Naibi Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyarandu |
NAIBU Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (pichani) anadaiwa kumiliki kampuni
inayojishughulisha na masuala ya utalii kitendo ambacho kinamwingiza kwenye
mgongano wa kimasilahi.
Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa Nyalandu anamiliki Kampuni ya Nitoke Safaris Ltd
jambo ambalo limeelezwa kuwa ni kinyume na Kanuni za Utumishi wa Umma hasa kwa
kuwa yeye ni msimamizi wa sekta hiyo.
Taarifa
kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni na Leseni (Brela), zinaonyesha kuwa
wamiliki wa Kampuni hiyo ni L.S.Nyalandu na Faraja G. Nyalandu, huku kila mmoja
akimiliki asilimia 30 ya hisa.
Kampuni hiyo ilisajiliwa Aprili 24, 2009 na kupewa nambari 70735, wakati huo Nyalandu akiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, wadhifa alioupata kuanzia mwaka 2000.
Ofisi za
kampuni hiyo ziko PPF Complex Suit, namba 24 Barabara ya Mzingo, Arusha na
magari ya kampuni hiyo yamekuwa yakibeba watalii mkoani Arusha.
Alipoulizwa
kuhusu madai hayo jana akiwa Mwanza, Waziri Nyalandu alikiri kuwa mmoja wa
wamiliki wa kampuni hiyo lakini akasema tayari alishajitoa.
Katika
kujenga hoja ya utetezi wake, Nyalandu alisema kama ambavyo haipendezi yeye
kumiliki kampuni ya utalii akiwa waziri wa wizara hiyo, haitapendeza pia waziri
wa habari kumiliki gazeti.
“Huwezi kuwa
Waziri wa Utalii na ukafanya biashara ya utalii huko katika kampuni hiyo mie
nilishatoka kitambo,” alisema bila kufafanua zaidi.
Hata hivyo,
kumbukumbu za Brela zinaonyesha kuwa waziri huyo bado ni mmoja wa wanahisa
ingawa haijafahamika kama ni tatizo la Brela kutorekebisha kumbukumbu za jalada
lake baada ya kujitoa au la.
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alipoulizwa na gazeti hili jana
alionyesha kushtushwa na taarifa hizo na kusema hajui kama Naibu wake anamiliki
kampuni ya utalii.
“Siwezi ku comment (kutoa maoni), chochote juu ya jambo hilo kwa sababu sijui kama ana kampuni ya utalii na pili, ndiyo kwanza nasikia hizo taarifa kutoka kwako (mwandishi),” alisema Kagasheki.
Taarifa
zilizowakariri baadhi ya mawakala wa utalii mikoa ya Kilimanjaro na Arusha
zilidai kuwa Nyalandu ni mmoja wa washindani katika biashara hasa ya kwenda
mbuga za wanyama.
Haijafahamika
kama Nyalandu aliwahi kutangaza kuwa na masilahi na kampuni hiyo au kama
aliwahi kuiorodhesha kama moja ya mali anazomiliki kama Sheria ya Maadili ya
Viongozi inavyotaka.
“Siyo tatizo kiongozi kumiliki kampuni, lakini unatakiwa ku-declare interest (kutangaza masilahi) lakini kwa Nyalandu ni tofauti kidogo kwa sababu sasa yuko kwenye sekta hiyo,” alidokeza wakili mmoja.
Wakili huyo
ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema hata kama Nyalandu atakuwa haipi
upendeleo kampuni hiyo, lakini kwa akili ya kawaida, ni rahisi binadamu kuhisi
kampuni hiyo itakuwa ikipewa upendeleo wa aina fulani.
Hata hivyo,
Wakili mwingine, Albert Msando wa Arusha, alisema kwa dhana nzima ya utawala
bora, Waziri wa Maliasili na Utalii au Naibu wake au watendaji wa Tanapa
hawapaswi kumiliki kampuni ya utalii.
“Kwa waziri
ku-declare interest (kutangaza masilahi), haitoshi kwa sababu kwanza ndiyo
itachochea zaidi watu kufanya biashara na kampuni yako hata kama hauko kwenye
utendaji wa kila siku,” alisema.
“Waziri anaingia vikao vyote vya kusimamia sekta ya utalii…unaenda nje kwenye maonyesho kwa nini watu wasiamini unapokwenda huko unatangaza pia kampuni yako kwa fedha za Serikali?” alihoji.
Septemba 11,
2009, Rais Jakaya Kikwete alinukuliwa akisema mchakato wa kutungwa kwa sheria
mpya ya kutenganisha biashara na siasa upo katika hatua za mwisho na
ungewasilishwa bungeni.
Rais Kikwete
alikuwa akizindua Baraza la Usimamizi la Taifa (NGC) la Mpango wa Kutathmini
Utawala Bora barani Afrika (APRM), katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Alisema madhumuni ya kutenganisha biashara na siasa kwa watumishi wa umma itawapa fursa viongozi kuwatumikia wananchi kwa karibu zaidi katika kufanikisha dhana ya utawala bora.
Hata hivyo,
Serikali haijapeleka muswada huo bungeni ambao ungewazuia viongozi wa kisiasa
wakiwamo madiwani, makatibu wakuu wizarani, wabunge na mawaziri kujihusisha na
biashara.
Tuhuma dhidi
ya Waziri Nyalandu zimekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti taarifa
kuwa aliingilia utendaji kazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kwa
masilahi binafsi.
Nyalandu
anadaiwa kuiandikia barua Menejimenti ya Tanapa akiiagiza ikutane na Kampuni ya
Ahsante Tours ambayo ilikopeshwa kinyemela na Tanapa hadi deni kufikia
Dola 80,000 za Marekani.
Utaratibu
unataka kampuni ya utalii inayotaka kupandisha mgeni mlimani kulipia kwa kadi
benki.
Mgogoro huo umeibuka baada ya Tanapa kuifungia kampuni hiyo kwa udanganyifu, lakini Waziri Nyalandu akaingilia kati na kuiamuru Tanapa kukutana na Ahsante Tours na kumaliza mgogoro huo.
Jumatatu
iliyopita, Nyalandu aliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam
akidai kuwa uamuzi wa Tanapa wa kuifungia Ahsante Tours ulikuwa wa dhuluma na
kuituhumu Tanapa kwa rushwa.
Agizo hilo
la Nyalandu limeibua mtafaruku mkubwa huku kampuni nyingi za utalii zikihoji
ilikuwaje Tanapa iiruhusu kampuni hiyo kupitisha wageni bila kulipa ada stahili
kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment