To Chat with me click here

Sunday, July 29, 2012

KIGOGO WA POLISI ADAIWA KINARA WA DAWA ZA KULEVYA


MAPAMBANO ya kudhibiti dawa za kulevya nchini yanaelekea kugonga mwamba, baada ya baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi kudaiwa kuingia kwenye mtandao wa biashara hiyo haramu.

Vigogo hao wanadaiwa kushirikiana na askari wadogo, wakiwatumia kama wasambazaji wakuu wa bidhaa hiyo. Askari hao wanadaiwa kutumika kusambaza dawa hizo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga na Mara kwa kutumia pikipiki zao, huku vigogo hao wakiwalinda wasikamatwe.

Uchunguzi wa muda mrefu wa Mwananchi Jumapili, umebaini kuwa mtandao huo unamhusisha pia kigogo mmoja wa Makao Makuu ya Jeshi Polisi.
Kigogo huyo anadaiwa kumtumia mkuu wa kituo kimoja cha polisi mjini Mwanza, ambaye amepandishwa cheo kwa haraka kipindi kifupi, kupokea fedha kutoka kwa wasambazaji hao.

Msemaji wa Polisi
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alipoulizwa kuhusu suala hili hivi karibuni, alisema kuwa Jeshi la Polisi litaanza kufanyia uchunguzi wa kashfa hiyo baada ya kupata vielelezo.

Hata hivyo, Senso aliomba suala hilo aulizwe Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza ili atolee ufafanuzi kwa kuwa lipo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa hususan Mwanza.
"Suala hilo ninaweza kulijibu katika sehemu mbili, moja tukipata ushahidi mezani tutaanza kuufanyia uchunguzi. Pili, aulizwe Kamanda wa Mkoa wa Mwanza kwa sababu kwa sehemu kubwa, linahusu mkoa wake," alisema Senso.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alipoulizwa alisema kuwa hana taarifa za suala hilo akiomba apewe muda ili alifanyie kazi.

Alisema biashara ya dawa za kulevya ni hatari na kwamba, ni muhimu kwa jeshi lake kuzifuatilia ili kuidhibiti.
Imebainika kuwa mtandao huo unaratibiwa na kigogo mmoja wa Kituo cha Polisi Wilaya, mkoani Mwanza, ambaye hukusanya fedha kutoka kwa wahusika na kuwasilisha mgawo huo kwa kigogo mmoja wa Polisi Makao Makuu, ambaye tayari amemjengea nyumba ya kifahari jijini Mwanza. 

Wabebaji
Kwa mujibu wa uchunguzi, dawa hizo husafirishwa na polisi waliovalia sare kwa kutumia magari ya watu binafsi au pikipiki zinazotumika kubeba abiria maarufu kama bodaboda, hasa wale wa Kituo cha Mabatini wakiongozwa na askari mmoja (jina tunalo).

Askari huyo anayedaiwa pia kuwa na uhusiano wa karibu na maofisa wa
jeshi hilo kwa kuwa wanamtumia kuratibu shughuli hizo, awali alikuwa akitumia pikipiki ya kijana mmoja (jina tunalo), ambaye mwaka jana aligongwa na gari na kufa papo hapo katika maeneo ya Igombe nje kidogo ya Mji wa Mwanza.

Hata hivyo, kifo cha kijana huyo kinadaiwa kupangwa baada ya kubainika kuwa anafahamu mtandao huo na huenda angetoa siri kwa kuwa alikuwa tayari amehama katika ‘kijiwe’ alichokuwa akikitumia kukutana na askari huyo wa Kituo cha Mabatini.

Askari huyo alitumia pikipiki ya kijana huyo kupeleka dawa kwenye maduka ya wauzaji yaliyopo mjini Mwanza.

Uuzaji
Imebainika kuwa katika Jiji la Mwanza dawa za kulevya aina zote huuzwa kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi na vifaa vya umeme hasa vile vinavyotoka Dubai, ambapo huwekwa kwenye vifaa hivyo.
Baadhi ya vifaa vinavyowekewa dawa  hizo ni pamoja na masinki ya vyoo, ambapo mara nyingi wanunuzi hawatiliwi shaka kwa kuwa wanaingia kama wanunuzi wa vifaa hivyo.
Pia huuzwa maeneo ya gereji, kwenye magofu hasa maeneo ya Nyamanoro, Capri-Pointi, Mkunguni Kirumba (jirani na Kituo cha Polisi Kirumba, Bustani za Ghand Hall, Rwagasore, Nyegezi Stand, Igogo, Kamanga, Mbita, Uhuru, Liberty Kirumba Mwaloni, hata nyumba za wafanyabiashara ambao wamekuwa wakichangia shughuli za Serikali.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa ingawa kuna ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, wahusika hawakamatwi kwa sababu wamekuwa wakitumia mwavuli wa kuwa karibu na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Uingizaji dawa za kulevya
Magari ya wafanyabiashara watatu wa Kanda ya Ziwa yakiwamo mabasi na malori yao, ndiyo yamekuwa yakitumika kuingiza dawa hizo katika Jiji la Mwanza na miji mingine ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Magari hayo yamekuwa yakikamatwa mara kwa mara kutokana na taarifa za wasamaria wema, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa zaidi ya wahusika kurejeshewa magari yao na kuwaacha madereva wakishikiliwa kwa muda ili kupoteza lengo.

Miongoni mwa magari yaliyowahi kukamatwa na kuachiwa haraka, ingawa yalikuwa na shehena ya dawa za kulevya ni basi la mfanyabiashara mmoja lililokuwa limebeba kilo 600 za bangi Novemba mosi mwaka jana, eneo la Ramadi Wilaya ya Magu.

Kesi zake zakwamishwa
Mtandao huo umefanikiwa kukwamisha zaidi ya kesi 250 zenye vielelezo vya ushahidi, zilizo na watuhumiwa zaidi ya 80 waliokamatwa na dawa hizo katika Mkoa wa Mwanza.

Hata hivyo, kati ya kesi hizo 20 tu ndizo zilipelekwa mahakamani huku ikidaiwa kuwa polisi waliharibu ushahidi kutoita mashahidi mahakamani, hivyo zikafutwa.

Majalada ya kesi hizo 250 yaliwahi kulalamikiwa hadi ya Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, lakini askari waliolalamikia kitendo hicho, walijikuta wakihamishwa vituo vyao vya kazi.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na maofisa kadhaa wa polisi, wamekuwa wakitumia Tume ya Maadili ya Ofisi ya IGP kutoa tuhuma za uongo, zilizopikwa dhidi ya askari waadilifu walioonekana kukwamisha biashara hiyo.

No comments:

Post a Comment