Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, hali ndani ya bunge jana jioni 
ilichafuka, baada ya mwenyekiti wa bunge, kushishwa kabisa kuongoza 
kikao hicho kufuatia kuzuka kwa malumbano makali baada ya Mkuu wa mkoa 
wa Iringa, Stella Manyanya kukituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo 
(CHADEMA) kuwa vinara wa mgomo wa madaktari.
  Manyanya alisema kuwa, CHADEMA wamebainika kuchochea mgogoro huo, hali
 iliyomfanya Mbunge wa Ubungo kusimama na kuomba mwongozo akimtaka 
Manyanya kuthibitisha ama kukanusha tuhuma hizo.
  Lakini katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Iramba mashariki Mwigulu 
Mchemba alisimama na kunukuu hotuba ya kambi ya upinzani, ambayo 
ilitamka bayana kuwa inaunga mkono madai ya watumishi wa serikali, na 
kwamba kwa kauli hiyo inadhihirisha bayana kuwa ndio wakuu wa mgomo huo.
  Badala ya kutoa mwongozo, Mabumba hakumtaka Manyanya kukanusha ama 
kuthibitisha alimruhusu Mchemba kuendelea kurusha makombora mazito dhidi
 ya CHADEMA, safari hii akidai kuwa ni vimbelembele kutoa matamshi ya 
kulaani kupigwa kwa Ulimboka huku, wakimwacha mmoja wa viongozi wake 
bila kumhudumia wala kumjulia hali.
  Katika kujichanganya kwa wabunge hao wa CCM, wakati Mchemba akidai 
kuwa CHADEMA ndio wachocheaji wakubwa wa mgogoro huo kwa kuwatumia 
madaktari, mwenzake Manyanya alitoa hoja safari hii akidai kuwa, ndio 
waliohusika na tukio la kumvamia na kumteka na kisha kumpiga Dk. 
Ulimboka.
  Hata pale Mnyika aliposimama na kuomba tena mwongozo wa mwenyekiti, 
huku akiweka bayana jinsi inavyoelezwa ushiriki wa maafisa wa polisi, na
 hata Dk. Ulimboka mwenyewe kuwataja wengine kwa majina, alimtaka 
mchangiaji kuthibitisha ushiriki wa CHADEMA kumjeruhi ama siyo afute 
kauli yake.
  Lakini kwa mara nyingine tena, Mabumba hakumtaka Manyanya wala Mchemba
 kuthibitisha kauli ama kufuta kama inavyofanywa kwa wabunge wa 
upinzani, badala yake alimruhusu mkuu huyo wa mkoa wa Iringa kuendelea 
na mchango wake bila kufuta kauli wala kuithibitisha.
  Kushindwa huko kwa waziwazi kwa Mwwenyekiti wa kikao hicho cha bunge, 
kuliwachefua wabunge wengi wa upinzani, huku wale wa CCM wakionekana 
kufurahia jambo hilo. 

 
 
No comments:
Post a Comment