WAKATI
kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ya
kuwataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuacha kulitegemea Jeshi la
Polisi katika kukabiliana na wapinzani wao ikiibua upya machungu ya mauaji ya
raia, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema uvumilivu wake
umefika kikomo.
Badala
yake CHADEMA kimesema kitachukua hatua zote za kulinda haki zake za msingi,
ikiwemo uhuru wa kuendesha mambo ya siasa kwa mujibu wa katiba na sheria na
zaidi kupambana na hujuma zote, zikiwemo za wizi wa kura wakati wa uchaguzi.
Msimamo
huo ulitolewa juzi usiku na Mbunge wa Ilemela, Ezekiel Wenje ambaye alisema
CHADEMA, kimevumilia vya kutosha kile alichokiita unyanyasaji, uonevu na wizi
wa kura ambao alidai umekuwa ukifanywa waziwazi na viongozi wa CCM katika
chaguzi kadhaa hapa nchini.
Akizungumza
katika kipindi cha ‘Malumbano ya Hoja’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha
ITV, Wenje alisema viongozi wa CHADEMA wamejitahidi kwa muda mrefu kuwa
waungwana na kulazimishwa kukubali udhalimu huo kwa nia ya kuokoa nchi isiingie
katika machafuko.
Huku
akiungwa mkono na washiriki wengine wa mdahalo huo, Wenje alisema serikali
imekuwa ikitumia vibaya madaraka yake na rasilimali za nchi kukandamiza vyama
vya upinzani, ama wale wote wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kuikosoa.
“Kuanzia
sasa hatutakubali tena uonevu huu. Wapinzani wameibia kura zao waziwazi, na
tunapojaribu kusema ukweli, tunashambuliwa na kupigwa.
“Hakuna
amani katika nchi inayoendeshwa kwa uonevu, maana demokrasia ya kweli ni
kutenda haki na usawa kwa wote,” alisema Wenje.
“Wakati
katika uchaguzi wa Marekani matokeo yote yalitangazwa kikamilifu, utashangaa
kuona pale Ilemela, msimamizi wa uchaguzi alishikwa kigugumizi kutangaza
matokeo kwa siku tatu,” alisema.
JK kikaangoni
Mbali
na msimamo huo uliotolewa na Wenje, CHADEMA pia kimemshukia Rais Kikwete na
kumtaka awawajibishe mara moja maofisa wa serikali waliohusika kutekeleza amri
za viongozi wa CCM za kuwapiga na kusababisha vifo vya wananchi.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
CHADEMA, Wilfred Lwakatare amesema kauli ya Kikwete mjini Dodoma wakati
akifunga mkutano mkuu wa CCM, imebainisha na kuweka wazi kuwa vyombo vya dola
viliwakamata, kuwatesa na kuwaua wananchi hususan viongozi na wanachama wa
upinzani kwa amri ya chama tawala.
Lwakatare
alisema hoja ya Rais Kikwete ni jibu tosha kwa Watanzania kwamba CCM imekuwa
ikilitumia Jeshi la Polisi kutimiza matakwa yao kisiasa.
“Kwa
kuangalia muktadha wa mtiririko wa matukio ya kudhibiti upinzani kwa kuvuruga
kazi za kisiasa za vyama vya upinzani yanayofanywa na vyombo vya dola, kwa kuua
Watanzania wasiokuwa na hatia, kauli hiyo ya Kikwete imetufikisha kwenye kilele
cha ushahidi kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa kukabiliana na hoja na
shughuli halali za kisiasa zinazofanywa na CHADEMA.
“Kikwete
amethibitisha pasi na shaka kuwa CCM waliwatumia polisi katika kumuua kijana
Ally Singano Zona wakati wanachama na wapenzi wa CHADEMA walipofanya mapokezi
ya viongozi wao wa kitaifa Agosti 27, 2012, mjini Morogoro,” ilisema sehemu ya
taarifa ya Lwakatare.
