•  Bilioni 200 zatengwa kuwalipa
SERIKALI imeamua kuagiza madaktari kutoka nchi za nje watakaochukua nafasi ya wale wa hapa nchini ambao wamegoma kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
SERIKALI imeamua kuagiza madaktari kutoka nchi za nje watakaochukua nafasi ya wale wa hapa nchini ambao wamegoma kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Habari kutoka katika moja ya vyanzo vya kuaminika zimesema kuwa uamuzi
 huo wa serikali ulipitishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri 
kilichokutana mjini Dodoma juzi chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya 
Kikwete.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilidai kuwa Rais Kikwete alikerwa 
na tabia ya madaktari kupingana na serikali licha ya juhudi zote 
zilizofanywa kuboresha maslahi yao.
Kwa mujibu wa habari hizo, kiasi cha sh bilioni 200 kimetengwa kwa 
ajili ya kuwaleta na kuwagharimia  madaktari hao wa nje na pia baraza 
limepitisha azimio la kuzungumza na hospitali za jeshi kama  Lugalo na 
zingine ndogo kubeba jukumu hilo kwa sasa pamoja kuagiza madaktari 
wastaafu wote warejee kazini katika kipindi hiki cha mgomo.
Habari zimedai kuwa madaktari hao wanasadikiwa watatoka katika nchi 
rafiki, zikiwemo India, China, Cuba na Afrika Kusini, na kwamba wataziba
 kikamilifu pengo la wale wa hapa nchini ambao wamegoma.
Inaelezwa kuwa mara baada aya kukamilika na kuanza rasmi kwa huduma za
 matibabu, madaktari wa hapa nchini waliomo katika mgomo na wale zaidi 
ya 200 waliodaiwa kufukuzwa na serikali kimyakimya, watalazimika  
kurejeshwa kazini kwa masharti makali.
Hata hivyo, uamuzi wa serikali  kuwatimua madaktari wakati suala lao liko mahakamani, umewagawa wabunge.
Baadhi ya wabunge walijaribu kuhoji suala hilo Bungeni, lakini 
walikwama baada ya Spika Anna Makinda  kuzuia mjadala huo kwa madai kuwa
 suala hilo liko mahakamani.
Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangala, alisema kuwa kilichofanywa na 
serikali ni kiini macho kwani juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda  alisema 
serikali  haiwezi kutoa kauli dhidi ya madaktari kwa madai kuwa kuna 
kesi mahakamani.
“Juzi serikali imesema kuwa haiwezi kutoa kauli kwa vile jambo hilo 
lipo mahakamani, sasa imewezaje kuwafukuza madaktari wakati jambo lipo 
mahakamani?” alihoji Dk. Kigwang’ala.
Aliitaka serikali kuondoa kesi hiyo ili kurejesha majadiliano kwani ndio njia pekee ya kukabiliana na mgogoro huo.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alimshangaa Spika Anna Makinda kuzuia 
mjadala huo kwani ungeweza kujadiliwa bila kuingilia uhuru wa mahakama.
Juzi uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,  uliwafukuza kazi 
madaktari 229 walioko katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na 
mgomo unaoendelea wa kushinikiza  kulipwa posho zao za mwezi mmoja.
Hospitali zingine ambako madaktari wamefukuzwa kutokana na mgomo huo ni pamoja na Mbeya na Dodoma.
Jeshi lachukua nafasi za madaktari
Wakati huo huo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeanza 
kutekeleza kwa vitendo agizo la serikali la kutoa huduma za kitabibu kwa
 wagonjwa kufuatia mgomo wa madaktari nchini. Juzi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa bungeni alisema serikali imeamua 
kuwatumia madaktari waliopo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wastaafu 
na hospitali zote za jeshi kuendelea kutoa huduma ya matibabu kwa 
wagonjwa.
Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe katika mahojiano maalum na 
gazeti hili, alisema juzi baada ya Waziri Mkuu Pinda kutoa agizo hilo, 
walianza utekelezaji wake ambapo kwa jiji la Dar es Salaam, hospitali 
Kuu ya Jeshi Lugalo Kikosi ya 521, Mgulani na ile ya Kikosi cha 
Navy-Kigamboni na hospitali zake zote kote nchini zilianza kutoa huduma 
hiyo bila vikwazo.
“Kwanza naomba umma uelewe hivi hospitali za JWTZ hapa nchini kwa 
asilimia 70 zimekuwa zikiwatibu raia bila vikwazo vyovyote hivyo agizo 
hilo la serikali huenda likaongeza idadi ya wagonjwa kutibiwa katika 
hospitali zetu labda kwa asilimia 90.
Mgawe alisema madaktari wanajeshi wapo kwa ajili ya kulinda taifa na 
watu wake, hivyo akawahakikishia wananchi wanaougua kutosita kwenda 
katika hospitali za jeshi hilo kutibiwa akidai kuwa hawaoni mantiki ya 
daktari kugoma.

 
 
No comments:
Post a Comment