SIKU chache baada ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed
Msangi, kudaiwa kuhusika kwenye sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, imeelezwa kuwa ofisa
huyo amewekewa ulinzi mkali.
Habari za ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa ofisa huyo anaishi kwa mashaka
kutokana na tuhuma nzito aliyotupiwa, hatua iliyowafanya wakuu wake kumpa
walinzi wawili wa kulinda usalama wake wakati huu ambapo uchunguzi unaendelea
chini ya tume maalumu iliyoundwa.
“Issue ya Dk. Ulimboka imemweka pabaya afande Msangi, anaishi kwa hofu sana
hadi kufikia hatua ya kupewa walinzi wawili,” kilieleza chanzo chetu cha
habari.
Hata hivyo, pamoja na kukiri kusikia tuhuma hizo ambazo amezikana, Msangi
ameviambia vyanzo vyetu vya habari kuwa, yeye hana hofu kwa kuwa anajua
hajafanya wala kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio la Ulimboka.
Alikanusha kupewa ulinzi, ingawa vyanzo vyetu vya habari vilishuhudia kwa
siku mbili akiwa ameambatana na watu wengine wawili kila alipokwenda, ingawa
alikiri kuwa ni askari wake na kwamba hilo ni jambo la kawaida.Kwa mujibu wa kanuni za kazi za polisi, Kamanda wa Polisi wa mkoa ama wa
Kanda Maalumu ndiye tu anayepewa ulinzi binafsi, lakini si mkuu wa upelelezi wa
mkoa.
JK, serikali imtese Ulimboka kwa lipi?
Rais Jakaya Kikwete, ameeleza kushangazwa kwake na tuhuma zilizotolewa na
baadhi ya madaktari na wana harakati kwamba serikali inahusika kumteka na
kumpiga kikatili mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari, Steven Ulimboka.
Katika hotuba yake jana kwa Watanzania, Kikwete pamoja na kuelezea
masikitiko yake makubwa na kuhuzunishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa
Dk. Steven Ulimboka usiku wa Juni, 26, 2012, alidai kushangazwa na tuhuma
kwamba serikali inahusika na ukatili huo, akisema haoni sababu ya msingi ya
kufanya hivyo, ikizingatiwa kuwa ndiye aliyekuwa kiungo muhimu baina ya
serikali na madaktari.
Kikwete alisema ingawa ni ukweli kwamba Dk. Ulimboka hakuwa mtumishi wa
serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano hayo na pia kulikuwa na
rai ya kutaka asiwepo, bado ndiye aliyeamuru aachwe aendelee kuwapo maadam
madaktari wenzake wamemuamini na anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao
wenyewe walioajiriwa na serikali.
Aliongeza kuwa kutokana na mwenendo wa mazungumzo ulivyokuwa ukiendelea,
hakukuwa na sababu za serikali kufikia hatua ya kumdhuru Dk. Ulimboka.“Kwa nini serikali imdhuru Dk. Ulimboka? Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi
na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Nimesema kuwa
ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana
shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa,” alisema.
No comments:
Post a Comment