To Chat with me click here

Thursday, November 15, 2012

VIONGOZI CHADEMA WANUSURIKA KWENDA JELA

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliokabiliwa na kesi ya kudharau amri ya mahakama, wamenusurika kwenda jela miezi minne baada ya kufanikiwa kulipa faini.

Katika kesi hiyo namba 58 ya mwaka 2012, viongozi watano walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kudharau amri halali ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, dhidi ya shauri namba 69.

Katika kesi hiyo, Wakili wa upande wa mlalamikaji, Boniphace Matata, alisema viongozi hao walistahili kuhukumiwa kifungo jela kutokana na kudharau amri ya mahakama ya kuwataka kufika ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Diwani wa Kata ya Kitangiri, Henry Matata, aliyekuwa akipinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kumvua uanachama.

Katika kesi hiyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Angelo Rumisha, baada ya kusikiliza hoja za wakili wa mlalamikaji pamoja na utetezi wa wakili wa walalamikiwa, aliwatia hatiani viongozi hao kwa kuwahukumu kifungo cha miezi minne jela au kulipa faini ya Sh 155,000 kila mmoja.

Hata hivyo, viongozi hao walifanikiwa kulipa faini na kunusurika kwenda jela kuanza maisha mapya ya miezi minne.

Walionusurika kwenda jela ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo Taifa, Benson Kigaila, Diwani wa Kata ya Kirumba, Dan Kahungu, Katibu Uenezi wa Wilaya, Carlos Majora na Katibu wa Wilaya ya Ilemela, John Anajus.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea mahakamani hapo Novemba 19, mwaka huu, na walalamikiwa wote wanapaswa kuhudhuria mahakamani hapo bila kukosa.

Hivi karibuni, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa kwa viongozi wa CHADEMA, baada ya kudaiwa kudharau amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza.

No comments:

Post a Comment