To Chat with me click here

Monday, November 19, 2012

JK, KINANA WAWATISHA WANAOTAKA URAIS 2015



KINANA AAHIDI KUWASHUGHULIKIA WANAOPANGA SAFU


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewataka wanachama wenye nia ya kugombea urais kuacha kunyoosheana kidole na kukigawa chama, kwani chama hicho si mali ya mtu.

Pamoja na kutowataja wanachama hao, lakini makundi makubwa yanayotajwa kuwa katika vita ya kuwania urais 2015 ni lile la Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowasa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma hivi karibuni, Rais Kikwete alikaririwa akisema hausiki wala kuyaunga mkono makundi hayo kwa namna yoyote ile.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa hadhara na wanachama wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele kuongoza makundi katika migogoro kwa lengo la kujihakikishia kuwa mwaka 2015 wanaupata urais hata kama chama kitakufa.

“Chama hiki siyo mali ya mtu, hivyo kila mtu ana haki ya kugombea nafasi yoyote anayoitaka, kama chama hiki kingekuwa mali ya mtu basi kusingekuwa na haja ya kufanyika uchaguzi kila baada ya miaka mitano,” alisema Kikwete.
Kikwete aliwataka wale wote wenye nia ya kuwania urais kuacha kujiingiza kwenye migogoro ambayo inazidi kukiweka chama kwenye nafasi mbaya katika kushinda kila chaguzi.

Migogoro na mipasuko ndani ya chama hicho imekuwa sababu ya chama hicho kupoteza baadhi ya majimbo na kata zake.

Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi kuhakikisha wanarudisha imani kwa wanachama na kukifanya chama hicho kuingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 kikiwa kimoja, ili kujijengea mazingira ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alitoa mfano kuwa katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma, baadhi ya watu walifikia hatua ya kuangaliana kwa jicho la husuda. Alisema kama chama hicho kitakuwa hakina umoja basi chama kitakuwa kwenye nafasi ngumu ya kushinda chaguzi hizo. Aidha Kikwete alisema kuna ulazima wa kujipanga katika kupambana na propaganda za wapinzani na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimejiingiza kwenye siasa.

Alisema kwa vyama vya siasa kuwakosea hiyo ni kazi yao wala hawashangai kwa kuwa wanapiga siasa, ili wapate kuaminika kwa jamii.
“Kwa vyombo vya habari kulaumu serikali kila siku kuwa hakuna kinachofanywa na seriakali yetu, si sawa; yaani hakuna hata jema wakati tunajenga barabara?” aliuliza.

Kikwete pia aliwataka wanachama wa chama hicho kuweka mikakati ya kukifufua chama ambacho kimepoteza muelekeo na kuchukiwa na baadhi ya wanachama. Alisema ni lazima kila kiongozi na mwanachama kujiuliza ni wapi wamekosea kwa lengo la kujikosoa, ili kurudisha imani.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdrahaman Kinana, alisema atahakikisha anakomesha tabia ya baadhi ya viongozi wanaopanga safu zao kwa kutumia kukigawa chama huku wakitumia rushwa.

Alisema tabia hiyo imesababisha mmomonyoko wa maadili ambao unasababisha chama hicho kupoteza sifa ya kuwa chama cha siasa. Alisema sekretarieti mpya iliyoingia madarakani itahakikisha inakomesha vitendo vyote vinavyosababisha chama hicho kupoteza sifa na kukifanya kuwa chama cha wanachama wote.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, alisema hawatamuogopa mtu na kwamba watahakikisha yeyote aliyeingia kwa rushwa atachukuliwa hatua zinazostahili, kwani hawawezi kuwa na viongozi wanaoingia madarakani kwa kuwanunua watu kama sambusa.

Pia alisema chama hicho hivi sasa kitaelekeza nguvu zake kukiimarisha kutoka chini, hivyo aliwataka mabalozi wa nyumba kumi kuhakikisha nao wanakuwa mstari wa mbele kupambaana na vitendo vya rushwa.

Alisema walioingia katika uongozi kwa kutumia rushwa, ndani ya miezi sita watatoka nje na hata wale waliokuwa wakitumikishwa kwa kushika bahasha za rushwa nao pia watashughulikiwa.

“Tutahakikisha tunasafisha chama pia na nyie wanachama msikubali kununuliwa kama sambusa,” alisema Mangula. Alisema nia yao ni kukabiliana wa wanachama wanaotoa rushwa na kurudisha sifa ya chama hicho chenye zaidi ya wanachama milioni 6.

Mangula alisema watahakikisha wanajenga chama imara na kukirudisha kwa wanachama wa chini na asiyeweza kwenda na kasi hiyo aondoke haraka.

No comments:

Post a Comment