua ndogo kwa kuzingatia
kwamba, ilipaswa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee taifa liongeze jumla ya MW 360
toka kwenye mitambo ya kununua na si ya kukodi ili kuendana na malengo ya
mpango wa taifa wa miaka mitano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali
ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo na hatua za uwajibikaji
zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.
Kashfa
ya Ununuzi wa mafuta ya kufua umeme
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba mpango wa dharura wa
umeme na ununuzi wa mafuta kwa
ajili ya kufua umeme isitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha “Richmond
nyigine”. Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ya kuachia
dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache imesambaa kwa kiwango cha kuwa vigumu
kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala. Katika siku za
karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya
kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutokana na
uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa
kuipatia zabuni kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd. (zamani ikiitwa BP (Tz) Ltd.)
ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50. Licha ya malalamiko ya wazabuni
hao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa
imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge hili tukufu ili uamuzi
huu wa Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni hayo na wapambe
wake wa ndani na nje ya Bunge lako tukufu. Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo
wanashinikiza Katibu Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha
kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo,
tarehe 10 Juni, 2011 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO William Mhando
alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) –
iliyokuwa inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili
kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa unaendelea
sehemu mbalimbali nchini. Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba mara baada ya kupata
barua hiyo, tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia barua
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba
mwongozo na ushauri juu ya utaratibu wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo
ya IPTL kwa dharura.
Mkurugenzi
Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya tarehe 28 June, 2011
ambapo aliielekeza RITA itumie mamlaka yake chini ya kanuni ya 42 ya Kanuni za
Manunuzi ya Umma zinazohusu Bidhaa, Kazi na Huduma zisizokuwa na Ushauri
Elekezi na Mauzo ya Mali za Umma kwa Tenda, Gazeti la Serikali Na. 97 la mwaka
2005 (Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of
Public Assets by Tender) Regulations, Government Notice No. 97 of 2005). Kanuni
hiyo inamruhusu Afisa Masuhuli kuamua namna ya kufanya manunuzi kwa dharura
bila kujali mipaka ya mamlaka yake endapo kwa kufanya hivyo kutahakikisha
uchumi na ufanisi wa manunuzi hayo na endapo ataona ni kwa manufaa ya umma
kwamba bidhaa au kazi zenye thamani inayozidi mamlaka yake zinunuliwe kama
suala la dharura.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia
Katibu Mkuu Maswi barua ya tarehe 18 Julai, 2011 kumweleza kwamba katika
makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia IPTL tani 500 za mafuta kwa siku
zilizokuwa zinahitajika kuendeshea mitambo yake kwa mwezi Julai, 2011, kampuni
za OilCom na Shell hazikuwa na akiba ya mafuta wakati ambapo kampuni ya Mogas
ilikuwa na lita laki tatu tu. Kwa upande mwingine, kampuni ya Oryx ilikuwa na
tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa dola za Marekani 1,069.30 au
shilingi 1,668,456.02 kwa tani. Aidha, kampuni ya BP (sasa Puma Energy) ilikuwa
na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo kwa dola za Marekani 901.02
au shilingi 1,405,864.77 kwa tani. Kwa kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu
Maswi alitoa ridhaa kwa RITA kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL
kutoka kwa kampuni ya BP kwa bei iliyotajwa hapo juu.
Mheshimiwa
Spika, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei ndogo ikilinganishwa
na bei ya Oryx, tarehe 27 Septemba, 2011 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO
alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya dola za Marekani
926.98 au shilingi 1,501,707.60 kwa tani. Aidha, wiki moja kabla ya hapo, yaani
tarehe 21 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikwishasaini mkataba mwingine na
kampuni ya Camel Oil kwa bei ya dola za Marekani 905.24 au shilingi
1,466,488.80 kwa tani. Kama inavyoonekana,
mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kwa tani kuliko bei ya BP.
Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na TANESCO ikaanza kununua mafuta ya
kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa makampuni ya Oryx na Camel Oil.
Mheshimiwa
Spika, kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya makampuni ya Oryx na Camel
Oil kuonyesha bei za shilingi 1,501.70. na shilingi 1,466.49 kwa lita, TANESCO
ilianza kununua mafuta ya makampuni hayo kwa shilingi 1,850 kwa lita! Kwa maana
hiyo, kwa mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye
makampuni hayo, TANESCO ilikuwa inayalipa makampuni hayo jumla ya shilingi
29,803,500,000 kwa mwezi. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba
na RITA yaliigharimu Serikali shilingi bilioni 13,140,000,000 kwa bei ya
shilingi 1,460 kwa lita. Hii ndio kusema kwamba kama TANESCO ingeendeleza
mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya
IPTL ingekuwa shilingi 23,520,600,000 na hivyo TANESCO ingeliokolea taifa
shilingi 6,282,900,000 kila mwezi!
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine kumekuwa na taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari
kwamba Mkurugenzi Mtendaji Mhando hakutendewa haki aliposimamishwa kazi ili
kupisha uchunguzi juu ya utendaji kazi wake. Nyingi ya taarifa hizo zimetolewa
bila kuwa na faida ya kuangalia nyaraka zinazohoji uadilifu
na uaminifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Mheshimiwa
Spika, Mkurugenzi Mkuu Mhando ni mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni binafsi
inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd. ya Dar es Salaam. Wakurugenzi wengine
ni mke wake Eva Martin William, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji, na watoto wao.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, mnamo
tarehe 20 Desemba, 2011, Santa Clara Supplies iliingia mkataba na TANESCO
ambapo Santa Clara Supplies ilikubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya
TANESCO kwa gharama ya shilingi 884,550,000. Mkataba huu ulisainiwa na
Mkurugenzi Mtendaji Mhando kwa niaba ya TANESCO na mkewe Eva Martin William kwa
niaba ya Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya TANESCO iliyoitaarifu Santa
Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo iliyoandikwa tarehe 24 Novemba,
2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Mheshimiwa
Spika, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza kwamba “… kiongozi wa
umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu
wake kama kiongozi wa umma.” Aidha, “… kuhusiana na uwazi kwa wananchi,
viongozi wa umma watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha
shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na
umma na haitatosheleza kwaokutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile
vile, “… kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu
wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma.” Zaidi ya hayo, “… kuhusiana na
maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza
kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.”
Mwisho, “… kuhusiana
na maslahi ya umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma
watapanga masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi,
iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati
ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi
ya umma.”
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia ushahidi huu wa maandishi, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inamtaka Mbunge yeyote wa chama chochote cha siasa chenye uwakilishi
ndani ya Bunge lako tukufu, anayefuata imani yoyote ya dini aseme kama, kwa mujibu
wa vifungu hivi vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi Mtendaji
Mhando ana sifa za kuitwa kiongozi mwadilifu wa umma. Hivyo, pamoja na
uchunguzi wa kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka
Mkurugenzi wa Mashtaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai zichukuliwe dhidi
ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka.
Mheshimiwa
Spika; hata hivyo hatua hizo dhidi ya Mkurugenzi wa TANESCO na watendaji
waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali kwa
ujumla wake kwa kuwa taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa
umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa
kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na hata vikao vya baraza la
mawaziri. Hivyo, ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza
masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi
katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili
ya mitambo ya umeme. Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa
kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa
PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali
waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti
ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila
mtu “… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita
aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.
