Ofisi ya Waziri
Mkuu imejibu uongo bungeni kuhusu uwepo
wa mgogoro kati ya Serikali na walimu hivyo nakusudia kumwandikia Spika aagize
swali hilo lijibiwe kwa ukweli na ukamilifu.
Tarehe 11 Julai
2012 wakati nikiuliza swali la nyongeza kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya
walimu watumishi wa umma katika Jimbo la Ubungo na nchi kwa ujumla kuwa ni lini
serikali itakamilisha kushughulikia madai ya walimu kwa kuwa matatizo ya walimu
yamedumu kwa miaka mingi kwa kiwango cha kufikia hatua ya walimu kutangaza
mgogoro na serikali.
Akijibu swali langu
kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Majaliwa Kassim Majaliwa
hakueleza kwa ukamilifu ni lini serikali itakamilisha kushughulikia madai ya
walimu badala yake akatoa majibu ya uongo kuwa walimu hawajatangaza
mgogoro na serikali.
Hata hivyo, ukweli
ni kuwa walimu wametangaza mgogoro na serikali na ushahidi ni tamko la
Serikali yenyewe kuhusu migomo sehemu za
kazi lililotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira tarehe 9 Julai 2012 ambalo limeeleza kuwa tayari
Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kwa niaba ya walimu nchini kimeishawasilisha
mgogoro katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi- Dar es salaam wenye usajili
CMA/DSM.ILA/369/12.
Hivyo, naendelea
kusisitiza serikali ichukue hatua ya kushughulikia vyanzo vya migogoro na
watumishi wa umma badala ya kusubiri mpaka matokeo ya migogoro kama migomo na
madhara mengine kwa nchi na wananchi ndio ianze kutumia nguvu kuidhibiti.
Migogoro kati ya
serikali na watumishi wa umma ina athari kubwa; wakati migogoro ya madaktari
huchangia katika kuathiri hali na uhai wa wagonjwa, migogoro kati ya serikali
na walimu inachangia katika kudidimiza ubora wa elimu na kuathiri maisha ya
wanafunzi.
Na wabunge tupewe nafasi ya kuishauri na kuisimamia
serikali kwa mujibu wa mamlaka ya bunge ya ibara ya 63 (2) na (3) kwa kuletewa
taarifa sahihi na pia kujibiwa maswali kwa ukweli na ukamilifu kabla ya
serikali kwenda mahakamani baada ya majadiliano yake na watumishi wa umma
kukwama kama ilivyotokea kwa madaktari.
Aidha, Spika
aliwezeshe bunge kupokea taarifa maalum ya kamati ya bunge ya huduma za jamii
kuhusu madai ya watumishi wa umma ambayo mengi chanzo chake ni ufinyu wa bajeti
ili katika mkutano huu wa bunge la bajeti unaoendelea bunge liweze kujadili na
kuisimamia serikali kushughulikia vyanzo vya migogoro badala ya matokeo.
John
Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
13/07/2012
No comments:
Post a Comment