Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameibua ufisadi mzito
unaofanywa na TANESCO na kuwaomba wabunge wasimame kidete ili
watuhumiwa wachuliwe hatua.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Kikwete, alifichua
ufisadi huo mbele ya waandishi wa habari mjini hapa, akisema kuwa
serikali imekuwa ikipoteza mabilioni ya fedha kulisaidia shirika hilo
wakati zinaishia mikononi mwa wajanja ambao ni menejimenti na Bodi ya
Wakurugenzi.
Tuhuma za Mbatia zinakuja ikiwa ni wiki mbili tangu Bodi ya
Wakurugenzi ya TANESCO iwasimamishe kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
hilo, William Mhando, na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu na
matumizi mabaya ya madaraka.
Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Robert Shemhilu, Ofisa
Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga, na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun
Matambo, walisimamishwa na bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jenerali
mstaafu, Robert Mboma, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Kwa mujibu wa Mbatia, wabunge wamekuwa wakifuatwa ndani na nje ya
Bunge na hata kwenye mahoteli walikofikia wakishawishiwa kuiunga mkono
TANESCO, jambo alilodai limewaingiza baadhi ya wenzao kwenye ufisadi.
Akifafanua kwa undani, Mbatia ambaye aliongozana na wabunge wote wa
chama chake, alisema kuwa mpaka sasa hawana imani na Kamati ya Nishati
na Madini kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake vile vile ni wajumbe kwenye
bodi ya TANESCO na wamekuwa wakitumika kuwarubuni wabunge wakingie kifua
ufisadi.
“Tulipokwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete kama chama kuzungumzia
mchakato wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Januari 21 mwaka huu…
tuligusia pia hali mbaya iliyokuwa ikiikabili TANESCO lakini Rais
alitueleza kuwa serikali imeipa ruzuku ya sh bilioni 136 ili
kuliwezesha,” alisema Mbatia.
Aliongeza kuwa kwenye bajeti ya mwaka jana, iliafikiwa kuwa TANESCO
itafutiwe mkopo wa sh bilioni 408 na serikali pia ikalipa deni lake la
sh bilioni 68 kwa shirika hilo pamoja na kulipatia mafuta ya sh bilioni
17.
Alisema kuwa mgogoro wa TANESCO ulianza kuibuka baada ya kuzushwa
uongo kuwa nchi inaweza kuingia gizani wakati wowote kutokana na hali
mbaya ya shirika, madai ambayo Mbatia alisema si ya kweli kwani ulikuwa
ni ujanja wa mafisadi kuzima kwa makusudi mitambo.
“Kisha TANESCO iliingia kwenye mchakato wa kutafuta wazabuni wa
kuiuzia mafuta mazito ya kuendesha mitambo yake ambapo ilifanya
mazungumzo na kampuni tatu zilizoonyesha kuwa tayari kuiuzia mafuta hayo
kwa sh 1,800 kwa lita,” alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, naye
alifanya mazungumzo na Kampuni ya Puma ambako serikali ina hisa za
asilimia 50 na kuafikiana kuwa inaweza kusambaza mafuta hayo kwa gharama
ya sh 1,460 kwa lita, bei iliyoonekana kuwa na unafuu zaidi.
Mbatia alifafanua kuwa pamoja na kampuni ya Puma kutokuwa kwenye
orodha ya zile zilizoomba zabuni hiyo, Maswi alitumia kanuni ya 42 (1)
ya mamunuzi ya umma inayompa mamlaka ya kuamua vinginevyo kwenye masuala
yenye maslahi ya umma kuipa zabuni hiyo hiyo.
“Kosa na kelele zote zimetoka hapo, mianya ya mafisadi imezibwa kwani
walitaka kuzipa zabuni kampuni za bei kubwa ili wavune sh bilioni tatu
ambazo zinaokolewa kila baada ya wiki mbili. Sasa kama kwa mwezi TANESCO
inaokoa sh bilioni sita kwa nini tumnyime zabuni huyu?” alihoji.
Mbatia alisema kwa mwezi Mei pekee TANESCO ilikusanya sh bilioni 85 na
matumizi yake kwa mwezi ni sh bilioni 11 ambapo kwa wastani wanapata
zaidi ya sh bilioni 60 wakiwa na ziada ya sh bilioni 50 kila mwezi.
No comments:
Post a Comment