Mheshimiwa
Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani tuliitaka Serikali katika mwaka wa fedha
2011/2012 itoe taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango
wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) sanjari na kutoa ripoti
ya tathmini ya utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya
shirika (2006-2010). Hata hivyo, katika mwaka husika wa fedha utendaji wa
TANESCO na hali yake ya kifedha imeendelea kususua huku ukigubikwa na tuhuma za
ubadhirifu na udhaifu wa kiutendaji hali ambayo imepelekea pia mkurugenzi
mtendaji na maafisa wengine waandamizi kusimamishwa na kuchunguzwa. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaona kwamba hali hii ni matokeo ya udhaifu katika uteuzi na usimamizi
wa serikali kwa mashirika ya umma na inataka uwajibikaji kutokana na hali hiyo
kudumu kwa muda mrefu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iwaeleze
watanzania ni mikataba mingapi mibovu yenye kuipa mzigo mkubwa wa kifedha
TANESCO na kuongeza gharama kwa wananchi imefanyiwa mapitio katika mwaka wa
fedha 2011/2012.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa
gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi
ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Takribani nusu ya umeme
unaozalishwa nchini hivi sasa unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege
na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta
toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa
ajili ya
kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na
hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, Watanzania hivi sasa wanabeba
mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na
ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na
upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya
nishati.
Mheshimiwa
Spika, mzigo huu usingekuwa mkubwa iwapo Serikali ingetekeleza katika mwaka wa
fedha 2011/2012 maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya kuhakikisha nyongeza ya
fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa upande wa sekta ndogo ya
Gesi kwa ajili ya mitambo ya umeme na kuharakisha kuwekeza katika Bomba la Gesi
pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant).
Kutokana
na hatimaye Serikali kuzindua ujenzi wa Bomba la gesi katika mwaka wa fedha
2012/2013 na ahadi ya Wizara ya Nishati na Madini kuwa ujenzi huo utakamilika
katika kipindi cha miezi kumi na nane ijayo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka
serikali kutoa kauli ya uhakika kwa taifa; je, katika kipindi hiki cha mpito
imeweka mikakati gani ya kuhakikisha mitambo ya kufua umeme iliyopo inayotumia
gesi itapata gesi inayohitajika kuliondoa taifa katika upungufu wa umeme.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka Serikali iache kutoa
kisingizio cha ‘ufinyu wa bajeti’ katika kutekeleza maoni na mapendekezo ya
kuongeza fedha za Miradi ya maendeleo ya sekta za nishati na madini na
tulipendekeza vyanzo vya nyongeza vya mapato kwa ajili ya sekta tajwa ikiwemo:
kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa
Kampuni za Madini peke hatua ambayo ingeongeza mapato ya mapato ya shilingi
bilioni 59; Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta
ya madini kwa kurekebisha kodi sekta ya madini peke yake tungeweza kukusanya
shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi rasmi ya Upinzani
inataka maelezo toka kwa Serikali ni kwa kiwango gani ushauri huo umezingatiwa.
Mheshimiwa
Spika, uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka
wa fedha 2011/2012 ulionyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya kufikisha umeme
vijijini kwa upande wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Kasi ndogo ya kusambaza
umeme ilielezwa pia mijini kutokana na idadi kubwa ya maombi ya wananchi
wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa
halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka
ufanyike ukaguzi wa kiufanisi kuhusu utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa
umeme; hivyo serikali inapaswa kueleza iwapo ukaguzi husika ulifanyika na hatua
zilizochukuliwa na serikali katika kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze katika mwaka wa fedha
2011/2012 imetekeleza kwa kiwango gani mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi
na pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili
kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi
wetu. Izingatiwe kwamba malalamiko yameendelea kuhusu mazingira ya kupitishwa
kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango
kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East
African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine
vikididimia. Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi
mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa
kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa na kasi ndogo ya serikali wakati
wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/212 kuhusu kupunguza gharama
wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza
kasi ya uunganishwaji wa umeme. Bado tumeendelea kupokea malalamiko toka kwa
wananchi wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za
kuunganishwa
umeme
kwa viwango ambavyo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu.
Hivyo,
tunaitaka Serikali ieleze hatua za ziada inazokusudia kuchukua pamoja na
kutekeleza maoni yetu ya kutaka TANESCO ibadili mfumo wa ankara ili kuruhusu
kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inawahimiza wananchi kutumia Kanuni za Sheria ya
Umeme zilizotolewa kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63)
ambazo kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya
usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa
hiyo iweze kutumika ipasavyo; hata hivyo kanuni hizo zinahitaji pia kufanyiwa
marekebisho kwa kuwa zimeweka mkazo katika fidia kutolewa kutokana na malipo ya
wateja wengine badala ya mapato ya Shirika kwa ujumla wake Gesi
Asilia.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 15 Julai 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa nchi yetu imejaliwa
utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi na kwamba
taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana
kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta
ya nishati kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 yanaonyesha bado serikali haichukui hatua thabiti
kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili
hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa katika
mwaka wa fedha 2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha
migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.
Mheshimiwa
Spika, kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea mradi mkubwa wa
Songosongo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji, na usafirishaji ambao uko
chini ya Kampuni ya Songas. Hata hivyo, kampuni ya Songas imeiajiri Kampuni ya
PanAfrican Energy Tanzania (PAT), ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji,
usambazaji na ugavi wa gesi asili. Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza bungeni
tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika
sekta ndogo ya gesi na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza
suala hilo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilifanya uchunguzi
wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa bungeni; hata hivyo mpaka sasa
maamizio ya bunge kufuatia taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni kwanini mpaka sasa kiasi cha
dola milioni 20.1 zilizopunjwa kifisadi hazijareshwa na serikali iache kutumia
kisingizio cha kuundwa kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji
wa maazimio.
Mheshimiwa
Spika, mradi mkubwa wa maendeleo ambao umepangwa katika mwaka wa fedha ni
ujenzi wa bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam ambapo kwenye kasma
3162 umetengewa
kiasi cha shilingi 93,000,000,000 huku kiwango kingine cha fedha za mradi huo
kikitarajiwa kupatikana kutokana na mkopo kutoka nje. Kutokana na unyeti wa
mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha bungeni na kuweka wazi
kwa umma mkataba wa mradi husika ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia
serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa
yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za
uwekezaji huo mkubwa. Aidha, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia
gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo
ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo
kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230
wa Somanga Fungu (Kilwa).
Mheshimiwa
Spika, pamoja na ujenzi wa Bomba la Gesi, Kambi ya Rasmi ya Upinzani
inasisitiza mradi wa kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) na
mradi wa usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na mradi wa matumizi ya gesi
kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la Petroli Nchini (TPDC) inapaswa
kuongezewa rasilimali katika mwaka wa fedha 2012/2013. Kuanza kwa utekelezaji
wa mradi kwa ajili ya viwanda vichache na Kaya 57 za
eneo la Mikocheni ni hatua ndogo ukilinganisha na mahitaji; hivyo, utekelezaji
kwa mwaka wa fedha 2012/2013 upanuliwe wigo ili kuhusisha pia kuwezesha taasisi
zingine mathalani Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuweza kuunganishwa katika
mtandao wa matumizi ya gesi asili. Hatua hii itapunguza pia matumizi ya umeme
katika maeneo yenye kuweza kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza
kutumika kwenye maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala.
