Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo |
TANZANIA na Japan zimetiliana saini mkataba
wa mradi wa makubaliano wa kuimarisha uwezo wa viwanda na uboreshaji ili kuleta
tija kwenye sekta hiyo.Japan ni moja ya nchi duniani zilizopiga hatua kiviwanda
tofauti na Tanzania ambayo ni changa katika sekta hiyo.
Miongoni mwa makubalinao ambayo Japan
imekubali ni kutoa mbinu za kiufundi kwa Tanzania kuboresha viwanda na
kutoa mbinu za kukuza ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati
wa kutia saini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Joyce Mapunjo alisema sekta ya viwanda ndio sekta inayopewa
kipaumbele katika kukuza maendeleo katika nchi mbalimbali dunia.
“Tunafurahi kutambua kuwa huu ni mradi wa
kwanza wa ushirikiano wa kiufundi wa aina yake unaolenga sekta ya viwanda hapa
nchini, kwani tunajua mpango huu utatufikisha mbali kwa sababu ni mambo
ya kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji,” alisema Mapunjo.
Alisema kupitia makubaliano ya mradi huo
waliupa jina la ‘Kaizen’, utasaidia kuimarisha sekta ya viwanda na
kuboresha bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
“Mradi wa Kaizen unatambulika duniani kote na
Shirika la Jica limekuwa likitekeleza mradi huu wa kiufundi katika nchi
mbalimbali tangu ulipoanzia katika Nchi ya Singapore mwaka 1983 na tuna imani
utaleta mafanikio na tija kwa wazalishaji bidhaa mbalimbali hapa
nchini,”alisema .
Alisema mradi wa Kaizen ni moja ya
mikakati stahiki ya sekta kadhaa ikiwamo sekta ya viwanda inayotokana na
mpango wa kitaifa wa maendeleo ya miaka mitano kuanzia mwaka 2011 hadi 2016.
Alisema mradi huo unatarajia kuwanufaisha
wafanyabiashara na wajasiriamali katika Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Dar
es Salaam. Alisema tayari wafanyabiashara walisha
shiriki katika mafunzo ya namna ya kuzalisha bidhaa kwa ubora yaliyotolewa na
Shirika la Jica.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Jica
hapa nchini, Yukihide Katsuta alisema lengo la kuanzisha mradi huo hapa nchini
ni kutoa fursa ya uzalishaji bidhaa zenye tija na ubora katika soko.
Katsuta mradi huo una lengo la kuongeza ubora na ufanisi wa utengenezaji wa bidhaa na kuweka mazingira salama katika maeneo ya kazi ili kuuza bidhaa zenye ubora.
No comments:
Post a Comment