MZEE wa miaka 75, mkazi wa kijiji cha Mahida
anashikiliwa na polisi wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumbaka
mwanafunzi wa darasa la pili mwenye umri wa miaka nane.
Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kilimanjaro jana, Robert Boaz zilisema mzee huyo anashikiliwa katika
Kituo cha Polisi cha Mkuu wilayani Rombo kwa uchunguzi zaidi.
“Yule mtoto amezoea kwenda kuchota maji kwa
yule babu sasa kwa maelezo ya mtoto ni kwamba yule babu alimuingizia kijiti sio
tendo la kubakwa lakini yote hayo ndio tunayachunguza,”alisema Boaz.
Hata hivyo taarifa nyingine zilizowakariri
ndugu na majirani zilidai siku ya tukio hilo Alhamisi iliyopita, mwanafunzi
huyo wa kike alikwenda kuchota maji akisindikizwa na mdogo wake wa kiume.
“Baada ya hilo tendo watoto walirudi nyumbani
na ndio yule wa kiume akamwambia dada yake hebu mwambie babu (anayeishi naye)
kuwa yule babu amekufanya nini,”alidai mmoja wa majirani.
Jirani huyo ambaye aliomba jina lake
lihifadhiwe, alidai kuwa yule mtoto alieleza kila kitu na ndipo wazazi
walipompeleka zahanati ya Mahida na baadaye Hospitali teule ya Huruma iliyopo
Rombo.
Majirani hao akiwamo Padre mmoja wa Kanisa
Katoliki, walidai baada ya madaktari katika hospitali hiyo ya Huruma kumfanyia
uchunguzi, mtoto huyo alikutwa na Manii sehemu zake za siri.
Kutokana na hasira waliyokuwa nayo majirani
hao, walihakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi
Holili lakini baada ya majirani kuchachamaa alihamishiwa kituo cha Mkuu.
No comments:
Post a Comment