Mafuta
Mheshimiwa
Spika, taarifa za Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011 mfumuko wa bei ya
nishati na mafuta umeongezeka kwa asilimia 41.0 kwa mwezi Disemba 2011
ikilinganishwa na asilimia 12.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2010. Kambi
Rasmi ya Upinzani inarejea kusisitiza kwamba (ukiondoa kupanda kwa bei ya
chakula kunakotokana na kushuka kwa uzalishaji na udhaifu katika usambazaji)
chanzo kikuu cha hali cha mfumuko wa bei ni ongezeko la bei ya nishati hususani
mafuta, umeme na gesi, hali ambayo imeshindwa kudhibitiwa kwa mikakati makini
ya haraka na kuelekea kuwa tishio kwa utulivu wa taifa kiuchumi, kijamii na
kisiasa.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 15 Julai 2011 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
iliitahadharisha Serikali kwamba muswada wa Sheria ya Fedha uliopitishwa na
bunge tarehe 22 Juni 2011 usingeweza kupunguza
ugumu wa maisha kwa wananchi kwa kuwa serikali haikupunguza mzigo mkubwa wa
kodi badala yake iliweka kipaumbele katika kupunguza tatizo la uchakachuaji kwa
kuongeza mzigo mkubwa wa kodi katika mafuta ya taa. Matokeo yake ni kwamba
katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango cha kodi kwenye bei ya mafuta ya petrol
hakikupungua, kodi katika dizeli ilipungua kwa kiwango cha shilingi 99 huku
mafuta ya taa yakiongezeka kodi kwa shilingi 358 kwa lita na kuongeza mzigo wa
gharama za maisha kwa sababu ya udhaifu wa serikali na vyombo vyake katika
kudhibiti uchakachuaji kwa kusimamia utawala wa sheria.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze ni hatua zipi ambazo
Serikali imechukua dhidi ya athari za kupanda kwa bei ya mafuta ya taa kwa
wananchi wa kipato cha chini na pia kwa hali ya mazingira nchini kutokana na
ongezeko la matumizi ya kuni na mkaa. Aidha, ikiwa mkakati huu umeweza
kudhibiti uchakachuaji Serikali inatoa maelezo gani kutokana na kuwepo kwa
malalamiko ya kuendelea kwa aina nyingine za uchakachuaji, na ni kwa nini taifa
liendelee kuingia gharama za vinasaba vinavyowekwa na EWURA wakati inaelezwa
kwamba uchakachuaji umeweza kudhibitiwa baada ya kupandisha bei ya mafuta ya
taa?
Aidha,
kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta kufuatia mabadiliko ya
kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta serikali ieleze imefikia hatua gani
katika mwaka wa fedha2011/2012 kufanya mapitio ya mkataba baina ya EWURA na
kampuni ya Global Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za
kuweka vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).
Mheshimiwa
Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na ukubwa wa
kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa juu kutokana na mfumo mzima
wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji, uhifadhi na usambazaji. Mfumo uliopo
unanufaisha makampuni makubwa mengi yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara
wachache wa ndani pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu
kwa kulinyonya taifa na kuongeza gharama za maisha kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa
Spika, hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa miaka mingi kuanza kwa mfumo wa
uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk Procurement System) ili
kupunguza gharama; hata hivyo hata baada ya kuanza kwa utaratibu husika katika
mwaka wa fedha 2011/2012 tija ya kutosha ya mfumo huo haijapatikana kutokana na
udhaifu wa kimfumo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu za
kutokurejesha hifadhi ya taifa ya kimkakati ya taifa ya mafuta (National
Strategic Oil Reserve) pamoja na kutokukamilisha mchakato wote wa kufufua
Kampuni ya Taifa ya Mafuta (COPEC) kinyume na ahadi ya Wizara ya Nishati na
Madini ya mwaka 2011. Aidha, ni kwa nini serikali haikununua hisa za kampuni ya
BP kwa kiwango cha kuwa na umiliki wa asilimia 100 (100%)
ili kuongeza miundombinu ya uhifadhi na usambazaji wa mafuta kwa uchumi na
usalama wa nchi. Kwa upande mwingine, Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua
mahususi ilizochukua katika mwaka wa fedha 2011/2012 za kulinda maslahi ya nchi
katika kampuni ya TIPER ambayo serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji
na uhifadhi wa mafuta.
Mheshimiwa
Spika, Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali itoe maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa kwenye mwaka wa fedha
2011/2012 za kulifanyia marekebisho shirika hilo ili kuwa na mamlaka itakayohusika
na kutoa vibali kwenye leseni na kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi na
kampuni itakayoshiriki katika biashara ya mafuta na gesi.
Madini
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011
thamani ya mauzo ya madini nje ilikuwa dola za kimarekani 1,965.23 milioni
ikilinganisha na dola za kimarekani 1,536.93 milioni mwaka 2010, sawa na
ongezeko la asilimia 27.9. Hii ilitokana na kupanda kwa bei ya dhahabu katika
soko la dunia. Hata hivyo mchango kwenye pato la taifa umekuwa ni asilimia 3.3
tu miaka karibu mitatu toka kutungwa kwa sheria mpya ya madini mwaka 2010.
Udhaifu wa Serikali katika kusimamia utawala wa sheria unapaswa kuondolewa kwa
bunge kupitisha maazimio ya kuisimamia serikali kulinusuru taifa dhidi ya hali
hii ambayo utajiri wetu
unaendelea kuondoka, kwa pamoja na hatua zingine, kuwezesha mwingiliano baina
ya sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi katika nchi.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua iliyofikia
katika kuzingatia ushauri tulioutoa wa kutaka Wizara ya Nishati na Madini
ishirikiane na Wizara ya Fedha kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za malipo
ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo ya kila kampuni na mchangunuo wake
yafahamike kwa umma badala ya mfumo wa sasa ambapo hurundikwa pamoja katika
takwimu za idara ya walipa kodi wakubwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze hatua ilizochukua kwenye
mwaka wa fedha 2011/2012 katika kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi
kutokana na uchimbaji wa madini kwa kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za
umiliki na mitaji (capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda
mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na
ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini
nchini.
Mheshimiwa
Spika, wakati umefika sasa kwa Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya tathmini
ya utekelezaji wa mapendekezo ya tume/kamati mbalimbali ambazo ziliundwa na
serikali kwa nyakati mbalimbali
kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado
hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Kwa miaka mingi Serikali inazo taarifa za
makampuni makubwa ya madini kutumia sehemu kubwa ya uwekezaji wao kama mkopo
(debt financing) na kutumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha
wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya
mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inarudia tena kuitaka serikali iwaeleze Watanzania ni
trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika
kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu
asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa
waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo
kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida kubwa.
Mheshimiwa
Spika, katika nchi yetu tuna migodi mikubwa mbalimbali kati yake sita
ilianzishwa kati ya mwaka 1998 -2009 kwa ajili ya kuzalisha dhahabu ambayo ni Golden
Pride Mine (1998), Geita Gold Mine (2000), Bulyanhulu Gold Mine (2001), North
Mara Gold Mine (2002), Buhemba Gold Mine (2002) na Tulawaka Gold Mine (2005),
Buzwagi Gold Mine ( 2009). Buhemba Gold Mine walifunga uzalishaji mwaka 2006
Mheshimiwa Spika, migodi yote hii waliwasilisha upembuzi yakinifu serikalini
kabla ya kuanza uzalishaji na kuonyesha kuwa watalipa kodi ya makampuni
(Corporate tax) lakini mpaka sasa ni michache tu ambayo imeanza kulipa Shilingi
Bilioni 32.18 kutoka Resolute Tanzania Limited na Shilingi Bilioni 145.52
kutoka Geita Gold Mine Limited tu , pamoja na makampuni haya kunufaika na
kupanda kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia kwa zaidi ya mara tatu kuanzia
mwaka 2002, na wakati huohuo makampuni haya yakiendelea kuweka uwekezaji mkubwa
kwenye miradi yao. Kutokana na umuhimu wa sekta hii nitaeleza japo kwa kifupi
kuhusiana na baadhi ya migodi hiyo mmoja mmoja:
Mheshimiwa
Spika, mgodi wa Bulyanhulu ambao mwanzoni ulitarajiwa kuwa na maisha ya miaka
15 na walitarajia kuzalisha ounces 400,000 za dhahabu kwa kila mwaka ila
wamekuwa wakizalisha ounces 6.5 milioni za dhahabu kwa gharama ya kuzalisha
ounce 1 kwa dola 130. Aidha walitegemea kuzalisha madini ya Shaba (Copper )
ounces 7.26 milioni na madini ya fedha ounces 5 milioni na kwa sasa umri wa
mgodi ni miaka 25 , yaani muda umeongezeka kwa kipindi cha miaka 10 zaidi.
