To Chat with me click here

Monday, November 5, 2012

CHADEMA: CCM IMEWAWEKA REHANI WATANZANIA



CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeweka rehani maisha ya Watanzania kwa kutowapatia ipasavyo huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mmoja wa viongozi wa chama hicho taifa, Lukas Webiro, alipozungumza na wananchi wa kata ya Kisorya kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika kijijini hapo.

Webiro alisema hali mbaya waliyonayo Watanzania hususan wale wa vijijini imesababishwa na uongozi mbaya wa CCM, kwani Watanzania wengi sasa hawana imani na maisha yao kutokana na ugumu wa maisha.

Kiongozi huyo aliwaambia wananchi wa kata hiyo kuwa wao kama Watanzania walikiamini Chama cha Mapinduzi na kukiweka madarakani, lakini sasa kimewageuka kwani hata wawakilishi wao waliowachagua wakiwemo wabunge na madiwani hawawajibiki kwao ipasavyo.

“Hawa watu wanasema wamejenga zahanati, wamejenga shule na je waulizeni mbona hazina walimu na watumishi wa kutosha kuna haja gani ya kujenga shule na zahanati ambazo hazina watumishi wa kutosha?’’ alihoji Webiro.

Naye Gabriel Lukas ambaye ni mwanaharakati kutoka mkoani Arusha, alisema kuwa sasa hivi wananchi hawana imani tena na CCM, kwani rasilimali za nchi haziwanufaishi wazawa bali zinaliwa na kundi la wakubwa huku wengine wakihangaika.

Alisema pamoja na nchi kuwa na utajiri wa kutisha bado wananchi wake wanaishi maisha kama kuku wa kienyeji ambaye akiamka hajui atakula nini.

No comments:

Post a Comment