To Chat with me click here
KUUAWA NA KUPORWA KWA MAPADRE JE UJAMBAZI WA KAWAIDA AU NI MAHUSIANO NA VITA YA KIDINI DHIDI YA WAKRISTO NA WAISLAMU?
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge) William Lukuvi, amesema kuvamiwa, kupigwa risasi na kuporwa
kwa mapadre wa Kanisa Katoliki Parokia za Isimani na Kihesa mkoani Iringa, ni
ujambazi wa kawaida na hauhusiani na masuala ya udini.
Hadi kufikia jana mchana, tayari watu wanne akiwamo mwanamke mmoja, walikuwa
wametiwa mbaroni, wakihusishwa na tukio hilo la uhalifu wa kutumia silaha.
Novemba 16, mwaka huu, zaidi ya watu sita waliokuwa na bunduki pamoja na silaha
za jadi, walivamia Parokia ya Isimani na kuwapiga risasi, Paroko wa Kanisa
hilo, Father Herman Myalla (36) na Angelo Burgio (66), raia wa Italia na
baadaye kupora zaidi ya Shilingi milioni nne na Euro 100.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuwajulia hali majeruhi
hao waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Lukuvi ambaye pia
ni Mbunge wa Isimani, alisema waliohusika katika uhalifu huo ni majambazi na si
vinginevyo.
”Kilichotokea ni ujambazi wa kawaida na hauhusiani na kitu kingine lakini pia
tunaamini wote waliofanya uhalifu huo watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Nimewajulia hali na nimewahakikishia kwamba kilichotokea ni ujambazi tu kwa
hiyo serikali iko pamoja nao,” alisema.
Katika tukio la kwanza lililotokea Novemba 15, mwaka huu majira ya usiku katika
Manispaa ya Iringa, watu wasiofahamika walivamia na kupora vitu mbalimbali
katika Parokia ya Kihesa na kumjeruhi vibaya mlinzi wa kanisa hilo, Bartholomeo
Nzigilwa.
Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk.
Gwanchelle Faustine, alisema jana kuwa hali za majeruhi watatu waliolazwa hapo
zinaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment