To Chat with me click here

Friday, November 2, 2012

MSIGWA AING’ANG’ANIA MALIASILI NA UTALII



Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amesema wizi wa pembe za ndovu pamoja na kuuliwa kwa wanyama, ni matokeo ya idara hiyo kuendelea kuwalinda majangili badala ya kuwachukulia hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mchungaji Msigwa, alisema Rais Jakaya Kikwete, anatakiwa kuingilia kati na kuvunja mtandao wa ujangili ili kunusuru wanyamapori na maliasili nyingine za Taifa.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema mpaka sasa ni miezi mitatu tangu alipowasilisha taarifa za ujangili bungeni na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, achukue hatua dhidi ya majangili hao na matokeo yake amewajibisha watu watatu wa Idara ya Wanyamapori huku watuhumiwa wakubwa wakiachwa.

Alisema jambo hilo ni hatari na kusababisha idadi ya wanyama kupungua kila wakati. Alisema wiki iliyopita, pembe za ndovu zenye uzito wa tani nne kutoka Tanzania na Kenya zenye thamani ya Sh. bilioni 2.5, ziliripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya Jiji la Hong Kong.

Mchungaji Msigwa alisema tangu kutokea kwa tukio hilo mpaka sasa, waziri husika amekaa kimya pamoja na serikali yake juu ya suala hilo kana kwamba kilichotokea ni jambo la kawaida.

“Kama ilivyokuwa katika sakata la ununuzi wa rada, ni vema Watanzania wakazingatia kuwa hatua ya pembe za ndovu za Tanzania kukamatwa na vyombo vya usalama vya Hong Kong, ni kielelezo cha kuwa waziri na serikali wameshindwa hata kusimamia na kulinda maliasili zetu na kuviachia vyombo vya usalama vya nchi nyingine vikitufanyia kazi hiyo. Hii ni aibu kubwa kwa serikali na CCM,” alisema.

Alisema pembe za ndovu zilizokamatwa ni matokeo ya kuendelea kuwalinda watuhumiwa wakuu wa ujangili.
Alikumbusha kwamba katika Mkutano wa Bunge uliopita, Kambi ya Upinzani bungeni pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliwataja vinara wa ujangili.

Alisema inashangaza kuona kwamba, hadi sasa watu hao hawajakamatwa hali inayochochea vitendo hivyo, wizi na ufujaji wa rasilimali nyingine za taifa.
“Kati ya wanaohutuhumiwa kuwa majangili, baadhi yao wameteuliwa katika Nec na pia ni washauri wa mwenyekiti wao. Hii ni hatari haina haja niwatajie majina wanajulikana na nyie fanyeni uchunguzi wenu mtawajua,” alisema.

Alisema hatua za msingi zinatakiwa kuchukuliwa ili kutokomeza suala hilo katika kulinda utalii wa nchi pamoja na kuongeza uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo.

Katika Mkutano wa Bunge uliopita, Mchungaji Msigwa aliwataja kwa majina vinara wa ujangili nchini akiwemo Bryson Baloshingwa aliyedai kuwa ni kiongozi wa mtandao wa ujangili kwa kufadhili uwindaji wa faru na biashara haramu ya meno ya tembo; uharamia unaofanyika katika hifadhi za Serengeti, Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara na Ngorongoro.

Alidai Baloshingwa anafadhili pia majangili wanaoua wanyama katika mapori ya akiba ya Ugalla, Rungwe, Moyowosi na Maswa.

Alisema inashangaza kwamba wafadhili na majangili wanafahamika kwa majina, lakini hawachukuliwi hatua na pindi wanapokamatwa hufunguliwa kesi rahisi zenye dhamana hivyo huachiwa kwa dhamana.

“Usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa hizi kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika ujangili,” alisema.

Tuhuma za Msigwa zinakuja wakati ambao Waziri Kagasheki amekuwa akisafisha Idara ya Wanyamapori ikiwemo kuwasimamisha vigogo wa idara hiyo.

Katika tukio la karibuni, Balozi Kagasheki amewatimua kazi vigogo watatu wa wizara hiyo akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya kubainika kuhusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.

Vigogo hao wamefukuzwa kazi baada ya tume iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo kufanya uchunguzi na kumaliza kazi yake.

Katika kashfa hiyo, vigogo hao wanadaiwa kuhusika na usafirishaji wa wanyamapori hai 116 na ndege 16 Novemba 24 mwaka 2010,  kwenda nje ya nchi kupitia Kia.

Waliosimamishwa ni Obeid Mbangwa, Mkurugenzi wa Wanyamapori ambaye wakati wa kadhia hiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori. Wengine ni Simon Charles Gwera, Ofisa Uwindaji wa Kitalii Cites na Utalii wa Picha – Arusha na Frank Mremi, Ofisa Uwindaji wa Kitalii Cites na Utalii wa Picha-Arusha.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, Adam Ng’imba, amewaumbua watendaji wa Idara ya Misitu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwamba ndiyo vinara wanaochochea uharibifu wa misitu wilayani humo.

