To Chat with me click here

Thursday, November 29, 2012

PESA ZA KIGENI, UPUNGUFU WA NISHATI VYAYUMBISHA SHILINGI YA TANZANIA


Watu kutoka mji wa Wete Zanzibar wakinunua chakula sokoni. Bei za chakula zilipanda karibuni hadi kufikia asilimia 100 kutokana na kubadilikabadilika kwa bei za fedha za kigeni.
Kubadilikabadilika kukubwa kwa bei za chakula ambako Tanzania imeshuhudia katika miezi ya karibuni ni ishara kwamba uchumi wa nchi haukutengamaa kimuundo, wanauchumi wasema. 

Baada ya bei za chakula kushuka kwa muda mfupi kutokana na kukaribia kwa msimu wa mavuno wa mwezi Oktoba, zilipaa tena mwezi wa Novemba baada ya nchi kukumbwa na uhaba wa mafuta. 

Kwa mujibu wa data zilizotolewa tarehe 23 Novemba na Wizara ya Viwanda na Biashara, baadhi ya bei za mazao zilipanda hadi kufikia asilimia 100 katika wiki za mwanzo za mwezi huu. 

Kwa mfano, mjini Dar es Salaam, bei kwa kila kilo moja ya maharage ilipanda kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola) hadi shilingi 1,200 (senti 75 za dola), bei ya mahindi ilipanda kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola) hadi shilingi 700 (senti 44 za dola), mchele kutoka shilingi 1,600 (dola 1) hadi shilingi 2,200 (dola 1.37) na unga wa ngano kutoka shilingi 600 (senti 37 za dola ) hadi shilingi 900 (senti 56 za dola). 

Ili kujilinda dhidi ya kuanguka kwa bei ya shilingi, Watanzania wengi wanategemea dola ya Marekani na pesa nyengine za kigeni kwa ajilli ya kununua na kuuza bidhaa, utaratibu ambao unazidisha kuiyumbisha pesa ya nchi na kusababisha kupaa kwa bei za chakula, kwa mujibu wa Mushengezi Nyambele, mchumi na katibu wa zamani wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania. 

"Hata watu wa kawaida wamepoteza imani na fedha yetu," aliiambia Sabahi. "Wote wanachagua dola, jambo ambalo husababisha uhaba wa dola nchini, na kwa hivyo kuchochea kuongezeka kwa bei." Alisema kuwa mafuta yanapanda kwa sababu mzunguko mdogo wa dola nchini Tanzania, badala yake kuathiri bei za bidhaa na huduma.

Nyambele alisema kuwa kuyumba kwa sehemu kunatokana na kushindwa kwa sera za serikali za fedha.

Matumizi ya fedha za kigeni kwa biashara ya ndani ni haramu nchini Tanzania, lakini serikali haijaweza kusimamia kwa ufanisi kuimarisha marufuku hiyo, Nyambele alisema. "Ni rahisi kupata fedha za kigeni nchini Tanzania kuliko popote ulimwenguni," alisema, na kuongeza kuwa dola za Marekani ni asilimia 95 ya fedha zote za kigeni zinazotumika nchini.

Benki ya Tanzania inapaswa kuzuia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa wafanyabiashara wa kimataifa na wasafiri kwa matumizi ya nje, alisema.
Mwezi wa Julai, Waziri wa Fedha William Mgimwa aliliambia bunge kuwa serikali ilikuwa na habari juu ya matumizi mabaya ya biashara za jamii na kuahidi kuwa serikali ingefanyia kazi kuziba mianya. 

Msemaji wa serikali Assah Mwambene aliiambia Sabahi kuwa utawala inakamilisha mkakati mpana wa kuondosha matumizi yasiyosimamiwa ya fedha za kigeni katika soko la ndani, lakini akakataa kuweka wazi ni lini sera hiyo itaanza kufanya kazi.

Uhaba wa akiba ya nishati wazuwia uchumi

Pamoja na hayo, ukosefu wa akiba imara ya nishati unasababisha changamoto kubwa zaidi kwa uchumi kuliko matumizi haramu ya fedha za kigeni, kwa mujibu wa mwanauchumi Honest Ngowi, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

"Tunahitaji kuupanua uchumi wetu na [kujenga] usalama wa nishati ili kujenga uchumi ulio imara," aliiambia Sabahi. "Tunahitaji kuwa na mpango maalumu wa vyanzo vya nishati ili kuepuka mifadhaiko ya nje." 

Serikali inapaswa kutumia kidogo zaidi na kutoa sera za kusimamia vizuri zaidi vyanzo vya nishati na kujenga uchumi utakaoweza kufyonza mabadiliko ya masoko bila ya kuathiri sana bei za walaji ambazo hulipia mitaani, Ngowi alisema.

Alisema kuwa akiba ya mafuta ya Tanzania ni sawa na siku 15 za matumizi, ambayo huufanya uchumi wa taifa kuwa katika hatari kwa mabadiliko ya masoko ya ndani na ya kimataifa. "Tunahitaji kuweka malengo ya muda mrefu, kama vile kuwa na mafuta ya kutosha ili kuusaidia uchumi wa nchi kwa muda wa miezi minne," alisema.

Utulizaji wa uchumi unaweza kufikiwa tu kwa kuweka sera za fedha ili kurahisisha uwekezaji wa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na matangi makubwa ya akiba na miundombinu mengine ili kusaidia vyanzo mbadala vya nishati, alisema.

TUME YA UCHUNGUZI WA AJALI YA BOTI ZANZIBAR WATAKA KUSHTAKIWA KWA MMILIKI WA MELI, MAAFISA WA SERIKALI



Tume moja ya serikali ya Zanzibar imependekeza kushtakiwa kwa mmiliki wa meli na maafisa wote wa bandari waliohusika na ajali ya boti mwezi Julai iliyopoteza maisha ya watu 81 na kusababisha zaidi ya 200 ambao bado hawajapatikana, liliripoti gazeti la Daily News la Tanzania.

"Mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti yanajumuisha hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya wale wote waliotajwa ndani yake," alisema Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na kiongozi wa tume hiyo, Abdulhakim Ameir Issa. "Tume pia imeishauri serikali kupitia sheria za usalama baharini na kuimarisha idara ya uokozi na udhibiti wa majanga."

Ripoti ya tume hiyo ilitaja uzembe, ufanyaji kazi usio wa kitaalamu na kutowajibika kama sababu kuu za ajali ya meli ya MV Star Gates, ambayo ilikuwa ya pili kuzama ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Tume hiyo pia ilithibitisha kwamba boti hiyo ilikuwa imebeba abiria 447, zaidi kabisa na idadi ya abiria 290 iliyotajwa katika orodha rasmi ya abiria.

Ripoti hiyo pia ilitaka kufidiwa kwa kila mtu aliyehusika kwenye ajali hiyo, zikiwemo familia za marehemu, wale waliojeruhiwa na wasiojeruhiwa kwa angalau shilingi 125,000 (dola 78) kila mwezi kwa miezi 80.

Boti ya MV Star Gates ilizama karibu na Kisiwa cha Chumbe kiasi cha saa 7:50 mchana, kwa mujibu wa Mwinyihaji Makame Mwadini, waziri wa dola katika ofisi ya rais na mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.