MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka 18
jela Kada wa CCM, Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein katika kesi
ya tuhuma za kuchota Sh2.2 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya
Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Mahakimu wawili katika jopo la waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo waliwatia hatiani
watuhumiwa kwa makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili na kuwahukumu
kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa. Kwa upande wake kiongozi wa jopo
hilo, Jaji Fatuma Masengi aliwaachia huru washtakiwa hao kwa maelezo kwamba
upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote saba yaliyokuwa yanawakabili.
Hata
hivyo, hukumu hiyo haikuweza kuwaokoa watuhumiwa na hasa Farijala na Maranda
watatumikia adhabu yao kwa miaka mitatu jela kwa kuwa adhabu zote walizopewa
zitakwenda kwa wakati mmoja. Tayari Maranda na Farijala wanatumikia kifungo
kingine cha miaka mitano jela, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8
bilioni za EPA, ambapo walihukumiwa na mahakama hiyo Mei 23, 2011. Jopo
lagawanyika Jopo la mahakimu watatu lililokuwa likisoma hukumu hiyo
liligawanyika na kusoma hukumu mbili tofauti, ambapo hukumu moja iliyoandaliwa
na kusomwa na kiongozi wa jopo hilo, Jaji Masengi aliyewaachia huru washtakiwa.
Hata
hivyo, katika hukumu ya pili, iliyoandaliwa na Hakimu Projestus Kahyoza na
mwenzake Catherine Revocate iliwatia hatiani washtakiwa katika makosa sita kati
ya saba yaliyokuwa yakiwakabili, na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu kwa
kila kosa. Hata hivyo, wakati wakisoma hukumu hiyo, mahakimu hao walisema
badala ya washtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 18, hukumu yao itaenda
sambamba hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Kabla ya hukumu Kabla
ya hukumu hiyo kutolewa, hakimu Kahyoza na mwenzake walipitia ushahidi
uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashtaka akiwamo mtaalamu
wa maandishi, Joseph Mgendi ambaye aliweza kuangalia saini katika nyaraka
halisi na zinazodaiwa kughushiwa, ikiwamo hati ya usajili ambapo
alibainisha kuwa zilikuwa zimeghushiwa.
Pia walipitia utetezi
uliotolewa wa mshtakiwa Maranda, ambaye aliyakana mashtaka yote saba
yanayowakabili na kwamba, alikataa katakata kuwa hakuwahi kula njama na
kughushi hati ya usajili wa Kampuni ya Money Planners & Consultant. Hakimu
Kahyoza alisema, Maranda alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda Brela kusajili
kampuni hiyo na kwamba, aliyewahi kwenda kusajili kampuni ni binamu yake,
Farijala. Hakimu Kahyoza alisema, Maranda katika utetezi wake alisema yeye
hakuwahi kughushi hati yoyote hivyo, haikuwa rahisi kwake kutoa hati
iliyoghushiwa pia, hakuwahi kuiba fedha BoT na wala hakuwahi kujipatia fedha
yoyote kwa njia ya udanganyifu. Kahyoza alifafanua kwamba, Maranda alidai mfumo
uliotumika kuwaingizia fedha kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CBA uliendeshwa
kihalali ndiyo maana, BoT hawakuwahi kulalamika hivyo, aliiomba mahakama imuone
hana hatia.
Akisoma utetezi
uliotelewa na Farijala, Hakimu Kahyoza alisema, Farijala naye alikataa
madai ya kughushi, kuwasilisha nyaraka bandia benki, kuiba fedha yoyote na
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na aliiomba mahakama imwachie huru kwa
sababu hana hatia. Yasiyo na utata Hakimu Kahyoza alisema kuwa mahakama
ilibaini kuwapo kwa masuala yasiyokuwa na utata ambayo ni pamoja na kwamba
Maranda na Farijala ni ndugu, waliwahi kufanya biashara pamoja na waliingiziwa
fedha kwenye akaunti namba 0101379004 ya United Bank of Africa ambazo ni kiasi
cha Sh2.2 bilioni. “Baada ya kuweka msingi huo, mahakama ilijiuliza je,
washtakiwa walikula njama ya kuiibia BoT, walighushi hati ya usajili wa
kampuni namba 150731, walighushi hati ya mkataba kati ya Kampuni ya Money
Planners & Consultant na Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani,
waliwasilisha nyaraka za kughushi benki, waliibia BoT na kwamba je, walijipatia
fedha kwa njia ya udanganyifu,” alihoji Kahyoza.
Hakimu huyo alisema
kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, hakuna utata kuwa hakuna mahali
panapoonyesha washtakiwa ndiyo walikuwa wamiliki wa kwanza wa kampuni hiyo
Money Planners & Consultant na kwamba majina yanayodaiwa kuwa ni wamiliki
wa kampuni hiyo ya Thobias Kitunga na Paulo ni majina ya
uongo na ya kufikirika. Alisema licha ya majina hayo kuwa ya kufikirika,
mabadiliko ya kampuni hiyo ya Money Planners & Consultant hayakuwahi
kufanyika na hata Brela hakuna kumbukumbu, hivyo saini zilizopo katika nyaraka
za kampuni hiyo ikiwamo hati ya usajili ni za kughushi. Alisema sababu ya
kuthibitisha hilo ni kwamba, ofisi ni ileile iliyopo Magomeni Mapipa, Mtaa wa
Iramba nyumba namba 7 hata baada ya mabadiliko. “Hati hizo za usajili
hazikusainiwa na Msajili wa Biashara toka Brela, Noel Shani bali zilisainiwa na
washtakiwa wenyewe. Hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 333 na 335 (c) (e)
vimetufanya tufikie hitimisho kuwa washtakiwa walighushi nyaraka hizo,”
alisema Hakimu Kahyoza.
Alisema Maranda na
Farijala walighushi hati ya mkataba ya Septemba 8, 2005, wakitumia majina ya
Thobiasi na Paul na kwamba hati hiyo haikusainiwa na Kampuni ya Money Planners
& Consultant. “Maombi ya kupewa fedha hizo Sh 2.2 bilioni, yalipitiwa
na watu kadhaa wakiwamo Mwanasheria wa BoT na kupeleka kibali cha mwisho
kwa Gavana aidhinishe malipo, hakuna hata mmoja aliyebaini kuwa katika hati ya
mkataba kati ya Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani na Kampuni ya Money
Planners & Consultant, haikuwa na saini ya Kampuni ya Money Planners
& Consultant,” alisema. Aliongeza: “Kwa sababu hiyo inaonyesha wazi,
washtakiwa ndiyo walighushi nyaraka hizo hivyo hati ya usajili wa
kampuni hiyo, hati ya mkataba ni za kughushi.” “Tuna haki ya kuamini kuwa washtakiwa
kwa kujua, walifanya hivyo kwa nia mbaya ya kuwasilisha hati hizo za kughushi
CBA na baadaye BoT”, alisema Kahyozi. Alisema hakuna ubishi kuwa hakuwapo hata
shahidi mmoja aliyewahi kuthibitisha kuwa washtakiwa hao waliwahi kuiibia BoT
Sh 660,210,000.
“Katika hili hatupo
tayari kukubaliana na upande wa mashtaka kwa sababu halijathibitika”. Aliongeza
kwamba, hakuna utata kuwa BoT iliweka kwenye akaunti ya washtakiwa zaidi ya
Sh2.2 bilioni na kwamba, kiwango hicho cha fedha kiliwekwa baada ya washtakiwa
kuwasilisha hati za kughushi katika benki hiyo kuu ikiwamo hati ya
usajili na hati ya mkataba. Hakimu alisema kulikuwapo na maofisa wa juu
BoT waliotakiwa walithibitishe hilo, lakini, Mwanasheria wa BoT yeye alikuwa
anathibitisha uhalali wa hati hiyo ya mkataba ambayo haikusainiwa upande mmoja
na Kampuni ya Money Planners kuwa, “Ina nguvu kisheria hivyo, inaweza
kutumiwa na BoT kuhamisha au kuchukua fedha zinazoongelewa katika
maombi ya washtakiwa”. Alifafanua hakimu, “Mwanasheria alimaanisha kuna watu
wengine walithibitisha, sisi kwa mtazamo wetu ni ajabu kwa maofisa hao
hata mmoja hakuwahi kuona katika hati ya mkataba hakuna saini ya Kampuni ya
Money Planners. Tunajiuliza walimezwa katika huu mtego au walipumbazwa? Kama
walipumbazwa, upumbazo huo ulikuwa ni wa hali ya juu na kujikuta wote wanaingia
kwenye mtego huu.” alisema Hakimu Kahyoza.
