MJADALA mkali
uliibuka bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
(Chadema) kuwalipua baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali akitaka
wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Zitto alitoa kauli
hiyo jana bungeni wakati akiwasilisha hoja yake
binafsi kuhusu kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua
dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Bila ya kuwataja
kwa majina, mbunge huyo aliwataja watu hao kwa nyadhifa kuwa ni watu wote
walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010,
walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na
waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni
mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi, wakuu wa majeshi, wanasheria wa
Serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa
TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010. Kutokana na hilo, Zitto aliitaka
Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa
Bunge wa Aprili mwakani.
“Mbali na hilo
napendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma au mume au mke
wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na
kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema Zitto.
Pia Zitto alitaka
Serikali kuwasiliana na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery
Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda
Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo mengine ziweze kurejeshwa.
Aliwataka
Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata wapi na
Takukuru wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote wanaomiliki fedha hizo
kinyume cha sheria.
Alipendekeza
kwamba Serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 ianzishe kodi maalumu ya
asilimia 0.5 ya thamani ya fedha zilizotoroshwa ili kuweka rekodi za uhakiki
fedha za ndani na zinazotoka nje.
Mbunge huyo
alisema mazungumzo yake na wachunguzi wake binafsi kiwango cha fedha
kinachomilikiwa na Watanzania Uswisi peke yake ni takriban mara 20 ya kiwango
kilichotangazwa na benki ya taifa ya nchi hiyo. Alisema fedha hizo ni sehemu tu
ya fedha ambazo Watanzania wamezificha katika benki mbalimbali za nje.
Alitoa mfano wa
Benki ya UBS peke yake iliyopo katika nchi hiyo ina maofisa 240 ambao
wanashughulikia wateja wa Tanzania na kila ofisa mmoja husimamia mteja mmoja
mwenye kiwango kisichopungua dola za Marekani 10 milioni.
Zitto alisema
Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola za Marekani 196 milioni
zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za benki za nchi hiyo. Alisema kuwa
pamoja na Mkurugenzi wa Takukuru kukaririwa akisema kuwa ataiandikia Serikali
ya Uswisi barua kuomba kurejeshwa kwa fedha hizo, lakini mpaka sasa hakuna
hatua zilizochukuliwa.
No comments:
Post a Comment