VYAMA
vya CCM na Chadema vimetoa onyo kali kwa wabunge wanaotuhumiwa kwa kashfa ya
kuhongwa na baadhi ya kampuni za mafuta na kulihujumu Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), vikisema havitasita kuwawajibisha pindi tuhuma hizo
zitakapothibitika.
Kauli
ya vyama hivyo imekuja siku moja baada ya wabunge watano, watatu wa CCM na
wawili wa upinzani kudaiwa kuhusika na vitendo hivyo vya rushwa, ambavyo
vimesababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati
na Madini na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili majina ya wahusika yawekwe
hadharani.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa juu wa vyama hivyo walisema wanasubiri
kwa hamu taarifa rasmi kutoka bungeni.
CCM:
Rushwa adui wa haki
Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa alisema chama hicho kimewaapiza wanachama
wake wote kutotoa wala kupokea rushwa.
Alisema
rushwa ni kosa la jinai hivyo anaamini vyombo husika vya dola vitachukua hatua
zinazofaa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikazia kauli hiyo akisema rushwa
inaelezwa katika katiba ya chama hicho kwamba ni, ‘adui wa haki’ na wanachama
wote waliapishwa kuwa hawatapokea wala kutoa rushwa.
Alisema yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za CCM, anajiweka katika kundi la wasaliti wa chama.
Alisema yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za CCM, anajiweka katika kundi la wasaliti wa chama.
Alisema
wabunge ni kundi maalumu nchini ambalo linalipwa vizuri ili lisimamie vyema
misingi ya maendeleo ya nchi pasipo tamaa wala vishawishi hivyo wanapotajwa
miongoni mwa kundi la wala rushwa, CCM kinalaani vikali tukio hilo.
Kuhusu
tuhuma hizo kutajwa kuwahusisha wabunge watatu wa chama hicho, Nape aligoma
akisema habari hizo siyo rasmi, hivyo hawezi kuzizungumzia.
Hata
hivyo, alisema CCM kinasubiri uchunguzi ufanyike ambao ndiyo utakaoweka
bayana wahusika wa tuhuma... “Tusubiri uchunguzi ukamilike. Idadi
inawezekana ikawa hiyo au ikapungua au kuongezeka.”
Dk
Slaa: Hatufumbii macho ufisadi
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema: “Nalaani kitendo cha wabunge
kuhusishwa na ufisadi hasa ikizingatiwa kwamba Chadema tumekuwa tukiupinga
vikali. Tumekuwa tukipinga rushwa kwa sababu ndiyo inayoielekeza nchi pabaya…
Chadema hatufumbii macho rushwa.”
Alisema
tangu kuanza Bunge la 10, Chadema kimekuwa kikiona baadhi ya mambo
yanayoendelea katika mhimili huo muhimu wa dola yamejaa walakini... “Ndiyo
maana sisi Chadema tumekuwa tukisema Bunge limepoteza mwelekeo.”
Alisema
akiwa mtendaji mkuu wa chama, anasubiri taarifa kamili kutoka katika kikao cha
wabunge wa chama hicho ili kuweka wazi majina ya wahusika na kisha kufuatiwa na
kikao cha Kamati Kuu (CC) ambacho kitakaa na kuchukua hatua kali.
“Tunahitaji
tupate maelezo ya kina... chama chetu hakikurupuki… Nasubiri taarifa ya kokasi
ya chama. Katiba ya Chadema inatambua uwapo wa kikao cha wabunge wetu na kwa
bahati nzuri, kiongozi wake mkuu ni Mwenyekiti wa Chadema (Freeman Mbowe) na
katibu (David) Silinde ni mbunge wetu. Tunasubiri taarifa yao.”
Alisema
Chadema kina kanuni ya kudhibiti rushwa hivyo, mbunge wake akitajwa miongoni
mwa wanaohusishwa na rushwa, atawajibishwa kupitia kikao cha CC ya chama hicho.
NCCR-Mageuzi yakoleza moto
Katika
hatua nyingine, Chama cha NCCR- Mageuzi jana kilikoleza moto baada ya kumtaka
Spika Anne Makinda awataje wabunge hao bungeni ili wafukuzwe na kufungwa kama
Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inavyotaka.
Chama
hicho kimetoa wiki moja kwa Spika Makinda kufanya hivyo, kikionya kuwa
vinginevyo, chenyewe kitawasilisha hoja mahususi kutaka Bunge lichukue hatua
hiyo.
Mwenyekiti
wa chama hicho, James Mbatia alitoa tamko hilo mjini Dodoma, akisema
Sheria Namba 3 ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988, inataka
wabunge wanaothibitika kujihusisha na rushwa wafukuzwe na kufungiwa kwa kipindi
cha miaka mitano.
“Ni
aibu kwa Bunge, taasisi inayoitwa tukufu kuwa na mafisadi. Kitendo cha Spika
kukubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na kuahidi kuzivunja nyingine,
maana yake anakubali kuna mafisadi. Sisi tunamtaka atutajie wabunge hao bungeni
ndani ya juma moja,” alisema Mbatia.