Mgodi wa Bulyanhulu uliwekeza kiasi cha dola 550 milioni kwa mchanganuo wa kuwa
dola 300 milioni kwa uwekezaji wa awali kabla ya kuanza uchimbaji na dola 250
milioni kwa shughuli za uendeshaji wa mgodi. Mgodi huu ulitegemea kuzalisha
kiasi cha dola 900 milioni kutokana na uchimbaji na uuzaji wa madini ya shaba
(copper) pekee na mapato
ya dhahabu yalikuwa yamewekewa ukomo wa dola 300 kwa ounce tuu pamoja na kuwepo
kwa badiliko la bei kwa zaidi ya mara tatu yaani sasa ni dola 950 kwa ounce
moja. Ilikadiriwa kuwa mrahaba wa asilimia 3 uliotegemewa kulipwa serikalini ni
kiasi cha dola 58 milioni, na fedha zilizopaswa kulipwa moja kwa moja
serikalini zilikadiriwa kuwa ni dola 64 milioni ( mrahaba dola 58
milioni,mrahaba wa moja kwa moja –direct dividend dola 2 milioni na kodi ya
zuio ya dola 4 milioni). Mgodi wa Bulyanhulu kwa sasa umeweza kuongeza hifadhi
ya dhahabu kutoka tani 13.64 milioni na kufikia kiwango cha tani 36.05 milioni
mwaka 2007 kiwango ambacho ni asilimia 90 zaidi ya kiwango kilichokadiriwa
wakati wa kusaini mikataba na kuanza uchimbaji. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu
ulilipa kiasi cha dola 26.54 milioni kama mrahaba kwa serikali, na hawajalipa
kodi ya makampuni .
Mheshimiwa
spika, kuhusu Mgodi wa Geita Gold Mine mgodi huu ulianzishwa kwa gharama
inayokadiriwa kuwa dola 152 milioni kwa ajili ya uwekezaji wote ambao ulifanywa
kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji na gharama za kuendeleza uchimbaji kwenye
mgodi husika. Mgodi hu ulikuwa umeweka malengo ya kifedha kwa bei ya dola 300
kwa ounce na kuwa thamani halisi (NPV) ni dola 100 milioni,Net cash flow dola
201 milioni, mrahaba dola 30 milioni,kodi ya makampuni dola 13 milioni,kipindi
cha kurejesha gharama miaka 5 na gharama za uzalishaji ni dola 181 kwa ounce.
Kwa mwaka 2000 mapato halisi yalikuwa dola 14 milioni na hii ilitokana na
ukwelikuwa kulikuwa na uzalishaji mdogo, na pia bei iliyokuwa imetarajiwa ya
dola 350 kwa ounce haikupatikana ila ilikuwa dola 279.321 kwa ounce moja. Mwaka
2004 mapato halisi yalikuwa zaidi ya mara nne ya matarajio nah ii ilitokana na
uzalishaji kuwa mkubwa na bei ya dhahabu kuongezeka kwani likikuwa dola 409.271
kwa ounce ikilinganishwa na ukadiriaji wa dola 350 kwa ounce uliokuwa umewekwa
awali. Ila kwa ujumla ni kuwa mapato halisi ya mgodi huu kuanzia mwaka 2001
yamekuwa yakiongezeka mara dufu kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya
dhahabu kuendelea kupanda kwenye soko la dunia. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu
ulikuwa haujalipa kodi ya makampuni pamoja na uzalishaji kuongezeka na kuwa
mara mbili zaidi ya matarajio na bei ya dhahabu kuwa kubwa mara tatu zaidi ya
matarajio kwenye soko la dunia na hii iliufanya mgodi huu mapato yake
kuongezeka zaidi ya mara tatu na mgodi uliendelea kutangaza kuwa unapata hasara
na haujaweza kurejesha uwekezaji uliofanywa.
Mheshimiwa
Spika, kuhusu mkodi wa Tulawaka katika mgodi huu uwekezaji uliofanywa
ulikadiriwa kuwa ni dola 34.6 milioni na gharama za uendeshaji zilitarajiwa
kuwa dola 325 kwa uzalishaji wa ounce 1, thamani halisi (NPV) Dola 9.507
milioni,net cash flow dola 29 milioni, mrahaba dola 5.367 milioni na kipindi
cha kurejesha gharama miaka 4(pay back period) na walitarajia kulipa kodi ya
makampuni mwaka 2008 ya dola 2.8 milioni. Kwa mwaka 2004 hapakuwa na uzalishaji
na hivyo hapakuwa na mapato yeyote ila kwa
mwaka 2004-2007 mapato halisi ya mgodi huu yamekuwa asilimia 72.5 ya zaidi ya
makadirio ya awali yaliyowekwa. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu haukuwahi kulipa
kodi ya makampuni pamoja na ukweli kuwa uzalishaji ulikuwa asilimia 7 chini ya
matarajio ila mapato halisi yaliongezeka kwa asilimia 72.5 zaidi ya matarajio
yaliyowekwa.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Mgodi wa North Mara mpaka disemba 2007 ilikadiriwa kuwa
kuna ounce 3.6 milioni ukilinganisha na zilizokuwa zimetangazwa awali wakati
mgodi unaanza uzalishaji kuwa ni 2.94 milioni ounce mwaka 2002 wakati wa
ufunguzi rasmi wa mgodi. Mgodi huu mpaka mwaka 2007 ulikuwa umebadilisha
wamiliki kwa zaidi ya wamiliki 3 tofauti tofauti na ii inafanya kuwa ngumu sana
kuweza kupata taarifa halisi za mwenendo wa m,apato kutokana na kila mmiliki
kuweka utaratibu wake na kuanza upya kama vile hapakuwa na kilichofanywa na
mmiliki aliyemtangulia. Aidha wamiliki wa awali waliweza kuuza migodi hii na
kunufaika moja kwa moja bila serikali kupata chochote kutokana na mauziano
yaliyofanywa.
Mheshimiwa
Spika, kwa taarifa hizi tunaweza kuelewa kuwa uzalishaji halisi wa dhahabu
kwenye migodi hiyo mitano kuanzia mwaka 1999 -2007 ulikuwa 8.388 milioni ounces
ukilinganisha na matarajio yaliyowekwa awali kuwa ni kuzalisha 6.882 milioni
ounces ambacho ni asilimia 21.88 zaidi ya matazamio ya awali. Umri kwa ajili
ya uzalishaji wa migodi hii umeongezeka kwa wastani wa miaka 4 kwa kiwango cha
chini na miaka 10 kwa kiwango cha juu, na hii ilitokana na kugundulika kwa
machimbo mapya ya dhahabu pamoja na kuongezeka kwa teknolojia ya kisasa zaidi
kwenye tasnia hii.
Mheshimiwa
Spika, mapato halisi yaliyoweza kupatikana kutokana migodi hii mitano mikubwa
kwa kipindi hicho cha kuanzia mwaka 1999-2007 ilikuwa dola 3.8 bilioni ambazo
ni asilimia 64 juu zaidi ya matarajio yaliyowekwa wakati uwekezaji ukifanywa
ambayo ni dola 2.3 bilioni .Pamoja na mapato hayo ni kuwa fedha iliyolipwa
serikalini kama mrahaba ilikuwa dola 99.6 milioni tu kwa kipindi chote hicho.
Kwa migodi yote hiyo matarajio ya bei yaliyowekwa yalikuwa kati ya dola 300-350
kwa ounce wakati uhalisia ni kuwa bei ilipanda na kufikia kiasi cha dola 950
kwa ounce 1.
Mheshimiwa
wa Spika, mapitio yaliyofanywa na Mamlaka ya ukaguzi wa madini (TMAA) kuanzia
mwaka 2004-2008 nchini yalionyesha kuwa mgodi wa TanzaniteOne Tanzanite Mine
(TTM) umekuwa ukilipa mrahaba kwa kutumia viwango vya awali vya makadirio
ambavyo viliwekwa wakati mgodi huu ukianzishwa nchini. Halikadhalika ripoti
hiyo inaonyesha kuwa kampuni hii imekuwa ikitoa taarifa za zisizokuwa za kweli
juu ya mauzo yaliyofanyika nchini na kwenye makampuni makubwa nje ya nchi ili
kuweza kukwepa kulipa mrahaba stahiki serikalini. Tathmini hiyo ya ukaguzi
inaonyesha kuwa kwa kipindi hicho kiasi cha dola 42.7 milioni kiliongezeka
zaidi kulingana na kiwango kilichotangazwa nchini na kampuni hiyo.
Hii
maana yake ni kuwa kiasi cha dola 2.1 milioni kilichopaswa kulipwa kama mrahaba
serikalini hakikulipwa kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu
cha 93 (the Mining Act, Cap., 123) . Suala hili ni kwa mujibu wa barua
iliyotumwa kwa Meneja wa kamapuni ya Tanzanite one iliyoandikwa tarehe
02.10.2009 yenye Kumb.Na DA23/168/01 iliyoandikwa na aliyekuwa Kamishina wa
Madini Mhe.Dalali Kafumu akiwataka wawekezaji hao kulipa hata hivyo deni hilo
halikulipwa kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua
ilizochukua huu ya kampuni hiyo. Aidha, tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya
kina kuhusu kuhamishwa kwa umiliki wa kampuni hiyo kwa kuzingatia kwamba baada
ya kutungwa kwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 Serikali iliahidi kwamba
uchimbaji katika eneo hilo ungeachwa kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Kambi
ya Upinzani , inaitaka serikali kuweka hadharani ripoti na taarifa zote
zilizowahi kutolewa kuhusiana na uwekezaji katika uchimbaji wa madini nchini
kuanzia mwaka 1995 hadi 2010 na kama serikali imefaidika na nini kutokana na
uwekezaji huo.
Pili
, tunahitaji mikataba yote iwekwe hadharani kwani kutokana na taarifa hizi ni
hakika kuwa mikataba yetu ni mibovu sana na tunalipotezea taifa mapato mengi na
hivyo kuendelea kudidimiza uchumi wa taifa.
Tatu,
Bunge liazimie kuwa mikataba yote mipya ya uchimbaji wa madini , mafuta na gesi
lazima sasa iletwe Bungeni na kujadiliwa kwa maslahi ya watanzania , kwani kama
tukiendelea na utamaduni wa kusaini mikataba husika kisirisiri taifa hili
litaendelea kupoteza mapato kutokana na uzembe na ufisadi kwa wanaohusika na
mikataba
Mheshimiwa
Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua iliyofikiwa katika
kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa ya kutaka Wizara ya Nishati na Madini
ishirikiane kwa karibu na Wizara ya Fedha katika kuweka mikakati na usimamizi
wa kuhusisha sekta ya madini katika kuimarisha fedha yetu. Wakati umefika sasa
wa kuwezesha Benki Kuu kutunza sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika
mfumo wa madini ya dhahabu. Hivyo Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na
Benki Kuu kuweka mfumo wa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo wadogo na pia
kutoza sehemu ya mrabaha wa dhahabu kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa
na Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kamati mbalimbali za bunge. Kambi Rasmi ya
Upinzani inasisitiza kwamba utaratibu huu uende sambamba na kusimamia mfumo wa
kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu kubwa ya fedha za nje (walau
60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya
Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu muhimu STAMICO ya kuwa
mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini nchini kwa niaba ya serikali.
Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yanadhihirisha kwamba
majukumu haya muhimu ya kisheria hayajawekewa mazingira wezeshi yakutosha ya
kimfumo, kirasilimali na kikanuni takribani miaka miwili tangu kutungwa kwa
sheria husika.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuharakisha marekebisho ya sheria ndogo
(Establishment Order) iliyounda STAMICO ili kuendana na mahitaji ya sasa na
kuongeza mtaji wake ikiwemo kurejesha rasilimali zilizochukuliwa ikiwemo
majengo. Serikali izingatie kwamba sera mkakati katika sekta ya madini iwe ni
kuhakikisha Watanzania wana umiliki katika miradi mikubwa ya madini ama kupitia
hisa za makampuni hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au kwa kampuni ya
umma kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika madini nyeti ikiwemo
urani.
Mheshimiwa
Spika, wwa kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wakala wa Jiolojia (GST)
aliendelea na utekelezaji wa mradi wa kutambua maeneo ya madini, Wizara ya
Nishati na Madini ieleze iwapo utekelezaji wa mradi huo ulienda sambamba na
kufanya tathmini ya kina (mineral appraisal) ya madini yetu ili kupendekeza mabadiliko
ya kisheria na kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika
kama mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na
rasilimali zake kamailivyopendekezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani. Aidha, ni
kiwango gani cha mapato kilichopatikana kwenye mwaka wa fedha 2011/2012
kutokana na kuiwezesha GST kutoza malipo kwa mujibu wa sheria ndogo
(Establishment Order) iliyounda wakala husika. Ili kulinda maslahi ya taifa
kuhusu matumizi ya ramani na ripoti za utafiti na uchunguzi huo katika mwaka wa
fedha 2012/2013 ukaguzi maalum (Special Audit) ufanyike kuhusu mfumo wa utoaji
leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini ili kudhibiti uporaji
(grabbing) unaoendelea katika rasilimali muhimu za taifa.
Mheshimiwa
Spika, tarehe 15 Julai 2011 tulitoa tahadhari juu ya maamuzi ya serikali ya
kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani
bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi
yanayohitajika suala ambalo linaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa
kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia linaweza kuhatarisha usalama.
Aidha, Kambi ya Rasmi ya Upinzani ilitaka maelezo ya kina kuhusu mauzo na
mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra
Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato.
Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River
(Mbamba Bay) na Bahi Kaskazini (Dodoma). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua
kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifanya ufuatiliaji juu ya suala hilo,
hivyo Wizara ya Nishati na Madini inapaswa kueleza kiasi gani cha fedha
kimefanikiwa kupatikana nani hatua zipi Serikali imechukua kwa makampuni
mengine ya madini, mafuta na gesi asili yaliyofanya mauziano katika mwaka wa
fedha 2011/2012.
Mheshimiwa
Spika, licha ya ahadi ya serikali ya toka mwaka 2010 ya kumaliza migogoro
katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo wadogo
ikiwemo kudhibiti migongano kati ya wenye leseni kubwa na leseni ndogo,
migogoro hiyo imeendelea katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha bungeni orodha ya maeneo yote yenye
migogoro ya madini nchini pamoja na ratiba ya utatuzi wa migogoro husika. Pia,
pamoja na kuandaa Mkakati wa Kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili mkakati huo
usiwe maneno matupu; Serikali iwasilishe pia mpango kazi na bajeti ya
utekelezaji wa mkakati husika. Aidha, Serikali ianzishe mfumo wa kisheria wa
kuwezesha wananchi waliokuwa wakilimiki ardhi katika maeneo yenye madini kuweza
pamoja na fidia ya mazao na maendelezo kuwa na hisa katika umiliki wa migodi
husika.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia kushamiri kwa migogoro baina ya wafanyakazi na wawekezaji
katika sekta ya madini, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Wizara ya Nishati
na Madini iweke mfumo wa mashauriano na Wizara nyingine ili kuharakisha utatuzi
wa migogoro husika. Aidha, kumekuwepo na wimbi la malalamiko ya wafanyakazi
walioachishwa katika migodi wa Bulyankulu, Kampuni ya Caspian katika mgodi wa
Mwadui Shinyanga , masuala ambayoyanahitaji ushirikiano wa wizara na mamlaka
mbalimbali katika kuyashughulikia. Aidha, Wizara ya Nishati na Madini itoe
maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi
ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea
kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha
Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kimelikanusha.
