Ikulu imesema kwamba mgomo wa Madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi ya kutibu binadamu, wamerejea kazini.
Aidha,
imesema kwamba sasa siyo wakati wa kulumbana tena, bali ni wakati wa
kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa
kujadiliwa.
Taarifa
ya maandishi ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilieleza hayo
jana baada ya kutakiwa kutoa kauli kuhusu ombi la baadhi ya viongozi wa
dini kutaka Rais Kikwete akutane nao, wanaharakati na madaktari kujadili
mgomo wa Madaktari.
Juzi,
baadhi ya viongozi wa dini nchini waliingilia kati mgomo huo wa
madaktari wakimwomba Rais Kikwete aitishe kikao nao ili kufanya
mazungumzo yatakayowashirikisha madaktari na wanaharakati kwa lengo la
kuondoa tatizo hilo.
Aidha,
wametaka wanaharakati na wanasiasa waache kushabikia na kuchochea mgomo
na badala yake washiriki kutafuta suluhu ya kweli kwa faida ya
Watanzania wote.
Mambo ya msingi
Taarifa
ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salvatory Rweyemamu kujibu
swali aliloulizwa na gazeti la HABARI LEO kuhusu ombi hilo la viongozi
wa dini, alisema mambo ya msingi kwa sasa ni manne.
“Kwamba
mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu
sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini. Hili ni jambo jema sana. Sasa
siyo wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya
kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa.
“Kwamba tokea madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, Serikali ilifanya jitihada kubwa za kukutana na madaktari hao.
Mbali
na Kamati ya Majadiliano ya Serikali, Madaktari pia wamekutana na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na
Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda. Kamwe, Serikali haijapata kukataa
kukutana na viongozi wa madaktari,” alieleza Mkurugenzi huyo.
Alieleza
kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hussein Mwinyi walikataa wakidai kuwa Waziri
hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.
“Huu ni ushahidi mwingine kuwa kamwe Serikali haijapata kukataa kukutana na kuzungumza na madaktari,” alieleza.
“Kwamba
mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa Serikali, akiwemo Rais,
hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na
wakakubaliwa. Hivyo, hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba
kukutana na viongozi wa Serikali,” Mkurugenzi huyo aliutaja msingi
mwingine.
Moja
ya hoja za madaktari hao waliogoma ni kutaka kulipwa mshahara zaidi na
Serikali na katika mapendekezo yao walitaka kulipwa Sh. milioni 3.5 kwa
mwezi kwa daktari anayeanza kazi; kiwango ambacho ukijumuisha na madai
mengine ya posho kinafikia Sh. milioni 7.7.
Rais
Kikwete katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi Juni, aliwaeleza
madaktari hao kwamba Serikali haina uwezo wa kulipa kiwango hicho, na
kwamba wako huru kutafuta mwajiri mwingine anayeweza kuwalipa, na hivyo
hawana sababu ya kugoma.
“Kama
daktari anaona kuwa hawezi kufanya kazi Serikalini bila ya kulipwa
mshahara huo (Sh. milioni 7.7) awe huru kuacha kazi na kwenda kwa
mwajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho,” alisema Rais Kikwete.
Kutokana
na ukweli huo, aliwatakia kila la heri wasioweza kufanya kazi
serikalini, lakini akaongeza kuwa “hana sababu ya kugoma ili ashinikize
kulipwa mshahara huo. Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo.” “Isitoshe,
hana sababu ya kuendelea kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa
kumlipa anachokitaka. Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa
kukuandikia barua ya kujieleza au kukuachisha kazi. Kwa nini upate
usumbufu wa kupata barua hizo na kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa
kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya
saa 24?,” alihoji.
Rais
Kikwete pia aliwaonya Madaktari hao kwa kuingia katika mgogoro na
Mahakama ambayo iliwapa amri kurudi kazini wakaikataa na mgogoro
mwingine na waajiri wao isivyostahili.
No comments:
Post a Comment