WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda juzi jioni alifanya kazi ya ziada kuzima
hasira za wabunge waliokuwa wakitaka kuona Waziri wa Nishati na Madini,
Pofesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi,
wakiwajibika kwa kujiuzulu nyadhifa zao vinginevyo wangekwamisha bajeti
ya wizara hiyo.
Habari ambazo Tanzania Daima, imezipata zinadai kuwa wabunge hao
walidhamiria kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka
2012/2013 inayotarajiwa kusomwa bungeni leo.
Chanzo cha habari hizo kilidai wabunge walifikia hatua hiyo baada ya
vigogo hao kuripotiwa kuwa waliruhusu ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya
umma kwa kuipa zabuni kampuni ya Puma Energy (T) Ltd zamani BP.
Kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya
kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kuziweka
kando kampuni zilizokuwa zimechaguliwa kupitia mchakato halali wa
zabuni ya TANESCO.
Suala hilo linahusishwa na kusimamishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa
TANESCO, William Mhando, kwamba alichukuliwa hatua baada ya kukataa
kutii maelekezo ya wizara.
Katika kikao cha juzi usiku cha wabunge wa CCM, kilichoongozwa na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wabunge hao walikuwa na msimamo wa
kumuwajibisha Muhongo na Maswi.
Wakati wabunge wakiwa na msimamo huo, Pinda aliingia akiwa na lengo la
kuilinda serikali na chama kinachotawala (CCM).
Pinda alidai kuwa kumshinikiza Rais Kikwete amuwajibishe waziri
aliyemteua miezi mitatu iliyopita ni kutomtendea haki na kuuonyesha umma
kuwa hakufanya chaguo sahihi.
Tanzania Daima, ilidokezwa kuwa wajumbe wote walikubaliana kwamba
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini alifanya makosa na alivunja sheria.
Wabunge wa CCM walitaka Maswi na Muhongo watoswe ili kujenga heshima ya serikali na kusimika utawala wa sheria.
Inadaiwa kuwa kulikuwa na wabunge waliopangwa kimkakati kushawishi
wenzao wasiisulubu serikali kwa kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini
leo.
Miongoni mwa wabunge wanaotajwa ni Waziri Mkuu Pinda, William Lukuvi,
Jenista Mhagama na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage.
Inadaiwa kuwa Mwijage ana maslahi katika Puma Energy iliyopewa zabuni
ya kuiuzia mafuta IPTL na Maswi.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka, anadaiwa kutaka iundwe
kamati teule ya Bunge kuchunguza uozo ulio ndani ya wizara na TANESCO.
Baadhi ya wabunge wakasema wazo lake ni sawa, lakini katika mazingira
ya sasa ya kisiasa ya CCM, tume itaibua uchafu mwingi ambao utaimaliza
serikali mbele ya umma.
Sendeka alisema: “Mbona katika sakata la Richmond iliundwa kamati
iweje hivi sasa isiundwe wakati kosa la Maswi linafanana na la Lowassa?”
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, inasemekana alijenga hoja
kuwa CCM na serikali walifanya makosa kwenye sakata la Richmond ambalo
lilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kuachia ngazi.
“Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana, na sasa makosa yetu
yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale yale, tuwaache hawa
kwa maslahi ya CCM,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe walishikilia msimamo wa kuwajibishwa kwa
Muhongo na Maswi kwa madai kuwa endapo wataachwa, wataimaliza serikali
ya CCM.
Walisema kuwaacha ni sawa na kulitangazia taifa kwamba wao ni wavunjaji wa sheria walizozitunga wenyewe.
Tanzania Daima imeelezwa kuwa hata hivyo hatimaye wabunge hao
walikubaliana kwa shingo upande kuwa msimamo wa wabunge wa CCM ni
kulinda chama na serikali.
No comments:
Post a Comment