To Chat with me click here

Friday, November 9, 2012

UFISADI WA KUTISHA UZINDUZI JIJI LA ARUSHA


Rais Kikwete akizundua Jiji la Arusha.

UZINDUZI wa Jiji la Arusha uliofanyika wiki Ijumaa iliyopita (Oktoba 2,2012) umekomba hazina ya Jiji hilo kwa zaidi Sh milioni 100 kutumika kama gharama za sherehe hizo huku malipo mengi yakiwa wamejaa utata.

Jiji hilo lilizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa michezo wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid na kuhudhuirwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, kimataifa na wananchi wa Arusha.

Hata hivyo, pamoja na sherehe hizo kufana, tayari kuna taarifa za tuhuma kuwa sherehe hizo ziligubikwa na matumizi makubwa ya fedha za Halmashauri ya Jiji hilo, huku matumizi mengi yakionekana kutokuwa na lazima.

Katika mchanganuo wa awali ambao Raia Mwema imefanikiwa kuuona kama dokezo kwenda kwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Omar Mkombole kutoka kwa Mweka Hazina wa Jiji, K.A.Mpakata, Mhazini huyo aliomba kiasi cha Sh milioni 114,149,500 ili kufanikisha sherehe hizo.

Dokezo hilo lenye kumbukumbu namba MD/S.40/7.VOL 111 lililoandikwa Oktoba 30, lilikuwa na kichwa cha habari: “Yah. Gharama za uzinduzi wa Jiji ambazo zimewasilishwa kwa ajili ya malipo mpaka leo tarehe 30/10/2012,” likieleza kwamba katika kikao cha Kamati ya Fedha kilichofanyika Oktoba 23, mwaka huu, kiasi cha Sh 66,000,000 ziliombwa kwa ajili ya shughuli za uzinduzi wa Jiji, na kwamba makizio ya gharama hizo yalikuwa kabla ya ujio wa Rais Jakaya Kikwete.

“Lengo la kuandika barua hii ni kuonyesha hali halisi ya gharama tofauti na makisio yaliyopitishwa na kikao cha Kamati ya Fedha cha tarehe 23/10/2012,” lilisomeka dokezo hilo.

Habari zilizofikia Raia Mwema baada ya sherehe hizo za uzinduzi wa Jiji la Arusha, zinabanisha kwamba kiasi cha fedha hizo Sh milioni 100 zilizombwa katika dokezo hilo la Mweka Hazina, kilipunguzwa hadi kufikia zaidi ya milioni 95, kabla ya Kamati ya Fedha kukutana tena, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikiwa tayari matumizi yake yamefanywa na Mweka Hazina huyo pamoja na watumishi wengine wa Idara ya Fedha.

Kwa mujibu wa mchanganuo uliopo, fedha ambazo malipo yake yamezua utata katika dokezo hilo, yamehusu malipo kwa kikundi cha wasanii maarufu cha Orijino Komedi kutoka jijini Dar es Salaam, ambacho kinadaiwa kulipwa Sh milioni 12.0.

Malipo ya kiasi hicho cha fedha yalizua utata mkubwa hata katika kikao cha Baraza la Madiwani ambapo awali ilidaiwa kuwa wasanii hao walikubalina na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, kulipwa kiasi cha Sh milioni 5.0 kwa shughuli ya kutoa burudani katika sherehe hizo.

“Katika hali ya kushangaza, Mweka Hazina alilipa milioni saba zaidi tofauti na makubaliano ya awali na mkuu wa wilaya, kwamba wasanii hao wangelipwa Shilingi milioni tano tu,” kinaeleza chanzo chetu cha habari hizi.

Kibaya zaidi, chanzo hicho kinasema wasanii hao wachekeshaji wa Orijino Komedi hawakupata nafasi ya kufanya onyesho lao, zaidi tu ya kiongozi wao, Masanja, kupewa muda usiozidi dakika tatu kuwasalimia wananchi waliohudhuria.

Juhudi za Raia Mwema kumpata Mkuu wa Wilaya, Mongela, kuhusu taarifa hiyo ili kupata ufafanuzi zaidi hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni jana Jumanne.

Utata mwingine wa matumizi ya fedha, unapatikana katika malipo ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Diamond, ambaye anadaiwa kulipwa Sh milioni 10. Kama ilivhyo kwa wasanii wa Orijino Komedi, msanii huyo naye hakupata fursa ya kupanda jukwaani kutumbuiza baada ratiba ya shughuli hiyo kuvurugika kutokana na Rais Kikwete kuchelewa kuingia katika uwanja wa sherehe, na hivyo fedha hizo alizolipwa kwenda bure.

Taarifa zaidi zinadai kuwa hatua ya kuwaalika wasanii hao ilifikiwa kwa lengo la kuwavutia wananchi kuhudhuria sherehe hizo, na hasa kutokana na kile kinachodaiwa kuwa sababu za kisiasa. Inaelezwa kwamba mji wa Arusha ni ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivyo watu wengi wangepuuza sherehe hizo.