Ng’imba aliyaeleza hayo mwishoni mwa wiki mbele ya vigogo hao wa wizara wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyotembelea misitu ya Ruvu Kusini na Ruvu Kaskazini.

Alisema biashara ya mkaa na hususani unaotokana na uvunaji wa misitu ya Pwani inafanywa kwa mtandao wa vigogo wa Idara ya Misitu ambao wameweka vijana kwenye kambi kwenye misitu hiyo.

“Na leo halitapita lori la mkaa kabisa kwa sababu vigogo walioandaa ziara hii wanajua kamati ya Bunge inakuja, wanazuia magari yao…hii ni biashara inayofanyika kwa mtandao kutoka wizarani, ukikamata lori simu zinapigwa na wanatoka ofisini kuja kuliruhusu liondoke,” alisema.

Alisema wakati fulani, Meneja wa Msitu wa Ruvu Kusini, alikamata shehena ya mkaa lakini cha kushangaza kigogo mmoja wa idara ya misitu alikwenda Kisarawe na kuruhusu lori hilo liendelee na shughuli zake.

“Ninyi viongozi wa wizara vunjeni mitandao ya ujangili ndipo tutaweza kupambana hii vita, hali ni mbaya, napenda nikuhakikishie Mheshimiwa Mwenyekiti (wa kamati ya Bunge, James Lembeli), hili ni eneo la msitu lakini sio msitu, kuna vichaka vichache tu na walioimaliza si wengine ni hawa vigogo wa idara ya misitu pale wizarani,” alisema.

Alisema kuteketea kwa misitu hiyo kunahatarisha maisha ya wananchi wa Pwani lakini zaidi watakaoumia ni wakazi wa Dar es Salaam hivyo jitihada za makusudi zinahitajika kuinusuru.

Awali, wananchi wanaofanya ulinzi shirikishi kwenye misitu hiyo, wanakabiliwa na tatizo la kipato na kwamba serikali haiwalipi chochote kutokana na kazi wanayofanya hivyo wamekuwa wakishindwa kutekeleza jukumu hilo ipasavyo.

Walisema majangili ni watu wenye silaha na fedha hivyo inakuwa rahisi kwa walinzi kushawishika kupokea rushwa na kuacha kulinda.
Waliiomba serikali kuingia nao mkataba wa kulipa asilimia kadhaa kwa ajili ya vijiji vinavyozunguka misitu ili kutoa motisha kwa wananchi wanaolinda misitu.

Baada ya maelezo hayo, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TSF), Kanda ya Mashariki, Bakari Mohammed, alisema kumekuwa na jitihada kubwa za udhibiti wa uharibifu ikiwemo kukamata mkaa na majangili wanaoingia msituni kuvuna miti.

Hata hivyo, Lembeli alimtaka Meneja huyo kufanyiakazi tuhuma hizo badala ya kujitetea kwa takwimu za malori, mbao ni tani za mkaa zilizokamatwa.
Alisema misitu hiyo imeteketea kabisa hivyo serikali inatakiwa kuchukua hatua za ziada kuirejesha misitu hiyo.

Alisema kamati yake imeshuhudia uharibifu mkubwa na wa kutisha wa misitu hiyo na kusema ipo katika hali mbaya. Alisema kamati yake imebaini kwamba uharibifu unachochewa na matajiri wanaoishi Dar es Salaam ambao wanamahitaji makubwa ya nishati ya mkaa na kwamba tatizo lingine ni kukosekana kwa nishati mbadala ya uhakika.

Lembeli alisema uhifadhi wa misitu hiyo pia haiendani na idadi ya watumishi kwa kuwa inategemea ulinzi shirikishi wa wananchi wa vijiji vinavyoizunguka ambao nao hawana kipato cha uhakika.

Lembeli ambaye pia ni mbunge wa Kahama (CCM), aliitahadharisha serikali kuhusu umuhimu wa kutunza misitu hiyo na kutoa asilimia kadhaa ya kile kinachopatikana kutokana na ulinzi unaofanywa na wanakijiji.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya misitu hiyo, Meneja Msaidizi wa TFS, Kanda ya Mashariki, Bernadetha Kadala, alisema hali ya misitu hiyo ni mbaya kwa kuwa imevamiwa na kuvunwa na wafanyabiashara haramu wa mkaa, kuni, mbao, kurunge na nguzo.

Alisema misitu hiyo pia imevamiwa na watu kwa ajili ya makazi na kilimo, na malisho ya mifugo. “Maeneo mengi ndani ya misitu ya Ruvu yana uwazi kutokana na uharibifu huu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na doria za mara kwa mara ambazo zimewezesha kukamatwa kwa mbao, mkaa, kuni, nguzo, magogo, magari, pikipiki na baiskeli za wahalifu.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2012/13, doria zilizofanyika zimekamata malori matano, mkaa magunia 810, mbao 445, nguzo 150 na magogo 190.

No comments:

Post a Comment