To Chat with me click here

Tuesday, July 3, 2012

MADAKTARI BINGWA WAMJIBU KIKWETE

AGIZO la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na mgomo kuacha kazi limechukua sura mpya baada ya madaktari bingwa ambao awali hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi huyo wa nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini. Badala yake, madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao juzi, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka, walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapowarejesha kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa.

Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura jana na kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi wa mabingwa hao Dk. Catherine Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao.

“Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu… kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi.
“Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo.

Alisema hata wao hawana sababu ya kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na kuwaona Watanzania wakifa kwa kukosa vifaatiba na dawa. Dk. Mng’ong’o alisema madaktari hapa nchini wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa muda mrefu hivyo wakati wa kubadili hali hiyo umefika na kuwasaidia Watanzania maskini wanaotibiwa kwenye hospitali hizo.

  • Waomba kukutana na Rais
Madaktari hao walisema kuwa sasa wanaomba kukutana na rais ili kujadili hatima ya mgomo huo.“Tunamheshimu rais na mamlaka zote ila tunachoamini ni kuwepo kwa meza huru ya majadiliano kati yetu na yeye kwa sababu nafasi ya kumaliza kero hii anayo,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Dk. Godbless Charles alihoji sababu za kuwepo kwa taarifa tofauti kuhusu ongezeko la mishahara wakati waliishauri serikali kuwa wazi kuhusu nyongeza hiyo.

“Kumekua na majibu tofauti mfano Waziri wa Afya na UStawi wa Jamii aliliambia Bunge kwamba nyongeza ya mishahara ni asilimia 15. Hotuba ya rais Kikwete inasema nyongeza hiyo ni asilimia 20 wakati ripoti ya wataalam iliyokutana na kamati ya Waziri Mkuu ilipendekeza asilimia 25 je, nia ya serikali iko wapi?

“Wakati viongozi wa serikali wakitoa taarifa zinazotofautiana ripoti ya ufafanuzi wa madai na hoja za madaktari iliyotokana na majadiliano ambapo tulikuwa wajumbe hatukutoa pendekezo lolote juu ya ongezeko la mshahara,” alisema Dk. Godbless.

Alisema tangu kuanza kwa mgogoro kati ya madaktari na serikali jumla ya vikao sita viliketi kati ya hivyo vikao vinne vilijadili juu ya uboreshaji wa huduma za afya kwa watanzania. “Ni masikitiko yetu kuwa ripoti ya ufafanuzi wa hoja na madai yetu iliyotolewa Juni 31 mwaka huu, taarifa ya waziri wa afya, taarifa ya waziri mkuu ndani ya Bunge na hotuba ya rais haikuzungumzia kwa jinsi gani serikali itaboresha huduma za afya kwa watanzania,” alisisitiza Dk. Godbless.

Katika hotuba yake kwa wananchi rais Kikwete aliwataka madaktari wote waliogoma kuchakazi kwa kuwa viwango vikubwa vya mishahara wanaoitaka serikali haiwezi kuilipa.

No comments:

Post a Comment