Aliongeza kwamba
washtakiwa hao walifanya matendo hayo yote kwa nia mbaya na kuwafanya watu
wengine, wawe sehemu ya kughushi. Kuhusu shtaka la kula njama, kwa ujumla
maelezo yote yanaonyesha Maranda na Farijala, walikubaliana makazi
ya ofisi yawe Magomeni, Mtaa wa Iramba nyumba namba 7 ambako ni nyumbani kwao,
waliwasiliana, walikutana, walijadiliana hivyo walitenda kosa la kula
njama. “Sisi hatuna sababu za kusitasita kuwa kweli washtakiwa walikula njama
dhidi ya BoT. Ni kweli walikula njama,” alisisitiza Kahyoza. Jaji Masengi Kwa
upande wake, Jaji Masengi aliwaachia huru washtakiwa wote kwa sababu upande wa
mashtaka ulishindwa kuyathibitisha mashtaka yote saba yanayowakabili. Jaji
Masengi alisema BoT ndiyo wangekuwa walalamikaji wakuu, lakini haikuwahi
kulalamika kutoa fedha hizo zinazodaiwa kuibwa na washtakiwa wala Kampuni ya B.
Grancel ya nchini Ujerumani.
Kuhusu kughushi,
alisema ushahidi uliotolewa haukutosheleza kuthibitisha kosa hilo na kwamba
licha ya utetezi kuwa na upungufu lakini hakukuwa na sababu za kuwatia hatiani.
Kabla ya hukumu Kabla ya kusomwa kwa hukumu ya Hakimu Khayoza na Hakimu
Catherine, Wakili wa Serikali, Alapha Msafiri aliiambia mahakama kuwa
washtakiwa siyo wakosaji wa mara ya kwanza, wanatumikia kifungo cha miaka
mitano jela katika kesi namba 1161 ya mwaka 2008. Msafiri aliiomba mahakama
itumie kifungu cha 348 na 358 cha Makosa ya Jinai (CPA), kutoa amri Maranda na
Farijala walipe fidia au warejeshe kiasi walichojipatia kwa njia ya
udanganyifu. Wakili Majura Magafu, anayewatetea Maranda na Farijala, alidai
kuwa ni kweli washtakiwa walitiwa hatiani lakini, isiwe kigezo
cha kuwapa adhabu kali kwa sababu kesi namba 1163 na 1161 zilifunguliwa
siku moja, zinahusu makosa ya aina moja isipokuwa zilipangiwa jopo tofauti.
“Hii ni tofauti na mtu aliyetenda kosa akaachiwa halafu akafanya tena kosa
lingine, pia mazingira ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa yalikuwa na utata
kwa namna moja au nyingine na kwamba washtakiwa walitenda makosa bila ya kujua
kama wanatenda makosa,” aliwatetea wakili huyo na kuongeza: “Kwa hiyo ni
dhahiri, matukio hayo hayakufanyika kwa makusudi kwa asilimia 100, kwa kuwa wao
waliamini ni halali lakini baadaye ilibainika kuwa si halai”.
“Waheshimiwa
washtakiwa wote wana matatizo ya kiafya, Farijala ana matatizo ya presha ya
macho na Maranda ana tatizo la Figo, naomba kama mahakama itaridhia chini ya
kifungu cha 38, ina mamlaka ya kuangalia mazingira ya utendwaji wa matukio,
hali za watuhumiwa na kuwaachia kwa masharti maalumu kutokana na
afya zao,”alisema Magafu. Pia aliiomba mahakama itamke wazi wazi kuwa adhabu
watakayopewa washtakiwa kama itakuwa ni ya kifungo, inastahili kuanza lini kwa
sababu kumekuwapo na utata wa sheria, kuwa ni lazima wamalize kifungo cha awali
ndiyo waanze kingine. Kwa upande wa Hakimu Catherine Revocate, alisema
wamejadiliana kwa kuangalia mazingira ya kesi, afya za washtakiwa
na kwamba ni wakosaji wa mara ya kwanza kwa sababu kesi hiyo inasimama peke
yake, katika shtaka la kwanza hadi la saba kasoro shtaka la sita waliloachiwa
huru; washtakiwa hao watatumikia kifungo cha miaka mitatu katika kila kosa.
No comments:
Post a Comment