To Chat with me click here

Monday, November 26, 2012

TANZANIA KUBADILIKA INAWEZEKANA



Mwaka wa 1961 tulipata uhuru wa bendera toka kwa wakoloni wa Uingereza, Wakati huo tukiitwa Tanganyika chini ya chama cha TANU na Mwenyekiti wake akiwa Mwl. Julus Nyerere. Kwa wale wanaokumbuka taifa lilitangaza vita dhidi ya maadui watatu, umasikini, ujinga, maradhi.

Miaka zaidi ya 45 ya uongozi wa TANU na sasa CCM bado hali ya nchi yetu ni mbaya sana kwa walio wengi. Wale maadui watatu bado wana tamba, yaani umasikini, ujinga, na maradhi. Na kama hiyo haitoshi hivi sasa tuna adui wa nne aitwe rushwa/ufisadi

Wengi wetu tumejiuliza tatizo liko wapi? Mbona hali inazidi kuwa mbaya? Bila shaka kuna waliokata tamaa na kuamini kwamba kamwe hatutaweza kuiondoa Tanzania katika umasikini uliokithiri.

Serikali iliyoko madarakani imeanda mikakati na sera nyingi za kupambana na hao maadui wa nne, lakini mwenye macho haambiwi tazama!

Miaka ya sitini tulitangaziwa Azimio la Arusha kama silaha ya kumkomboa mtanzania, watu wengi wakati huo walilipokea Azimio kwa matumaini makubwa, leo wote tunajua hatima ya Azimio ilikuwa nini wakubwa walipokutana kule Zanzibara; walilitosa Azimio la Arusha baharini!

Wakubwa hawa wakaja na sera mpya ya uwekezaji kama muarubaini wa matatizo ya Tanzania. Toka wakati huo wamezunguka dunia nzima kuwakaribisha wawekezaji waje kumkomboa mtanzania kwani hawa viongozi wetu kama wazazi wetu ndio haswa wanaojua dawa ya matatizo yetu.!

Leo (2012) ukizunguka nchi nzima utasikia kilio cha jinsi wageni walivyo chukua nchi na wenye nchi wakibaki kulia tu. Ukiuliza unajibiwa na hawa wakubwa wetu wanaotupenda sana kwamba hao wageni ni wawekezaji na bila wao tutabaki na umasikini wetu.!

Mtanzania amekata tamaa, aliikimbilia CCM akiamini itamkomboa lakini wapi, na anapojaribu kugeukia vyama vya upinzani anambiwa hakuna mtu mwenye uwezo huko, hao wapinzani ni wababaishaji tu. Sasa aende kwa nani?

Naomba niseme hivi na kuwakumbusha watanzania wenzangu maneno yaliyopo katika Azimio la Arusha, naamini maneno haya bado yana maana kubwa sana katika kumkomboa mtanzania hata leo:

“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha, unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge, ili tusionewe tena, tusinyonnywe tena.”

Hali mbaya ilioko Tanzania leo ni matokeo yakuendelea kukubali kunyonywa, kupuuzwa na kuwa wanyonge katika nchi yetu wenyewe wakati tukiamini kuwa hatuna la kufanya ili kujikomboa.

Watanzania wenzangu, tukumbuke kuwa Tanzania ni nchi yetu wote, tuliyopewa na Mungu kuwa urithi wetu na watoto wetu. Tanzania sio mali ya kikundi cha watu wachache ambao wao ndio wanaotuamulia nini la kufanya. Tanzania ni haki yetu sote toka kwa Mungu. Sisi wenyenchi kwa pamoja ndio wenye haki ya kuamua mwelekeo wa taifa letu. Tanzania sio mali ya CCM, nchi hii ni yetu sote, Tanzania sio mali ya serikali ya CCM, nchi hii ni haki ya kila mtanzania. Ni dhambi kubwa sana kwa kikundi kidogo cha watu kupora haki ya kuzaliwa ya watanzania na kuwaamulia jinsi ya kuendeleza nchi yao.