CHADEMA
pia kimedai kuwa kauli hiyo ya Kikwete imefumbua fumbo la kwa nini polisi
mkoani Iringa, chini ya usimamizi wa RPC Michael Kamuhanda waliamua kutumia
nguvu kubwa kuingilia shughuli halali ya CHADEMA kufanya mikutano ya ndani,
ikiwemo ufunguzi wa matawi katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa, na
hatimaye wakamuua mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012.
“Kwa
kuangalia mtiririko wa matukio ya huko nyuma kama ambavyo tumewahi kuyatolea
kauli na taarifa huko nyuma na kuangalia ripoti za uchunguzi wa tukio la
Nyololo, hasa uchunguzi uliofanywa na Baraza la Habari Tanzania na Tume ya
Utawala Bora na Haki za Binadamu (TUBHB), sasa ni wazi kila mmoja anaweza kuona
kulikuwa na kila aina ya dalili ya maelekezo ya kisiasa kutumia polisi
kuidhibiti CHADEMA.
“Kikwete
pia amewasaidia Watanzania kuanza kutafuta majawabu kwa nini watuhumiwa wa kesi
ya mauaji ya aliyekuwa Kiongozi wa CHADEMA, Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo,
ambao katika tuhuma zao walishirikiana na viongozi wa CCM kuua, waliweza
kutoroka mikononi mwa polisi na hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa,”
alisema Lwakatare.
Pamoja
na kukumbusha vurugu za Ndago huko Iringa, CHADEMA kimezidi kudai kuwa kauli ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete imefumbua fumbo juu ya mazingira ya utata
yanayozunguka kifo cha kada wa CHADEMA, Mbwana Masoud, kilichotokea Igunga
baada ya uchaguzi mdogo, aliyekutwa ameuawa kinyama baada ya kutekwa na kuteswa
na vijana wa CCM waliopewa mafunzo ya kufanya kazi hizo katika makambi ya
Ulemo, Iramba, Singida.
“Upo
uthibitisho mkubwa, kuwa CCM kimeingiza silaha za moto bila kibali na kuwapatia
vijana wake katika mafunzo kwenye makambi maeneo mbalimbali nchini.
“Tangu
utolewe ushahidi huo, kwa kutaja aina ya bunduki, namba yake, uwezo wa kubeba
risasi na ilikotengenezwa, mbali ya polisi kushindwa kufanya uchunguzi ili
kuwaambia Watanzania kwa nini CCM wanaingiza silaha nchini, Mwenyekiti wa CCM,
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, ameshindwa kutoa ufafanuzi wowote,
hali ambayo inahatarisha ulinzi na usalama wa nchi,” alisema.
Lwakatare
alizidi kuishambulia kauli ya Rais Kikwete akidai imefunua ukurasa mpya wa
kilele cha ushahidi wa namna ambavyo kuna ushirika kati ya CCM, serikali yake
na vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, kushughulikia vyama vya upinzani,
hususan CHADEMA kwa kuteka, kutesa na kuua raia wasiokuwa na hatia, lengo kubwa
ikiwa ni kutimiza matakwa ya propaganda za CCM kuwa CHADEMA ni chama cha vurugu.
Kutokana
na hali hiyo, CHADEMA kimemtaka Rais Kikwete kutekeleza barua ya Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyemwandikia kutaka matukio yote ambayo vyombo vya
dola, vimetumika kuteka, kutesa na kuua kwa malengo ya kisiasa ya kupambana na
wakosoaji wa CCM na serikali yake, vifanyiwe uchunguzi huru, kwa kuunda Tume ya
Kimahakama/Kijaji ili ukweli ujulikane na haki ionekane ikitendeka badala ya
kutoa lugha ya kisiasa kwa nia ya kujikosha mbele ya umma.
Aidha,
wakati uchunguzi huo ukifanyika, watuhumiwa wote, wakiwemo viongozi wa CCM,
serikali na watendaji wa Jeshi la Polisi waliokubali kutumiwa na CCM, hata
kuvunja haki za binadamu, katiba na sheria, wanawajibika kwa wao kujiuzulu au
kufukuzwa kazi na Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment