MBUNGE wa jimbo la
Ubungo, John Mnyika atakuwa ni mmoja wa mashahidi wa Serikali watakaoithibitishia
mahakama namna walivyohusika washtakiwa wanaotuhumiwa kumuua Mwenyekiti wa
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30).
Jeshi la Polisi
mkoani Singida, limemefikia azimio hilo baada ya kumhoji Mnyika kwa saa tatu
juzi usiku, kuhusiana na tukio hilo la mauaji lililotokea baada ya mkutano wake
wa hadhara uliofanyika Julai 14 mwaka huu, majira ya jioni.
Mahojiano hayo
yaliyoanza saa 11.53 jioni na kumalizika saa 3:15 usiku, yaliendeshwa chini ya
kikosi maalum cha askari wa upelelezi kutoka jijini Dar es Salaam kwenye ofisi
ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa.
Habari zilizolifikia
gazeti hili jana zilithibitisha kwamba Jeshi la Polisi lilimtaka Mnyika awe
tayari kuitwa wakati wowote ili kusaidia kwenye kesi hiyo ya mauaji. Tayari
watu 18 wametiwa mbaroni, miongoni wakiwemo wanachama wa Chadema, kwa tuhuma za
kuhusika kwenye mauaji ya kijana huyo wa CCM.
Mnyika alihojiwa huku
akiwa na wakili wa Chadema na mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Tundu
Lissu. Mauaji hayo ya mwenyekiti wa UVCCM yalifanyika Julai 14 mwaka huu saa 10
jioni huko katika kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.
Mauaji hayo yanadaiwa
kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na vurugu zilizotokea kwenye mkutano wa hadhara
ambao Mnyika alikuwa mgeni rasmi.
Katika hatua
nyingine, mshauri na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila
Mkumbo, ambaye alikuwa ameambatana na Mnyika, alitarajiwa pia kuhojiwa
kuhusiana na mauaji hayo jana.
No comments:
Post a Comment