Mhe. Lazaro Nyarandu |
SERIKALI
imesema licha ya jitihada zinazofanywa kumaliza tatizo la ujangili kwenye
hifadhi za taifa hususan mapori ya akiba, tatizo hilo linazidi kukua kutokana
na baadhi ya watumishi kujihusisha na vitendo hivyo.
Akizungumza kwenye mahafali ya Chuo cha Hifadhi ya Wanyamapori na Utalii Afrika (Mweka), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema serikali inatambua ongezeko la ujangili kwenye hifadhi na inafanya kila linalowezekana kumaliza tatizo hilo.
Nyalandu
alisema imekua vigumu kumaliza haraka tatizo la ujangili kutokana na baadhi ya
watumishi kutokuwa waaminifu na kuwa na tamaa, hatua inayosababisha
washirikiane na majangili kuua wanyama hususan tembo ambao meno yao kwa sasa
yanauzwa kwa bei kubwa bara la Ulaya na Asia.
“Bei
ya meno ya tembo imepanda sana miaka ya nyuma jino moja liliuzwa dola 100 za
Marekani, hivi sasa bei imepanda jino moja ni dola 1,000 hadi 1,100 na hii
ndiyo imewafanya watumishi wetu kupata tamaa na kujiingiza kwenye biashara
haramu,” alisema Nyalandu.
Alisema
kutokana na kushamiri kwa ujangili tayari serikali imeongeza mfumo wa uchunguzi
kwa kushirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi, ili kutoa siri na kupiga
marufuku uingizaji silaha za kivita ambazo zinatumiwa kuua wanyama.
Kuhusu
watalii, Nyalandu alisema hivi sasa zaidi ya watalii 800,000 wanaingia nchini
kwa mwaka na kwamba, lengo ni kufikia zaidi ya watalii milion moja ifikapo
mwaka 2015.
Awali,
Kaimu mkuu wa chuo hicho, Freddy Manongi alisema kumekuwapo na ongezeko kubwa
la wanafunzi kutoka 25 mwaka 1963 hadi 502 mwaka huu, hali ambayo imechangia
kuwapo changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa vifaa vya kufundishia.
Changamoto
zingine ni uhaba wa vitendea kazi kama magari kwa ajili ya wanafunzi kwenda
kujifunzia, miundombinu kama mabweni, madarasa, maabara na nyumba za walimu.
No comments:
Post a Comment