TAMKO LA SERIKALI LA KULIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI
Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia
30 Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika
habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha
wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na
mshikamano uliopo nchini.
Katika matoleo yake
hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18,
2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la
Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa
yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii. Mhariri
wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri
kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na
maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote
katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu
ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30
cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali
imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi,
kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu
hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali
(Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa
jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai, 2012.
Serikali inawataka
wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili
ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha,
kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
Kama ilivyoelezwa
Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo hivi karibuni waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha
kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na
kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya
habari uendane na wajibu.
Kuanzia sasa Serikali
haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa
taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo
nchini mwetu.
Imetolewa na:
OFISI YA MSAJILI WA
MAGAZETI WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment