Ukisoma
mabango haya niliyokuwekea kwenye ukurasa huu leo, hutapata shida kutambua kuwa
matatizo mengi ya Watanzania, si tu kwamba yanasababishwa na wanasiasa.
Ndiyo
maana nimejiepusha kujadili Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uteuzi
wa viongozi wapya wa Sekretarieti ya chama hicho. Kwa ufupi ni kwamba matatizo
ya Tanzania na Watanzania ni zaidi ya siasa na wanasiasa.
Ukisoma
ujumbe ulio kwenye mabango haya unauona upumbavu unavyotamalaki katika jamii
yetu. Bahati nzuri kwa wanaosambaza upumbavu huo ni kwamba wapo wanaouamini, na
kwa sabahu hiyo wamewafanya matapeli hawa waendelee kuwapo na wengine wazidi
kuibuka kila uchao.
Kwanza,
nisema kwamba tatizo la imani za kishirikina na ujinga wa kuamini ndumba
vimeenea sehemu nyingi duniani. Masuala hayo yapo pia Ulaya, Marekani na Asia.
Tofauti iliyopo ni viwango na aina za uongo; pamoja na idadi ya watu walio
wafuasi wa mambo hayo.
Hapa
kwetu hali ni mbaya. Mauaji ya albino ni aina ya ujinga huo. Dunia ya leo bado
kuna watu wanaamini kuwa kiungo cha albino kinaweza kuwatajirisha.
Pamoja
na ukweli kwamba Katiba yetu imewapa wananchi uhuru wa kuabudu (kuamini?), kuna
mambo tunayopaswa kuyahoji. Upuuzi huu unafanywa mbele ya Serikali ilhali
ikitambua kuwa wanaoendesha mambo haya ni waongo, matapeli, majizi na watu
waliodhamiria kuviza akili na maendeleo ya Watanzania.
Wapuuzi
hawa walianza kujitangaza kwa majina na mahali wanakoishi. Maendeleo ya teknolojia
yamewawezesha kumiliki simu. Matangazo yao yanapambwa kwenye kila kona hapa
nchini. Haitashangaza kuyaona kwenye ukuta wa Ikulu!
Walianza
kudanganya kuwa wanatibu Ukimwi. Serikali haikuchukua hatua madhubuti kukanusha
upuuzi huo. Wananchi wenyewe hawakuamini kuwa huo ni uongo. Hatua hiyo
haijawakatisha tamaa, maana wateja wapo japo ni wachache.
Sasa
wameibuka na mambo mengine hatari. Wapo wanaojitangaza kwamba wana uwezo wa
dawa wa kumfanya mwanafunzi afaulu mitihani! Wamelenga kuwapata wanafunzi wa
shule za msingi, vyuo na sekondari.
Kwa
maneno mengine ni kwamba mwanafunzi asisome kwa bidii. Atulie tu, siku ya
mtihani atashinda kwa sababu dawa ya kumwezesha kushinda imeshapatikana! Ujinga
huu unapatikana Tanzania, na pengine Afrika pekee!
Wameibuka
wengine wanaeneza ujinga kwamba wana uwezo wa kumfanya mtu apandishwe cheo
kazini! Huu ni upumbavu wa hali ya juu. Kama kweli dawa hizo zipo, basi jeshini
wote wangekuwa majenerali! Kusingekuwapo koplo wala sajini!
Kama
kweli kuna dawa ya vyeo, basi nchi hii kila mtu angekuwa mkurugenzi, au waziri,
au katibu mkuu, au rais! Badala ya watu kufanya kazi kwa weledi na juhudi,
wanaaminishwa kwamba dawa zitawawezesha kupata vyeo vya juu! Ujinga mtupu.
Wapo
wanaojitanabaisha kuwa na dawa za kurejesha mali zilizoibwa. Huu nao ni uongo
tu. Kama hivyo ndivyo, kwanini hawajajitokeza kumsaidia Zitto Kabwe ili
mabilioni yaliyofichwa ughaibuni yarejeshwe? Kwanini Serikali itumie gharama
kubwa kuendesha kesi za ufisadi ilhali kuna “wataalamu” inaoweza kuwatumia
kurejesha fedha hizo?
Wapuuzi
hawa wanajigamba kutibu kisukari, wakati wanatambua kuwa hakuna dawa ya kutibu
maradhi hayo. Kama ipo, wanasubiri nini kuisambaza duniani ambako matajiri
wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo?
Wengine
wanasema wana dawa za mapenzi kiasi kwamba kama mwanamme akimtaka mwanamke,
atampata! Au mwanamke akimtaka mwanamme, atampata! Huu ni uongo mwingine. Kuna
binti gani wa Kitanzania asiyependa kuolewa katika ukoo wa kifalme?
Mbona
hatujasikia kina Prince Charles kutoka ughaibuni wakifika hapa nchini kwa mvuto
wa dawa hizo kuleta posa kwa mabinti zetu? Mbona hatujasikia kijana mvulana wa
Kitanzania kaenda kuoa katika ukoo wa mfalme Hirohito au Akihito huko Japan?
Tunahangaika
na dawa za kuongeza nguvu za kiume, dawa za kufauli mitihani, dawa za mvuto wa
biashara na ujinga mwingi; huku tukiwaacha wazungu, wahindi na waarabu
wakijitwalia malefu ya ekari za ardhi yetu.
Tufanye
nini? Upuuzi huu lazima tuhakikishe unakomeshwa katika jamii yetu. Kazi ya
kuukomesha imerahisishwa na matapeli hao wenyewe kwa kuweka namba za simu
kwenye mabango yao. Serikali za Mitaa hazipaswi kufumbia macho ujinga huu.
Matangazo
haya yanaifanya jamii ya Watanzania ikose weledi wa kupambana na maisha kwa
njia za kisayansi. Yanawafanya wananchi wengi waamini kuwa unaweza kusafishwa
nyota kisha ukaamka ukiwa tajiri! Hizi ni athari za kupenda njia za mkato.
Watanzania tunapenda sana mkato.
Matangazo
haya ni wizi wa fedha kutoka kwa watu wenye uelewa mdogo, na hasa kutokana na
uhaba wa elimu na umasikini. Matangazo haya yanakifanya kizazi chetu kiwe cha
mbumbumbu wanaoamini katika mitishamba, miujiza, ngekewa; na si katika
kujisomea au kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Imani
hizi zinatufanya tusiwe na utashi wa kujenga mabweni, maabara wala nyumba za
walimu au hata kuweka madawati katika shule zetu! Hatufanyi kazi hizo kwa
sababu tumeaminishwa na wapuuzi hawa kwamba hata bila maabara, vitabu, vyumba
bora vya madarasa, nyumba za walimu na walimu waliohitimu vizuri, bado
tutashinda mitihani na mwisho tutayashinda maisha!
Matapeli
hawa wanawaumiza wananchi kiuchumi. Serikali nayo imebariki wananchi wake
waumizwe. Fedha ambazo wananchi wanahangaika kuzipata, wanazipeleka kwa watu
hawa kwa matarajio ya kufanikiwa zaidi. Huu ni wizi. Matapeli hawa wanapaswa
kushitakiwa kwa makosa ya wizi na ulaghai.
Haya
niliyoyasema kwa matapeli hawa wa mitaani, nayasema pia kwa matapeli wa
makanisani. Huko nako tunaaminishwa kuwa kusali pekee kunaweza kubadili maisha
yetu. Tunadanganywa. Kumeanzishwa redio eti za kuendesha maombi kwa sadaka
zinazopelekwa kwa njia ya Tigo-Pesa, M-Pesa, na kadhalika. Wizi tu.
Jamii iungane kutokomeza
imani hizi za kipuuzi. Tufanye hivyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu. Bila
kutokomeza ushirikina, tutabaki kuwa Taifa la ndoto na matarajio ya kipuuzi.
Tukatae.
No comments:
Post a Comment