MBUNGE wa
Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amehoji hatua zinazochukuliwa na serikali
dhidi ya makandarasi waliofanya uzembe na kusababisha mradi wa
miundombinu ya maji uliofanywa na Wachina katika maeneo mengi ya Jiji la
Dar es Salaam kutofanya kazi hadi hivi sasa.
Alitoa kauli
hiyo Bungeni jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza ambapo
alisema kwamba hatua hiyo imewasababishia adha wananchi. Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Maji Dk. Binilith Mahenge alisema kuwa mradi
huo ulikuwa na awamu nne na tayari awamu 3 zimeshapita hivyo katika
utekelezaji wa awamu ya nne watahakikisha wanaangalia tatizo
lililosababisha mradi huo kuchelewa kuanza kufanya kazi.
Awali katika
swali la msingi la mbunge wa Viti maalum, Rita Mlaki (CCM) ambalo
lililoulizwa kwa niaba yake na mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama
alitaka kujua kama Serikali inaweza kueleza ni kwa nini kata ya
mikocheni eneo TPDC karibu na viwanja vya mitambo ya TTCL halipati maji
mpaka sasa. “Mradi wa
miundombinu ya maji uliofanywa na Wachina katika maeneo mengi ya jijini
Dar es Salaam hususan wilaya ya Kinondoni haifanya kazi hadi hivi sasa,”
alisema Mbunge huyo.
Akijibu
swali hilo, Dk. Mahenge alisema kata ya Mikocheni iko katika eneo
linalopata maji kutoka mtambo wa Ruvu chini hivyo kutokana na mahitaji
ya maji kuwa makubwa ukilinganisha na uwezo wa uzalishaji wa mtambo wa
huduma ya maji katika maeneo mengi jijini hutolewa kwa mgao.
“Hii ni pamoja na eneo karibu na viwanja vyenye mitambo ya TTCL kata ya Mikocheni,” alisema Naibu Waziri huyo. Aliongeza
kuwa huduma ya maji katika kata hiyo na maeneo yote yanayopata maji
kutoka mtambo wa Ruvu Chini itakuwa ya uhakika zaidi baada ya kukamilika
kwa mradi unaoendelea hivi sasa wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini.
Alifafanua
kuwa mkandarasi anaendelea na upanuzi kuongeza uzalishaji wa asilimia
50, kutoka lita milioni 180 kwa siku za sasa hadi kufikia lita milioni
270 kwa siku. “Kazi hiyo
itakamilika mwezi machi 2013 sambamba na upanuzi huo bomba kubwa
litajengwa kuyatoa maji hayo kutoka eneo la mtambo kuyaleta jijini,”
alisema Dk. Mahenge.
Alisema Serikali imetenga jumla ya sh bilioni 116.4 katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kazi hiyo.
Naibu Waziri
huyo alitanabaisha kuwa mhandisi wa kusimamia kazi ameshateuliwa na
taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi katika hatua za mwisho na
ataajiriwa baadaye mwezi huu na ujenzi utafanyika kwa miezi 15.
Source: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment