Kamanda wa polisi mkoa wa Singida,Linus Vicent Sinzumwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) kutokana na vurungu zilizotokea kati ya wafuasi wa CHADEMA na CCM huko mkoani Singida.
Jeshi
la polisi mkoa wa Singida linawashikilia wakazi 18 wa kata ya Ndago
jimbo la Iramba magharibi kwa tuhuma ya kumuua mwenyekiti wa umoja wa
vijana CCM (UVCCM) Yohana Mpinga (30) baada ya kumpiga kwa kutumia
silaha za jadi.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoa wa Singida Linus Vicent Sinzumwa amesema tukio
hilo la kusikitisha limetokea Julai 14 katika kijiji cha Ndago.
Amesema
siku ya tukio, Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) kilikuwa na
kibali halali cha kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hicho cha
Ndago na mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa mbunge wa jimbo la
Ubongo jijini Dar-es-salaam Mhe. John J. Mnyika.
Mbali
na Mnyika, viongozi wengine wa Chadema waliokuwapo ni Mjumbe wa Kamati
Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano
wa chama hicho, Mwita Waitara.
Sinzumwa
amesema mara baada ya CHADEMA kuanza mkutano huo, viongozi wake
walianza kuporomosha mvua ya kashifa mbalimbali dhidi ya mbune wa jimbo
hilo Mwingullu Nchemba, kitendo ambacho kiliudhi baadhi ya watu
waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.
Kamanda
huyo amesema kuwa vurugu hizo zilihusisha kundi la wanachama wa CHADEMA
na wa CCM na zilisambaa ambapo wanachama hao walianza kurusha mawe ovyo
na askari wachache wa polisi waliokuwepo, walizidiwa nguvu na makundi
hayo.
Amesema katika kundi hilo ambalo wamelikamata,watawahoji na wataobainika kuhusika watafikishwa mahakamani wakati wowote.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mwita alidai mbali na mkutano huo kuwa na
baraka za Polisi, lakini pia walikuwa na taarifa juu ya mpango wa
kuvurugwa mkutano huo. Alidai
waliwatahadharisha askari waliokuwapo kwenye eneo hilo kuwa kuna vijana
ambao walikuwa wameandaliwa kufanya fujo ili kuhakikisha kuwa mkutano
huo haufanyiki.
Kwa
mujibu wa madai ya Mwita, taarifa hizo zilieleza kuwa kuna kikundi cha
vijana kilichokuwa kimeandaliwa na kununuliwa pombe pamoja na kukodiwa
gari ili kiharibu mkutano huo kwa kuhakikisha haufanyiki. Alidai
pamoja kutoa taarifa hizo, hakuna hatua yoyote ya makusudi
iliyochukuliwa na Polisi waliokuwapo karibu na eneo la mkutano, hali
iliyosababisha fujo kutokea mara tatu kabla ya mkutano huo kuendelea na
kukamilika salama na wao kuondoka katika eneo hilo.
“Lakini
kutokana na vurugu zilizokuwa zikisababishwa na kikundi cha vijana
ambao tayari walishatolewa taarifa yao kwenye mkutano huo mbele ya
Polisi, askari waliokuwapo hawakuthubutu kuchukua hatua kwa vijana
wale,” alidai Mwita. Alidai
wakati wakiendelea na mkutano huo na baada ya kutoa taarifa kwa OCD na
RPC, askari waliokuwa tayari kuzuia fujo walifika, lakini tayari fujo
zilishatulia na mkutano uliendelea kama kawaida.
Kutokana
na fujo hizo ambazo Mwita alidai zilitokea mara tatu, waliamua kufungua
jalada Polisi lenye namba NDG/RB/190/2012 na katika jalada hilo
walitaja majina ya watu waliokuwa wakifanya fujo mbele ya mkutano huo
kwa lengo la kufanya mkutano huo usifanyike.
Aliwataja
watu aliodai waliohusishwa na fujo hizo na walionaswa na kamera
zilizokuwa zikitumiwa kuchukua kumbukumbu ya mkutano huo kuwa ni Daniel
Sima, Tito Nitwa, Bakili Ayubu, Yohana Makala Mpande, Ernest Kadege,
Abel John, Athumani Ntimbu, Martin Manase, James Ernest, Simon Makacha,
Anthon John na Frank Yesaya.
“Kwa
hakika askari wa Ndago waliokuwepo mkutanoni mbali ya kutochukua hatua
yoyote, fujo za sisi kupondwa mawe zilizidi, askari wote walikimbia
akabaki OCS pekee ambaye naye alionekana dhahiri kutochukua hatua
stahili,” alidai Mwita.
Alisema
mpaka wanaondoka katike eneo la mkutano hakukuwa na taarifa yoyote juu
ya fujo ilizosababisha mtu kupoteza maisha na waliendelea na mkutano
mwingine katika Kijiji cha Kinampanda na waliporudi hotelini walipofikia
jioni mjini Singida walianza kusikia taarifa zinazoeleza kuwa kuna mtu
au watu wamepoteza maisha katika mkutano wao wa kwanza.
Mwita
alidai Chadema inalaani taarifa zilizosambazwa kuwa chama hicho
kinahusika katika kupoteza maisha ya mtu huyo kwani hakikujihusisha kwa
aina yoyote katika kufanya fujo na muda wote kilikuwa kikiomba msaada
kutoka kwa askari ili kutuliza fujo hizo.
Alisema
kutokana na habari zinazosambazwa kwa kuihusisha Chadema, kuwa
kinahusika katika kupoteza maisha ya mtu huyo, chama hicho kimebaini
kuwepo mbinu chafu ya kuvihusisha vyombo vya Dola katika kuwatisha
wananchi ili wasikiunge mkono katika kuleta mabadiliko ya kweli ndani ya
jamii.
Alisema
tayari chama chake kimeshapokea taarifa kutoka Jeshi la Polisi ya
kusitishwa kwa ziara yake ambayo kwa jana ingefanya mikutano miwili
katika kijiji cha Shelui na Kiomboi na wanatii amri hiyo.
No comments:
Post a Comment