WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
na mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwan wamezungumzia tuhuma ambazo zimekuwa
zikielekezwa kwao kwamba wanamiliki rasilimali zenye thamani ya mabilioni ya
shilingi.
Lowassa kwa upande wake amekuwa
akidaiwa kuwa tajiri anayemiliki kampuni kubwa za kibiashara na kumekuwa na
taarifa kwamba ana ukwasi ambao vyanzo vyake vinatia shaka na siyo rahisi
kuvitolea maelezo.
Kwa upande wake Ridhiwan naye amekuwa
akidaiwa kuwa na utajiri mkubwa na amekuwa akihusishwa na biashara za kampuni
za kusafirisha mafuta ambayo hupelekwa kwenye migodi, umiliki wa hoteli na
majengo kadhaa ya kifahari.
Wote wawili wamekuwa wakidaiwa kwamba
baadhi ya mali zao wamekuwa wakiziendesha chini ya kivuli cha wafanyabiashara
wengine wakubwa nchini ili kukwepa kuhojiwa walikotoa utajiri huo, taarifa
ambazo hata hivyo imekuwa vigumu kuzithibitisha.
Hata hivyo jana kwa nyakati na
mazingira tofauti, Lowassa na Ridhiwan walijitokeza hadharani na kukanusha
madai kwamba wao ni matajiri wa kupindukia.
Lowassa kwa upande wake akiwa mjini
Mbeya alisema yeye siyo tajiri kama ambavyo imekuwa ikidaiwa lakini wakati
huohuo akasema “sijafilisika”.
“Wengi wanasema kuwa mimi ni tajiri
siyo kweli, lakini sijafilisika kutokana na kuchangia makanisa kwani nina
marafiki wengi ambao wananisaidia katika kuchangia makanisa nao pia
hawajafilisika,”alisema Lowassa.
Lowasa alitoa kauli hiyo alipokuwa
akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wanawake ambao
ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji cha mkoani Mbeya,
kinachomilikiwa na Kanisa la Moraviani Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye alichangia kaisi
cha Sh25 milioni, alisema kila mtu ana wajibu wa kuchangia elimu na kwamba
mwanamke anapaswa kutazamwa kwa karibu zaidi kwani ndiye anayebeba jukumu kubwa
la kutunza familia.
Kwa upande wake Ridhiwan alisema:
“Ikiwa mimi ni tajiri wa kiasi kinachosemwa, basi mimi ninamzidi Bakhressa
(Said Salim, mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki), maana nimepewa kila
hoteli hapa mjini, kampuni za mafuta na kila biashara kubwa inayoanzishwa hapa
mjini ni ya Ridhiwan”.
Said Salim Bakhressa ni mfanyabiashara
ambaye anatajwa kuwa tajiri kuliko wote nchini na anashika nafasi ya pili
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, huku akiwa miongoni mwa
wafanyabiashara 10 wanaonyemelea kuingia katika nafasi za juu za utajiri
Afrika.
Hata hivyo Ridhiwan ambaye hivi
karibuni alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC),
aliongeza: “Ninaweza kuwa nafanya biashara moja au mbili, lakini siwezi kuwa
mmiliki kiasi chote hicho cha mali.
Mtoto huyo wa Rais Kikwete alikuwa
akijibu tuhuma kwamba magari yake kumi ya kusafirisha mafuta yamekamatwa na
kuzuiwa katika mpaka wa Kenya na Tanzania, Namanga mkoani Arusha kutokana na
kukwepa kodi, taarifa ambayo aliikanusha.
No comments:
Post a Comment