Mchanganuo huo umezidi kubainisha kuwa kiasi cha Sh 26,000,000 kilitumika kutengeneza fulana 3,000 wakati Sh 2,475,000 zilitumika kununua zulia jekundu ambalo mgeni rasmi angepita juu yake. Aidha, Sh 1,620,000 zinadaiwa kutumika kununulia njiwa 100 waliorushwa juu wakati wa uzinduzi huo, ikiwa ni sawa na wastani wa Sh 16,200 kwa kila njiwa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kwamba bei ya soko kwa njiwa moja ni kati ya Sh 2,500 na 3,000. Wachambuzi wa mambo wanasema bei iliyotumika kunulia njiwa hao, ya kiasi cha 16,000 kwa njiwa moja ni kubwa kuliko hata ya kuku wa kienyeji ambayo bei ya soko ni kati ya Sh 10,000 na 13,000.

Fedha nyingine zinazodaiwa kutumika vibaya ni pamoja na Sh 1,050,000 zilizolipwa kwa kikundi cha ngoma za Kimasai ambacho hata hivyo hakikutokea na wala hakikutumbuiza, pamoja na malipo ya Sh 1,500,000 kwa kikundi cha sanaa cha JKT Oljoro, ambacho nacho pia hakikupata nafasi ya kutumbuiza.

Utata mwingine ni malipo ya Sh 2,475,000 zinazodaiwa kununulia zulia jekundu. Hadi sasa, haijaweza kuwekwa wazi kama zulia hilo lilinunuliwa kweli au liliazimwa kutoka katika hoteli mojawapo za jijini Arusha. Kwa kiasi hicho cha fedha, Jiji lingekuwa na zulia lenye urefu wa mita zaidi ya 200 kwa wastani wa bei ya Sh 12,000 kwa mita moja ambayo ndiyo bei ya soko kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na gazeti hili.

Matumizi mengine yanayozua utata, ni malipo ya kukodisha Horn Speaker System kwa gharama ya Sh 1,000,000, uandaji wa ratiba ya sherehe za uzinduzi wa Jiji la Arusha Sh 1,200,000 na uandaaji na usambazaji wa barua za mialiko Sh 1,526,000.

Habari kutoka vyanzo vyetu vya kuaminika zinasema kwamba baada ya baadhi ya madiwani wa kambi ya upinzani kuanza kuhoji matumizi hayo, sasa maofisa wa halmashauri waliohusika na matumizi hayo wanahaha kuweka hesabu sawa kwa kugushi hati za malipo kabla ya taarifa za ufujaji huo wa fedha kuvifikia vyombo vya dola.

“Kwa jumla hali ni tete ndani ya Manispaa (ya Arusha). Tayari kuna maofisa wameanza kuwa matumbo joto wakihofu kuwa suala hilo linaweza kushikiwa bango na watendaji wa juu wa Serikali, hasa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye ni kati ya viongozi wanaofahamika kwa misimamo yao mikali kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma,” kinaeleza chanzo chetu kutoka ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumzia utata wa matumizi hayo ya mamilioni ya fedha, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Omar Mkombole alikanusha taarifa kuwa fedha hizo zimetumika vibaya, huku akisisitiza kufanyika kwa uhakiki wa matumizi ya fedha zilizotumika.

Anasema Mkombole: “Kwa sasa watu wa idara fedha wana ‘consolidate’ matumizi ya fedha na taarifa kamili itapatikana baada ya kesho (Jumanne) hivyo ni vizuri tusubiri, tuvute subira.”

Kwa uapande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo, akizungumza na Raia Mwema kwa simu, alisema hana taarifa kuhusu matumizi ya fedha kwa kuwa hakuwapo wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha.
“Sifahamu chochote kuhusu mchanganuo wa matumizi kwa kuwa kwa bahati mbaya nilikuwa nje ya ofisi kwa dharura hivyo sijui maamuzi waliyofikia,” alisema Lyimo.

Diwani wa CHADEMA, Kata ya Levolosi, Ephata Nanyaro, alisema wanapinga matumizi ya kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa sherehe ya saa tatu tu wakati halmashauri ina mahitaji mengi ya kuwahudumia wananchi.

“Walileta mchanganuo wao kwenye Baraza la Madiwani na sisi tulikataa kwa kuwa tayari kuna malipo mengi yalishafanyika tukawa tunawahoji tunajadili nini wakati malipo kama ya hawa wasanii wameshalipwa fedha? Binafsi kama kiongozi wa umma, nimesikitishwa sana na matumizi haya, naamni hata Mheshimiwa Rais akisikia fedha nyingi kiasi hiki zilitumika kwa suala la saa zisizozidi tatu, atasikitika sana,” anasema Nanyaro.

Diwani huyo alielekeza lawama kwa Kamati ya Fedha ya Baraza la Madiwani kwa kuridhia matumizi ya fedha hizo na kuongeza kuwa watumishi wasio waaminifu wanapata mwanya wa kuiba fedha za umma kutokana na udhaifu wa madiwani.



Jiji la Arusha lilizinduliwa wiki iliyopita baada ya danadana za muda mrefu kutoka serikalini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kisiasa na uongozi wa iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kushindwa kufanikisha mahitaji muhimu yanayokidhi kulifanya kuwa Jiji.

No comments:

Post a Comment