To Chat with me click here

Tuesday, July 24, 2012

MCHUNGAJI DK. GERTRUDE RWAKATARE (CCM) ACHOSHWA NA AHADI ZA SERIKALI


MBUNGE wa Viti Maalumu, Mchungaji Dk. Gertrude Rwakatare (CCM) amesema amechoshwa na ahadi za serikali ambazo hazitekelezeki. Mbunge huyo alisema anashangazwa na kitendo cha serikali kutotoa kipaumbele katika sekta ya miundombinu katika Wilaya ya Kilombero.

Dk. Rwakatare alisema tangu akiwa shule ya msingi, barabara za Wilaya ya Kilombero zimekuwa za vumbi licha ya kuwa kila siku serikali imekuwa ikitoa ahadi ambazo hazitekelezeki.

Aidha, aliihoji serikali kueleza kama Wilaya ya Kilombero ni wilaya ya muda au ni ya kudumu na kama ni ya kudumu kwanini isipewe kipaumbele katika ujenzi wa barabara za kiwango cha lami tofauti na ilivyo sasa.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka serikali ieleze ni lini ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kidatu-Taveta utaanza kutekelezwa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, alisema barabara ya Kidatu-Ifakara-Taveta, ujenzi umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Alisema ujenzi wa kilomita 10 za lami kutoka Kiberege Magereza hadi Ziginali ulikamilika mwaka 2006 na ujenzi wa kilomita 6.17 za lami kutoka Kibaoni hadi Ifakara mjini ulikamilika mwaka 2008.

Aidha, alisema ujenzi wa kilomita 24 za lami kati ya Kihansi na Mlimba ulikamilika mwaka 1999 na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya barabara ya Ifakara -Kibaoni hadi Ziginali kilomita 16.8 umekamilika mwaka 2010/11.

Hata hivyo, Mhandisi Lwenge alisema serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa sehemu ya Ifakara hadi Kihansi, barabara yenye urefu wa kilometa 126, umepangwa kuanza mwaka 2013/14

No comments:

Post a Comment