Mbatia
aliyeongozana kwenye mkutano huo na wabunge Moses Machali wa Kasulu Mjini na
Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini), alisema pamoja na Bunge kuendeshwa kwa
kanuni zake, kwa Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola inaweza pia
kuiga yaliyofanywa katika nchi nyingine za jumuiya hiyo, zikiwamo India
na Uingereza.
Kwa
mujibu wa Sheria zinazotumika katika nchi hizo, mbunge yeyote anayethibitika
kutumwa na mtu nje ya Bunge, kuongea au kuandika bungeni kwa masilahi ya mtu
huyo, anapaswa kufukuzwa ubunge na kufungwa.
“Kati
ya mwaka 1924 na 1956, Uingereza ilifukuza wabunge 59 na kati ya mwaka 2005
hadi sasa, Bunge la India liliwafukuza wabunge 11 baada ya kuthibitika
walihongwa na wafanyabiashara kuuliza maswali binafsi,” alisema.
Mbatia
aliendelea kueleza kuwa katika Bunge la Nane nchini, wabunge wanne walikamatwa
na kushtakiwa, kisha chama chao CUF, kiliwazuia kujihusisha tena na siasa baada
ya kubainika kuwa walifunga ndoa batili na Wasomali ili wapate hati ya kuishi
nchini.
“Sasa
suala hili, wabunge wote wanaohisi wamo kwenye orodha hii ya ufisadi waachie
ngazi. Mbunge yeyote na wa chama chochote anayeona ameshiriki uchafu huu, kwa
utashi wake aachie ngazi,” alisema na kuongeza:
“Kwa
vile vyama viadilifu, waige mfano wa CUF. Bunge lichukue nafasi yake kabla
hatujafunga Bunge Agosti 18 tuwe tumefanya uamuzi wa kuwafukuza.”
Mbatia
alisema ili Bunge lilirudi kwenye heshima yake, Spika Makinda pia anapaswa
kuzitaja kamati nyingine alizosema zinachunguzwa na ikiwezekana nazo zivunjwe
ili haki itendeke.
“Sisi
(NCCR-Mageuzi) tunataka pia Spika azitaje kamati hizo, ziko sita na tuseme pia
kwamba hatuna imani na Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge. Tunataka
nayo ijisafishe kwanza kwa kuwa nako kuna watuhumiwa.”
“Katika hili niombe kiti cha Spika kitende haki, hata kama kuna mbunge wa NCCR-Mageuzi anahisi alishiriki ufisadi huu, awahi mapema kuondoka, hii isiwe kwa vyama vingine tu,” alisema.
Mbatia
alisema suala la Tanesco ni tone tu, akisema ufisadi kwa wabunge ulianza siku
nyingi na kuongeza... “Mheshimiwa Kafulila (David) aliwataja wajumbe wa Kamati
ya LAAC lakini, mpaka leo hakuna kinachoendelea.”
Alisema
tatizo la ufisadi kuhusisha wabunge lilianza Juni 23, 2006 siku ambayo nchi
iliingia mkataba na Kampuni ya Richmond... “Kuanzia hapo kumeendelea kuwa na
sintofahamu katika Wizara ya Nishati na Madini. Dawa yake ni kuweka mikakati ya
Bunge kujitakasa.”
Sakata
lenyewe
Wabunge
hao watano (majina tunayahifadhi kwa sasa) wanatuhumiwa kutumia nafasi zao za
uwakilishi bungeni au ujumbe ndani ya kamati husika, kufanya biashara na
Tanesco na kutetea mafisadi wanaolihujumu shirika hilo kutoka ndani na nje.
Hata
hivyo, baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni walisema wanawafahamu
wabunge hao kwa majina, lakini wasingependa kuwataja kwa kuwa siyo wakati
mwafaka.
Moto
wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa na Mbunge wa Namtumbo
(CCM),
Vita Kawawa ambaye aliomba Spika avunje Kamati ya Nishati na kutaka pia Bunge lijadili kashfa hiyo.
“Waheshimiwa
wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa Kifungu cha
55 (3) f, Mbunge au Waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe.
Sasa
mimi naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo.”Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono
na idadi kubwa ya wabunge , ndipo Spika Makinda aliposimama na kukubali hoja
hiyo ya Mbunge Vita Kawawa na kutangaza kuivunja kamati hiyo.
Spika
Makinda alisema tayari pia, ameagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea
rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
“Nasema kwa dhati kabisa kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge. Wabunge mkae vizuri, kama kuna baadhi yetu wanakwenda huku na huku kujitafutia masilahi binafsi mnawezaje kuisimamia Serikali?”
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema ameshtushwa na
uamuzi huo wa Spika na kwamba anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge.
Akihitimisha
hoja ya wizara yake bungeni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alisema baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi vya
Tanesco kama wajumbe wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia mbalimbali
ikiwamo kufanya nalo biashara.
“Shirika
liliwahi kulipa Paundi 50,000 za Uingereza kwa ajili ya ununuzi wa vipuri,
lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari. Nguzo hizo za umeme kuna
biashara inaendelea. Tunajua kwamba nguzo hizo zinazalishwa Iringa na kupelekwa
Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka Afrika Kusini,”
alisema Profesa Muhongo.
No comments:
Post a Comment