Mhe. Zitto Kabwe |
Jumanne
tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari zinazohusu
matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu sakata ya
mabilioni ya Uswisi. Waziri amesema kwamba Serikali ya Uswisi inataka majina ya
Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze kusaidia uchunguzi. Habari kama
Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo iliandikwa na Gazeti la The Guardian
on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona
ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa
juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio
kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja,
Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la
Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wakati akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta
maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio sababu mpya
ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa
itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya
Serikali. Bunge limeagiza Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za
kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza
kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini?
Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya
Biashara jijini Dar es Salaam na namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje
(international transfers), leo Serikali inakuja na kauli za kukakata tamaa?
Kunani?
Pili,
Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi
za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao
na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano
kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge
linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya
Swiss. Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu
kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule Kongo – Kinshasa, Serikali ya Swiss
iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa
hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka
Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani
Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa kuwa na
zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya nje ya nchi
hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi inapewa.
Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi hivi.
Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata
wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi. Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya
Tanzania inashabikia majibu yao. Bila Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya
Waswiss kama kasuku. Tunasahau historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe
Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Sasa
Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza
utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka Serikali
ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili sio
suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa
kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni
suala la Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya
kutekeleza Azimio lao. Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia
maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza utoroshaji
mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea
Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya Tanzania. Hatutakaa kimya
mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge
itakuwa ni salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana
pa kujificha na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii.
Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la
Mazezeta. Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata kusema.
No comments:
Post a Comment