YASHINDWA KUTETEA MITAA YA
HALMASHAURI MPYA, CHADEMA WAONGOZA HALAMASHAURI
CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kudhihirisha umwamba wake katika Mkoa wa
Arusha, ambapo kwa mara nyingine tena kimeipiga kikumbo CCM na kutwaa
halmashauri mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Usa River.
Ushindi huo unakuja zikiwa
ni siku chache tangu chama hicho kiitwae Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha
ambayo ilikuwa ikiongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi, aliyefariki dunia.
Uchaguzi huo ulifanyika
kutokana na Halmasuri ya Arumeru Mashariki kugawanywa, na hivyo kuunda
halmashauri mpya ya mamlaka ya mji mdogo wa Usa River.
Kabla ya kugawanywa, mitaa
yote ilikuwa ikiongozwa na CCM na hivyo, ikalazimika viongozi hao wajiuzulu ili
uchaguzi ufanyike upya wa kuwapata wenyeviti wapya wa mitaa tisa.
Hadi tunakwenda mitamboni
jana jioni, tayari CHADEMA kilikuwa kimejizolea ushindi mkubwa katika mitaa
sita, huku CCM kiking’ara kwenye mitaa mitatu.
Mitaa hiyo na kura zake
kwenye mabano ilikuwa Manyata Kati (CHADEMA 118, CCM 78), Nganana (CHADEMA 127,
CCM 117), Kisambare (CHADEMA 613, CCM 190), Ngarasero (CHADEMA 785, CCM 355) na
Magadini ambako CHADEMA walipata kura 303 dhidi ya 106 za CCM.
Hata hivyo, CCM ilifanikiwa
kurejesha mitaa mitatu ya Magadirisho, Mlima Sioni na Usa Madukani.
Kwa ushindi huo, CHADEMA
sasa wamefanikiwa kuongoza halmashauri ya pili katika Mkoa wa Arusha, kwani kwa
zaidi ya miaka kumi wamekuwa wakiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Katibu wa CHADEMA Mkoa wa
Arusha, Amani Golugwa, alisema kuwa wanataka kuifanya halmashauri mpya ya Usa
River iwe ya mfano katika Jiji la Arusha.
“Tumejipanga kuiboresha Usa
River kuanzia usafi, mapato na miundombinu yake, kwani CCM wamekuwa wakisuasua,
lakini sasa wameachia,” alisema.
CHADEMA kimekuwa kikitoa
ushindani mkubwa kwa CCM katika Mkoa wa Arusha kwani hata kwenye uchaguzi mdogo
wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, chama hicho kilitwaa kiti hicho
kilichokuwa kikikaliwa na wapinzani wao baada ya aliyekuwa mbunge kufariki.
No comments:
Post a Comment