SAKATA
la wabunge kuhongwa kwa nia ya kuyatetea makampuni ya mafuta na menejimenti ya
Shirika la Ugavi wa Umeme Nchini (TANESCO) linazidi kuchukua sura mpya kadiri
siku zinavyosonga mbele.
Siku
moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
kuvurumisha makombora dhidi ya wabunge hao pasipo kuwataja kwa majina, Mbunge
wa Kuteuliwa, James Mbatia, ameibuka na jipya kuhusu sekeseke hilo.
Mbatia
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi amesema wakati
wowote kuanzia sasa atawataja kwa majina wabunge wote waliopokea rushwa kwa
lengo la kuwalinda viongozi wakuu wa TANESCO wanaokabiliwa na tuhuma za
kulihujumu shirika hilo.
Mbali
ya hilo, Mbatia amemshutumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa kuwalinda wabunge
hao aliodai wamehongwa na mafisadi hao wa TANESCO.
Kauli
hiyo aliitoa jana mkoani hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu uamuzi wa Spika Makinda kuridhia kuivunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini na kuiagiza Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge
kuwachunguza watuhumiwa.
Mbatia
alisema Spika anao ushahidi wa kutosha wa majina ya wabunge waliohongwa kwani
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliliambia Bunge kuwa
wana ushahidi wote.
Alibainisha
kuwa ushahidi huo ndiyo uliomfanya Spika Makinda akaridhia kuivunja kamati
husika na kuipa kazi Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge kuwachunguza
watuhumiwa.
Kiongozi
huyo pia alisema hawana imani na kamati iliyopewa jukumu la kuwachunguza
wabunge watuhumiwa wa rushwa kwa sababu inaundwa na baadhi ya watuhumiwa.
“Tunamtaka
Spika ajitakase kwanza kwa kuwaengua wajumbe ambao ni watuhumiwa, kinyume na
hapo hatuna imani na kamati hiyo,” alisema.
Alisema
Bunge ni chombo kitukufu na ili utukufu huo uonekane ni lazima maamuzi yanayofanywa
huko yaheshimiwe, hivyo akapendekeza kuwa mbali na Bunge kutumia kanuni zake
kuwahukumu wabunge watuhumiwa au linaweza kuiga maamuzi ya baadhi ya mabunge ya
Jumuiya ya Madola.
Alitolea
mfano mabunge ya Uingereza na India, ambapo Bunge la Uingereza limewahi
kuwatimua na kuwavua ubunge wabunge 57 na India imefanya hivyo kwa wabunge 11
kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Hivyo
basi tunatoa wito kuwa mbunge yeyote wa chama chochote anayeamini kwa dhamira
yake kwamba ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na anafanya biashara na
TANESCO kwa njia ya maslahi binafsi halafu anatumia rushwa kuwashawishi wabunge
wengine au amepokea rushwa kutetea uovu ni bora akajiondoa mwenyewe kwenye
ubunge kabla ya kuabishwa na Bunge,” alisema.
Mbatia
aliongeza kuwa wanamtaka Spika awe amewataja kwa majina wabunge waliopokea
rushwa si zaidi ya wiki moja ili Bunge liwachukulie hatua, huku akiwaomba
wabunge wenzake bila kujali itikadi za vyama vyao wafanye azimio la Bunge ili
wahusika mbali na kuvuliwa ubunge wafungwe jela miaka mitano.
“Kwa
mujibu wa sheria namba 3 kifungu cha 32 ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ya
mwaka 1988, mbunge anakatazwa kuzungumza, kuhoji, kupiga kura au kutetea jambo
lolote bungeni ambalo litakuwa na ushawishi wa maslahi yake binafsi kutoka nje
na kwamba adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka mitano jela,” alisema
Mbatia.
Mwenyekiti
huyo ambaye alifuatana na mbunge mwingine wa chama hicho wa Kasulu Mjini, Moses
Machali, alimtaka Spika kuzitaja kamati nyingine ambazo wajumbe wake wanatuhumiwa
kwa rushwa.
Mbali
na Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa, kamati nyingine zinazodaiwa baadhi
ya wabunge wake kujihusisha na vitendo vya rushwa ni ile ya Hesabu za Mashirika
ya Umma (POAC) chini ya Zitto Kabwe na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
inayoongozwa na Augustine Mrema.
Nyingine
ni ya Miundombinu chini ya Peter Serukamba, Viwanda na Biashara ya Mahmoud
Mgimwa na Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya James Lembeli.
“Tatizo
la nchi yetu ni kuchelewa kufanya maamuzi wakati muafaka. Tukilitakasa Bunge
kwa kuwashughulikia wabunge waliokula rushwa ni wazi hata serikali itaanza
kuwachukulia hatua wale ambao tumekuwa tukiwalalamikia kujihusisha na rushwa,”
Mbatia
aliwatahadharisha wabunge wa chama chake kuwa kama kuna yeyote aliyechukua rushwa
katika sakata hilo, ajiengue mapema.
Mbatia
pia alitumia mwanya huo kuwatia matumaini wabunge waadilifu wenye misimamo
mikali ya kuikosoa serikali kuwa wasiogopeshwe na sakata hilo ambalo alidai
serikali italitumia kuwanyamazisha wabunge kwa vile walikuwa wakiikosoa.
Ingawa
Mbatia hakuwataja kwa majina wabunge hao, habari ambazo Tanzania Daima inazo
zinaeleza kuwa wabunge zaidi ya sita wanatajwa kuwa katika kundi la wale
wanaotuhumiwa kuwatetea mafisadi wa TANESCO.
Inadaiwa
wabunge hao walipewa fedha na kampuni za mafuta ili washinikize kung’olewa kwa
Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eliakim Maswi
wanaodaiwa kuipa zabuni ya kusambaza mafuta kwa TANESCO kampuni ya Puma Energy.
Habari
zinaeleza kuwa, wabunge hao wako katika Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Kamati ya Miundombinu, Kamati ya
Viwanda na Biashara na Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Vyanzo vya habari hili vimedokezwa kwamba wabunge takriban
wote isipokuwa mmoja tu, walioko katika orodha hiyo wanatokana na Chama Cha
Mapinduzi (CCM).