AKATA RUFAA, ADAI ADHABU ZILIZOTOLEWA NDOGO
MBUNGE wa
Ubungo na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameamua kulivalia
njuga suala la tuhuma za wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini
kujihusisha na vitendo vya rushwa, akisema kuwa uamuzi wa Spika Anne Makinda
umeacha makando kando mengi, ikiwemo ukiukwaji wa katiba ya nchi, hivyo
anajipanga kuukatia rufaa.
Alisema
kuwa uamuzi wa Spika Makinda uliotangazwa juzi bungeni, umefanyika kwa namna ya
‘funika kombe’, hivyo rufaa yake inalenga kutaka taarifa kamili ya Kamati Ndogo
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iwasilishwe kwa ukamilifu wake kwenye
kamati husika ya kudumu ya Bunge na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu’
katika usimamizi na uendeshaji wa sekta ya nishati zijulikane, kisha uchunguzi
wa kina ukihusisha vyombo vingine nje ya Bunge, ufanyike.
Alifafanua
kwa kurejea hotuba yake aliyosoma bungeni kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani
bungeni wakati wa Bunge la bajeti lililopita, akisema kuwa alitoa angalizo tangu
awali kuwa ili ukweli ujulikane ilipaswa kuundwa Kamati Teule ya Bunge
kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na
tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi
wa mafuta kwa ajili ya mitambo ya umeme.
Alisema ni
muhimu kufanyika kwa uchunguzi wa namna hiyo, ukihusisha pia Mkaguzi Mkuu
kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa
Puma Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali
waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme, kwa kuzingatia masharti ya
ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, siku moja tu baada ya Spika Makinda
kutoa uamuzi wake bungeni juu ya tuhuma za wabunge kujihusisha na rushwa,
Mnyika alisema kuwa atakata rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu’ kilichotolewa
na Spika hakilingani na ‘makosa’ ambayo yameelezwa kuwa na uzito wenye kuathiri
“kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge
waliohusishwa”.
Akitolea
mfano, Mnyika alisema kuwa ikiwa ni kweli Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi kuwa amefanya makosa ya kuvunja haki za Bunge kwa kuzusha
tuhuma za uongo ili kujihami dhidi ya wabunge waliokuwa wanahoji utendaji wake,
basi adhabu aliyopewa hailingani na ukubwa wa makosa anayodaiwa kufanya.
“Kwa kosa
hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati ni sahihi,
anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki
za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au
walau kutakiwa kuwajibika.
“Baada ya
uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma kwamba baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati ya
Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi
zao za kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari na wananchi kwa simu na
kwenye mitandao ya kijamii sababu za kusimama bungeni tarehe 9 Novemba 2012
mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba muongozo.
“Nakusudia
kukata rufaa kwa sababu uamuzi wake una maudhui kadhaa yasiyozingatia katiba ya
nchi, sheria mbalimbali za nchi, kanuni za kudumu za Bunge, maamuzi ya awali ya
maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu
wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge letu,” alisema Mnyika na kuongeza;
“Kwa
kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa, nilitaka niombe muongozo wake
kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini,
hivyo Spika anapaswa kuueleza umma iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa
kamati nyingine au kuelekeza kamati nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa
kuisimamia serikali wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye
sekta za nishati na madini yenye athari kwa maisha ya wananchi.”
Aliongeza kusema
kuwa, kwa kuwa katika uamuzi wake Spika Makinda alieleza kwamba Waziri wa
Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Maswi wametoa
maelezo yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali, uwepo wa Kamati ya Bunge kwa
ajili ya kuisimamia wizara hiyo kwa niaba ya Bunge ni suala linalohitaji uamuzi
wa haraka kutokana na hali ya nchi juu ya sekta ya nishati kuwa tete bila
usimamizi wa kibunge.
Aidha,
katika taarifa yake hiyo, Mnyika ameonekana kushangazwa na kitendo cha Spika
Makinda kutoa onyo kali kwa Katibu Mkuu na wabunge kadhaa, lakini hakutoa onyo
kwa Waziri wa Nishati na Madini wala hakueleza chochote iwapo alipokea ushauri
kutoka kwa Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu ukiukwaji
wa kanuni uliofanywa bungeni wakati wa kadhia nzima.
Akikumbushia
hadidu rejea moja tu iliyopewa Kamati Ndogo iliyofanya uchunguzi ya “Kuchunguza
na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya
Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana”,
hivyo, kwa mujibu wake, baada ya uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake Spika
alipaswa kuanzisha mchakato wa adhabu, kama kulibainika kuwepo kwa makosa ya
ukiukwaji wa kanuni.
Alisema
kuwa uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna tofauti na maamuzi yaliyotangulia
ambayo yamesababisha mpaka sasa serikali haijawasilisha bungeni ripoti ya
utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Jairo, kufuatia uchunguzi uliofanywa na Kamati
Teule ya Bunge.
No comments:
Post a Comment