Kwa
kuwa ufafanuzi uliotolewa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii
(SSRA) kwa barua yenye Kumb. Na. AE/164/334/Vol II/2 umekataliwa katika migodi
mbalimbali, Wizara ya Nishati na Madini imechukua hatua gani kuepusha migogoro
iliyoanza kujitokeza baina ya wafanyakazi wa migodini na serikali kufuatia
kupitishwa kwa vifungu husika vya sheria vyenye kuagiza mafao kutolewa baada ya
kufikisha umri wa hiyari wa kustaafu wa miaka 55 au umri wa lazima wa miaka 60.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilihoji tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za
Kampuni ya New Almasi (1963) Limited kuchimba almasi kwa miaka 35 Mkoani
Shinyanga licha ya muda wa leseni yake Na. 224 kwisha na leseni yenyewe kufutwa
katika rejesta ya leseni za madini. Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba mkataba
kati ya New Almasi (1963) Ltd uliingiwa kinyemela kwa lengo la kuwezesha
uchimbaji wa almasi kuendelea katika eneo hilo kinyume cha sheria na ili
kuendeleza wizi wa rasilimali ya nchi yetu. Mamia ya wananchi waishio maeneo
jirani na eneo la New Almas wamekuwa
wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola kama vile polisi, mahakama na
vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni wavamizi wa eneo la leseni ya New
Almasi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua
kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuichunguza kampuni hiyo, uhalali wa shughuli
zake za uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa
kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na
zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo. Aidha, Serikali
ifafanue utaratibu wa kisheria ambao uliiruhusu Williamson Diamond Ltd.
kuendelea kuchimba almasi katika eneo la Luhumbo pamoja na utata juu ya uhalali
wa leseni katika eneo hilo.
MAKADIRIO
YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
Mheshimiwa
Spika, makadirio ya Matumizi na Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini
kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ni shilingi bilioni 641,269,000 ikilinganishwa na
Shilingi 538, 514,071,000 zilizotengwa wa Wizara mwaka 2011/2012 baada ya
kufanyika kwa uhamisho wa fedha. Bajeti hiyo imeongezeka kwa Shilingi
102,755,658,000 sawa na ongezeko la asilimia 19, hata hivyo ongezeko hili ni
dogo ukilinganisha na mahitaji yaliyotajwa na Mpango wa Taifa wa miaka mitano.
Mheshimiwa
Spika, makadirio ya mapato kwa upande wa makisio ya makusanyo ya maduhuli kwa
mwaka 2012/2013 ni Shilingi 193,007,543,000. Kati ya makusanyo hayo, jumla ya
Shilingi 173,702,263,000 zitakusanywa na Idara ya Madini, Shilingi 19,
217,277,000 zitakusanywa na Idara ya Nishati na Petroli, na Shilingi 88,003,000
zitakusanywa na Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu. Kambi Rasmi
ya Upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini ichukue hatua zaidi za kuongeza
mapato kwa kifungu cha 2001 cha Idara ya Madini Kasma 140101 ya Ada za Madini
na Kasma 140353 ya Mrabaha kwa pamoja; maeneo hayo yakiongezewa usimamizi kwa
mujibu wa matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake yana uwezo
wa kulipatia taifa kiasi kisichopungua bilioni 200 katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Aidha,
Wizara ya Nishati na Madini itoe maelezo iwapo matarajio ya makusanyo katika
Sekta ya Nishati na Petroli kifungu cha 3001 hususani kasma 140274 yanajumuisha
marejesho ya mapato ya mauzo ya gesi asili yaliyopunjwa kati ya mwaka 2004
mpaka 2010. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali izingatie kuwa mapato
katika shughuli za TPDC za utafiti wa mafuta pamoja na mauzo ya gesi asili
yanaweza kabisa kuongezeka ziada ya makadirio ya makusanyo ya bilioni 19 tu
iwapo udhibiti katika gharama na ukaguzi wa mikataba utaongezeka katika mwaka
wa fedha 2012/2013. Pia ili kuongeza mapato kwa serikali na TPDC Kambi Rasmi ya
Upinzani inataka mrabaha wa asilimia 12 kwenye gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa
sheria na isitishe mara moja utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa malipo
husika kwa mujibu wa wa sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato yameonyesha kwamba
wakati kwenye kifungu cha 2001 cha madini kuna mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye
kifungu 3001 kinachohusika na gesi na mafuta.
Mheshimiwa
Spika; Matumizi ya Kawaida yanaombewa Jumla ya Shilingi 110,078, 868,000 kati
ya fedha hizo shilingi 17, 292, 347,000 ni kwa ajili ya mishahara (P. E) ya
Wizara na Mashirika yaliyo chini yake na Shilingi 92,786, 521, 000 ni kwa ajili
ya Matumizi Mengineyo (OC). Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa rai kwa wabunge na
bunge kuungana pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya makubwa ya kawaida
kwenye matumizi mengineyo pamoja na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kubana
matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Serikali itakiwe kutoa
maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha Kitengo cha Sheria
ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kimetengewa
kiasi cha Shilingi 4,000,000,000 kama gharama za utetezi wa Serikali katika
kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya kuilipa kampuni ya Mkono &Co. Advocates .
Izingatiwe kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali ilifanya uhamisho wa
fedha wa kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi zilizopo
mahakamani zinazoihusu Wizara. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati ya mwaka 1995
mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa
za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha ya makampuni hayo. Aidha,
Serikali ieleze mkakati wa kudhibiti ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni
mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo
mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya
watu wachache. Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo
Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo
Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.
Mheshimiwa
Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika
sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya
Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Katika muendelezo wa
Serikali kampuni ya uwakili ya Mkono ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika
shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo kama Serikali
tungeshinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala
hilo. Lakini kutokana na uroho na kutaka maslahi binafsi kwa Kampuni ya Mkono
inaishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai
kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL wanakubali kusuluhishwa nje ya
mahakama.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliona hili kuwa ni mchezo wa
kuihujumu Serikali ambao umekuwa ukifanywa na makampuni binafsi ya uwakili
kuchelewesha kesi ili yeye aendelee kulipwa mabilioni ya fedha za walipakodi.
Huu ni uhujumu wa kodi za wavuja jasho wa nchi hii.
Mheshimiwa
Spika, katika muendelezo huo huo Kampuni ya Mkono &Advocates kwa sababu ya
uzoefu wake wa kazi hiyo na ushawishi wake mkubwa kwa viongozi wa Serikali
imekuwa ni kawaida kwa kampuni hiyo kuingia mikataba kuzitetea Kampuni za nje
zenye kutiliwa shaka kama ilivyo Kampuni ya matangazo inayotoka bara Asia
inayojiita Asia Business Channel inayodai kutengeneza matangazo ya biashara.
Kampuni hiyo yenye mwelekeo wa kutaka kutapeli ilitambulishwa kwa Mtendaji Mkuu
wa TMAA na Waziri wa Nishati kipindi hicho Mheshimiwa William Ngeleja kwa barua
yenye Kumb. Na. AB 88/233/01 ya tarehe 8 Desemba, 2011. Lengo lilikuwa ni TMAA
kuingia mkataba wa kutangaza sekta yetu ya madini nje ya nchi.
Katika
biashara hiyo ya kulazimisha, kampuni hiyo iliitumia Kampuni ya Mkono
&Advocates kuandika barua ya kusudio la kuishtaki TMAA kama itashindwa
kuilipa kampuni ya ASIA BUSINESS CHANNEL kiasi cha paundi za Kiingereza 35,500
kwa kazi ambayo majadiliano yalikuwa hayajafikia hatua ya mwisho. Kambi ya
Upinzani inajiuliza Kampuni hii kweli ni ya wazalendo au ni ya watu ambao
wanasukumwa na dhamira ya kufilisi rasilimali za Watanzania?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ambayo ina mamlaka ya kuiwakilisha Serikali katika kesi zote zinazoihusu
Serikali ieleze imechukua hatua gani kuhusu hali hii na ifungulie mashtaka
Kampuni zote zenye kuonyesha uzembe na hujuma katika kuishauri serikali kwenye
kesi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazohusu nishati na madini.
Mheshimiwa
Spika, aidha, kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itashindwa kutekeleza hilo ni wazi
Mshauri huyo Mkuu wa Serikali katika mambo ya sheria atakuwa na yeye ameshindwa
kazi na hivyo ni bora awape nafasi watu wenye uwezo wa kuangalia na kusimamia
maslahi ya umma.
Mheshimiwa
Spika, Miradi ya Maendeleo imetengewa Jumla ya Shilingi 531, 190, 861,000 kati
yake Shilingi 431,190, 861,000 ni fedha za ndani na Shilingi 100,000,000,000 ni
fedha za nje. Kati ya hizo kifungu cha 2001 cha Madini kimetengewa katika Kasma
3152 Shilingi 240,000,000 tu tena za nje kwa ajili ya Uwazi katika Tasnia ya
Uziduaji (Tanzania Extrative Industries Transparency Initiatives –TEITI) hivyo
kutokana na umuhimu wa asasi hiyo katika kuweka mfumo wa uwazi katika usimamizi
na uvunaji wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asili ni muhimu kiwango cha
fedha kikaongezwa na kuhakikisha kwamba Sheria ya TEITI inatungwa katika mwaka
wa fedha 2012/2013. Aidha, Taarifa zote tatu za TEITI (Reconciliation Reports)
ziwasilishwe na kujadiliwa bungeni. Kwa upande mwingine, bunge lisikubali
kupitisha kiasi cha Shilingi 40,000,000,000 kinacho ombwa kwenye
Kasma 3160 kwa ajili ya kulipia madeni ya Kiwira (KCPL) mpaka uhakiki ufanyike
juu ya uhalali wa viwango vya madeni husika kwa kuwa mradi mzima uligubikwa na
tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa Miradi ya Maendeleo ya Nishati na Petroli kifungu cha
3001, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu sababu za
kutekelezwa taratibu kwa mradi wa TEDAP (Kasma 3132) ambao iwapo utaharakishwa
utakuwa na mchango katika kuboresha mfumo wa gridi pamoja na kuhamasisha
matumizi ya nishati jadidifu kama vyanzo mbadala katika uzalishaji umeme nje ya
gridi. Aidha, pamoja na nyongeza ya fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya
Wakala pamoja na Mfuko wa Umeme Vijijini (REA/REF) (Kasma 3113); Kambi Rasmi ya
Upinzani inasisitiza umuhimu wa kuongeza kiwango cha fedha za ndani ili kufikia
bilioni 150 ili kuharakisha kasi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini.
Pia, kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme, pamoja na kuondoa kodi
katika vifaa vya umeme wa jua, serikali ieleze hatua ilizochukua katika kuweka
mazingira wezeshi kwa vifaa vya umeme wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi
mathalani vifaa vya kuhifadhia umeme (invertors). Kupitia Kasma 3147 Wizara ya
Nishati na Madini inaomba 47,959,861,000 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili
ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya dharura, hivyo ni muhimu maelezo
yakatolewa kuhusu matumizi ya fedha za mafuta ya mitambo
ya dharura kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ili kujenga uhalali wa matumizi ya
mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Nishati na Madini inaomba shilingi 62,000,000,000 kwa ajili ya
Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154).
Pamoja na mradi huo kuweka mkazo katika kufunga transfoma kubwa zaidi na njia
kubwa za umeme za msongo wa kV 33 kwa ajili ya wateja wakubwa wa katikati ya
Jiji; mradi uweke mkazo pia katika usambazaji wa umeme pamoja na kuongeza nguvu
ya umeme katika maeneo ya pembezoni ya Jiji la Dar es salaam. Izingatiwe kwamba
matatizo ya miundombinu ya umeme katika Jiji la Dar es salaam kutoendana na
kasi ya ongezeko la mahitaji ya umeme hayapo katikati ya jiji pekee bali pia
yapo maeneo ya pembezoni yenye ongezeko la wakazi na vitega uchumi mbalimbali.
Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Malambamawili, Kwembe, Goba Matosa, Msakuzi,
King’ongo na mengineyo katika Manispaa mbalimbali za Jiji la Dar es salaam.
Aidha, Wizara ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa ajili ya
kulipa fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo
ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba
ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kutokana na Mpango wa Dharura wa
Umeme uliopitishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 Serikali imepanga kuanza
utekelezaji wa miradi ya MW 240 Kinyerezi ambao umetengewa shilingi
5,000,000,000 katika Kasma 3163 na MW 150 Kinyerezi ambao umetengewa shilingi
bilioni 13,000,000,000 katika Kasma 3164. Hata hivyo, kwa miradi yote hiyo
Serikali iko katika hatua ya majadiliano na kufunga mikataba ya mikopo na
Kampuni za SUMITOMO na Jacobsen wakati ambapo michakato ya miradi hiyo ilianza
toka mwaka 2009. Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea kuitaka Serikali kutangaza
matatizo ya nishati ni janga la taifa ili kuweka mfumo wa dharura wa
kushughulikia kwa haraka kwa usimamizi wa uongozi mkuu wa nchi tofauti na sasa
ambapo miradi hiyo inachukuliwa kuwa ni ya kawaida chini ya Wizara ya Nishati
na Madini.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka uhakika toka kwa Serikali iwapo mitambo hiyo
inayotarajiwa kutumia gesi itakamilika lini na iwapo itapata nishati husika kwa
wakati na kwa uhakika kwa kuzingatia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa bomba la
gesi. Pia, Serikali itaje miradi mingine ya nyongeza ambayo utekelezaji wake
unakusudiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2012/2013 ili kufidia pengo la mwaka
wa fedha 2011/2012 na kuhakikisha kwamba kila mwaka wastani wa MW 360 za
mitambo isiyokuwa ya kukodi zinaingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa
Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2011/2012-2015/2016)
umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka kufikia MW 2780 kwa kuongeza MW
1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa kwenye mpango kipengele A.1.3 kuhusu
nishati. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na rasilimali ambazo zipo katika
taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza imefikia
hatua gani katika kufanya mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine
mikubwa ukiwemo wa Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100 kama
nilivyopendekeza bungeni tarehe 14 Juni 2011 na kuingiza pia makadirio ya
ujumla ya MW zinazotokana na miradi midogo midogo itakayoanzishwa katika maeneo
mbalimbali kama tulivyoshauri tarehe 15 Julai 2011.
Mheshimiwa
Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani
inarudia kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza mazingira wezeshi ambayo
yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo iweze kupata rasilimali kwa wakati
na makubaliano kukamilishwa mapema: Iringa-Mchuchuma na Ngaka (Makaa ya
Mawe-300), Kiwira (MW 200) , Singida (Upepo) na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji-
MW 358).
Mheshimiwa
Spika, ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo vilianzishwa na
Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati Mwalimu Nyerere, na awamu
zilizofuata sio tu zimeshindwa kuongeza kasi ya kuzalisha umeme bali pia zimeshindwa
kukarabati mitambo hiyo na hivyo kuzalisha chini ya kiwango. Taarifa ya Hali ya
Uchumi ya mwaka 2010 ilionyesha kwamba vituo vya kuzalisha umeme vilikuwa
vikifua umeme kwa wastani wa 53.5 tu ya uwezo wake; hivyo Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka pia Serikali kueleza imechukua hatua gani kwa mwaka 2011/2012
na inapanga kuchukua hatua gani za dharura kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kuhakikisha uwezo wa vyanzo vilivyopo kuzalishaji unaongezeka sanjari na
kupunguza upotevu wa umeme kutokana na ubovu wa mifumo ya usafirishaji na
usambazaji.
Mheshimiwa
Spika; ili kujiandaa kitaalamu kama taifa kwa mipango kabambe ya gesi wakati
nchi ikisubiri Sera ya gesi, Sheria ya Gesi na Mpango Kabambe wa Gesi (Gas
Master Plan) vinavyopaswa kuwasilishwa katika Mkutano wa Tisa wa Bunge. Pia
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua
iliyofikiwa katika kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta ili fani
hizo ziweze kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha, wakati wa
kuhitimisha mjadala wa mpango wa mpango wa taifa wa miaka mitano tarehe 14 Juni
2011 serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara. Hata
hivyo hicho hakijaingizwa kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano toleo la mwezi
Juni 2012 kifungu cha A.1.5. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza
ni hatua zipi zitaanza kuchukuliwa kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 na Wizara ya
Nishati na Madini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika kuwezesha
kuanzishwa kwa Chuo Kikuu
hicho muhimu ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika masuala ya mafuta
na gesi na bidhaa zitokanazo na gesi na mafuta.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha sekta ya gesi na sekta kuwa na manufaa kwa nchi yetu,
narudia tena mapendekezo kama tulivyoyatoa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani kama ilivyowasilishwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika hotuba
yake Ofisi ya Waziri Mkuu nanukuu kama ifuatavyo:
“Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani inatoa mapendekezo yafuatayo katika kuimarisha na
kuboresha sekta ya gesi na mafuta hapa nchini ili kuitayarisha nchi kwa utajiri
huu mkubwa:
i.
Wananchi wanaozunguka maeneo yanayopatikana au yanayopitia gesi asili wawe
sehemu ya mipango ya maendeleo ya gesi asili na hivyo kunufaika na matumizi ya
gesi badala ya kuachwa, hali inayoleta manunguniko na tishio la uendelevu wa
sekta husika na haswa ikizingatiwa kuwa uwekezaji unaofanywa katika sekta hii
kama wananchi hawataona kuwa na wao ni wafaidika ni rahisi sana kuweza kuhujumu
miundombinu hii na kuhatarisha usalama na hata uhai wa wananchi wengine .
ii.
Ujenzi wa miundombinu ya gesi uwe unazingatia mahitaji ya muda mrefu ili
kupunguza gharama na kuondokana na uhaba na uharibifu wa maliasili, mfano bomba
la Songosongo liliwekwa bila kuzingatia mahitaji asili ya gesi na hivyo
kujikuta kuwa wanashindwa kusafirisha gesi ya kutosha kutumiwa na wahitaji
wote;
iii.
Tuwekeze kwenye kuwapa elimu na maarifa vijana wa Kitanzania na haswa kwenye
Sekta ya gesi ili waweze kupata utaalamu wa jinsi ya kusimamia sekta hii kama
ambavyo nchi majirani zetu wa Uganda na Msumbiji wamefanya kwa kuwapeleka
vijana wao nje ya nchi ili kupata utaalamu juu ya uendeshaji wa sekta hii.
iv.
Serikali iliahidi kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwamba Sheria ya usimamizi
bora wa Fedha za Mafuta na Gesi (Petroleum Revenue Management act) italetwa
Bungeni mnamo mwezi Novemba. Kambi ya Upinzani inasisitiza kwamba Sheria hii
iletwe haraka ili kuweka wazi mapato yatokanayo na utajiri huu na namna bora ya
kutumia fedha hizi ili kuzuia uchumi kuathiriwa na pia kuzuia ufisadi. Hatutaki
Tanzania iwe kama nchi nyingine za Kiafrika ambazo utajiri wa Mafuta na Gesi
umekuwa ni laana badala ya Neema.
v.
Serikali iweke mazingira bora ya kujenga uwezo wa Watanzania kutoa huduma
kwenye kila hatua ya utafutaji wa Mafuta na Gesi. Hivi sasa kuna zaidi ya
wageni 1200 kwenye Meli za kutafuta Mafuta na Gesi katika Pwani ya Mtwara,
Lindi na Pwani. Kwa masikitiko makubwa sana wageni hawa wanakula hata nyanya,
mchicha na vitunguu kutoka nje ya Tanzania.
vi.
Vile vile tudhibiti makampuni ya Ulinzi kutoka nje kuwa na silaha kali kali kwa
kujenga uwezo wa Jeshi letu la Majini (Navy) ili liwe na kikosi maalumu kwa
ajili ya kulinda meli za kutafuta mafuta na Gesi na Makampuni haya yatozwe tozo
maalumu. Ni hatari sana makampuni ya kigeni kuwa na masilaha makubwa ndani ya ramani
ya nchi yetu”.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kwamba muswada wa
sheria ya fedha wa mwaka 2012 uhakikishe misamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni
za utafutaji wa mafuta na Gesi inaondolewa. Izingatiwe kuwa uzoefu kutokana na
misamaha ambayo imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini unadhihirisha kwamba
makampuni mengi yanatumia mwanya huo kuleta mafuta yasiyo na kodi na kuyaingiza
kwenye soko la ndani la reja reja. Hivyo, misamaha hii haina maslahi kwa taifa
na ni mianya mingine ya uhujumu uchumi kwa kuwa kampuni za utafutaji mafuta na
gesi zinayo fursa kwa mujibu wa mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao mara
baada ya mafuta kupatikana.
Aidha,
uamuzi huu uhusishe pia kampuni za madini bila kujali mikataba (MDA) kwa kuwa
imethibitika kampuni hizi zote hutengeneza faida nono bila kulipa kodi
inavyostahili.
Mheshimiwa
Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya serikali
katika mwaka wa fedha 2012/2013 Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Wizara
ya Nishati na Madini ieleze hatua
mahususi ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo: kutunga Sheria ya
kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika
mahesabu ya kodi isizidi 60% ya mtaji; kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba
ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi;
kufanya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains)
inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au
uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi kwa
kuzingatia kuwa mapendekezo yaliyoingizwa kwenye muswada wa sheria ya fedha wa
mwaka 2012 hayakuzingatia kwa ukamilifu msingi wa mapendekezo yaliyotolewa na
Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011.
HITIMISHO
Mheshimimiwa
Spika; kambi rasmi ya upinzani inapenda kuhitimisha kwa kusisitiza kwa mara
nyingine kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini
yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera,
kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali wenye dhamana
na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na
kuathiri uchumi wa nchi.
Mheshimiwa
Spika, mabadiliko ya kimfumo yanahitajika ili kuwezesha hatua za haraka za
kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti katika sekta nyeti za
nishati na madini sanjari na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika
katika sekta hizi, kufanya mapitio ya mikataba na kuharakisha utekelezaji wa
mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.
Mheshimiwa
Spika, nimalize kwa kuwashukuru wananchi wa Ubungo kwa ushirikiano wao katika
kazi nifanyazo za kuwawakilisha kwenye vyombo vya maamuzi na kuhamasisha
maendeleo Jimboni. Kwa namna ya pekee nitambue mchango wa madiwani wote
tunaoshirikiana katika kipindi ninachokuwa kwenye majukumu mengine ya ujenzi wa
taifa. Nawashukuru viongozi wa dini washauri wangu wa kiroho na wanafamilia yetu
ya Dalali kwa upendo na kuniasa kuendeleza ujasiri na uadilifu katika kusimamia
ukweli, haki na ustawi wa Jamii.
Mheshimiwa
Spika, natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum
Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika
wajibu wa kuwatumikia Watanzania na kuhamasisha mabadiliko katika taifa letu.
Hali tete na tata ya sasa inatutaka tuwe na mshikamano zaidi mpaka kieleweke.
Mheshimiwa
Spika; nawashukuru baadhi ya viongozi katika mamlaka mliotambua kwamba “siasa
siyo uadui” na kunipa ushirikiano kwenye serikali kuu, Wizara ya Nishati na
Madini, Manispaa ya Kinondoni, katika kamati ya nishati na madini na wabunge
wengine kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kibunge kwa manufaa ya taifa
letu na watu wote.
Mheshimiwa
Spika, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili mapitio ya utekelezaji
wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya
Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa
ya kuongeza bajeti ya wizara husika; kupokea mapendekezo ya kuzingatiwa katika
muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 na kupitisha maazimio mahususi ya
kuhakikisha sekta za nishati na madini zinachangia kikamilifu katika kuinua
uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi;
Mheshimiwa
Spika; kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha
John Mnyika (Mb)
John Mnyika (Mb)
Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara
ya Nishati na Madini
27/07/2012
No comments:
Post a Comment