Ninasema haya kwa sababu, kama sisi wenyenchi hatujui haki zetu na uwezo wetu katika kuamua hatima ya nchi yetu, daima tutakuwa watu wakuonewa na kunyanyaswa na kikundi kidogo cha watu wakishirikiana na wageni.

Hakuna mtu atakae kuja kuikomboa Tanzania kama sio mtanzania mwenyewe! Inasikitisha sana kuona kwamba kundi dogo la watanzania wenzetu wameingiwa na tamaa ya utajiri, na kuwa tayari kuiuza nchi kwa wageni ilimradi wao wapate neema hiyo hata kama sie wenyenchi tutashindia kipande cha mhogo na maji.

Na dhambi kubwa zaidi inayofanywa ni pale wanapotumia uchaguzi ili kumpora mwenyenchi haki yake ya kuzaliwa. Wote tunajua jinsi uchaguzi unavyoendeshwa kwa rushwa na wizi wa kura, halafu yule anae tangazwa mshindi anatamba kuwa amepewa ridhaa na wenyenchi ya kuwa kiongozi wao! Unajiuliza hivi kweli hawa ni watanzania wenzetu? Baada ya kuingia madarakani kwa hila, angalia wanapigania masilahi ya nani?

Mali asili zilizoko Tanzania ni mali ya watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, leo hiyo haki ya serikali kuamua nani aje kuchimba dhahabu na almasi bila kuwashirikisha wenyenchi wamepewa na nani? Wanafanya hivyo kwa faida ya nani?
Hawa ndio wale wanaotaka kuitwa waheshimiwa na watukufu na ukimwita “ndugu” inakuwa shida kubwa. Huo uheshimiwa wameupata wapi? Viongozi wenye roho za kutaka uheshimiwa ndio hao hao wanaojiona wanajua lile lililo bora kwa watanzania bila hata kuwataka ushauri. Hawa ndio viongozi ambao wakati wa Mwl. Nyerere walikubali kuitwa ndugu!

Huko nyuma kulikuwa na sera ya Chama kushika hatamu, na leo na wahimiza watanzania wenzangu tushike hatamu za nchi yetu kabla hatujachelewa kabisa.

Watanzania wenzangu, inawezekana kuichukua tena nchi yetu. Historia inaonyesha kwamba wanyonge wanapoamua kuwa kitu kimoja na kauli moja inawezekana. Inawezekana kabisa kuondoa umasikini, inawezekana kabisa kuondoa ujinga, inawezekana kabisa kuondoa maradhi, na inawezekana kabisa kuondoa rushwa, ndio, inawezekana! Inawezekana kufaidi utajiri wa nchi yetu kwa pamoja.

Hili linawezekanaje?

Ø Kwanza, kutambua na kuamini kwa moyo wako wote kwamba wewe kama mtanzania unaweza kubadilisha hali ya nchi yako.

Ø Pili, kukataa kabisa kununuliwa wakati wa uchaguzi, na kuwaepuka kabisa wale wote wanao taka uongozi kwa kuununua. Mtu ye yote anae kubali kununuliwa ili ampe kura mtu fulani, huyo ni msaliti na mtu wa hatari kwa maendeleo ya taifa letu.

Ø Kudai haki zetu za kimsingi kwa kuhakikisha kwamba katiba ya nchi inatungwa na sisi wenyenchi na sio kundi la wachache wakipita mikoani kuuliza maoni yetu kuhusu katiba.

Ø Kutumia haki yetu kama watanzania ya kusema hadharani bila uoga yale ambayo tunaona sio sawa na kutaka yarekebishwe haraka. Sisi kama wenyenchi hatuiombi serikali hisani ili ituondolee kero, tunaiagiza serikali.

Ø Serikali yo yote itakayo kuwa madarakani, ielewe kwamba sisi watanzania ndio waajiri, nao wao ni watumishi wetu. Kwa maneno mengine, sisi wenyenchi ndio waheshimiwa na wao kuanzia Rais ni watumishi wetu. Kama tusipolizingatia hili tutaendelea kunyanyaswa na kundi la wajanja wachache na hatutakuwa na wakumlaumu.

No comments:

Post a Comment