Waziri
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema shehena na makontena
mawili ya meno ya tembo yaliyokamatwa Hong Kong, yatachunguzwa kwa kutumia
vinasaba (DNA) ili kubaini kama asili yake ni Tanzania.
Aidha,
amesema maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wale waliokuwa zamu siku shehena hiyo ikipitishwa bandarini Dar es Salaam kwenda
Hong Kong, wanachunguzwa ili kubaini ukweli.
Alisema
hayo wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge waliokuwa wakijadili
maazimio mawili ya Bunge kuhusu marekebisho ya mpaka na upanuzi wa Hifadhi ya
Taifa ya Gombe na lile la kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane.
“Hatuna
uhakika bado kama meno yaliyokamatwa huko Hong Kong yana asili ya Tanzania au
yalikuwa yakipitishwa nchini mwetu…tunafanya mazungumzo na balozi wetu kule
China kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema
taarifa ambazo zimekwishapatikana zinaonyesha kwamba kontena moja linatokea
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kontena lingine bado halijaeleweka
wazi kwamba linatokea Tanzania au la, na ndio maana uchunguzi utahusisha vipimo
vya DNA ili kujua asili ya meno hayo.
Oktoba
16, mwaka huu, maofisa usalama wa Hong Kong waliyakamata makontena mawili
yaliyokuwa yamesheheni meno ya tembo yenye thamani ya dola za Marekani milioni
3.4.
Hata
hivyo, kontena moja kati ya hayo lenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.7
linadaiwa kuwa linatokea Tanzania.
Kama
hiyo haikutosha, shehena ya meno ya tembo ilikamatwa bandarini Dar es Salaam
Jumapili iliyopita na hali ambayo inaonyesha kasi ya kuuwa kwa tembo ni kubwa.
Mapema
katika mchango wake binafsi, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa, alisema kuongeza mipaka ya hifadhi ni suala zuri lakini serikali
inawajibu wa kulinda hifadhi hizo.
Alizungumzia
tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa meno ya tembo huko Hong Kong na
bandarini Dar es Salaam yanaashiria kwamba tembo waliopo kwenye hifadhi
wanauawa.
No comments:
Post a Comment