Chama cha
Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Tas) mkoani Mwanza, kimelaani vikali kitendo cha
familia moja wilayani Magu kumzika ndani ya chumba cha biashara mtoto wao
mwenye ulemavu wa ngozi (albino).
Mtoto
huyo aliaga dunia Desemba 15, mwaka huu nyumbani kwao mjini Magu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Tas Mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole, alisema kimsingi chama chake
hakikubaliani na kitendo hicho ambacho kilifanyika usiku wa manane bila
kuishirikisha jamii ya eneo husika.
Kapole,
ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wenzake wa chama hicho mkoani Mwanza na
taifa, alisema hatua yao ya kulaani kitendo hicho inatokana na ukweli kuwa
inaweza kuchochea mauaji dhidi ya albino.
Alifafanua
kuwa wiki iliyopita, alipokea taarifa kutoka wilayani Magu kuwa mtoto mwenye
ulemavu wa ngozi, Witness Edward Omari, mwenye umri wa miaka miwili na miezi
saba, mkazi wa mtaa wa Isandula mjini Magu, amefariki dunia na mwili wake
kuzikwa ndani ya chumba cha biashara kinachomilikiwa na baba yake.
Aidha,
alisema taarifa hizo zilieleza kuwa siyo tu kwamba mtoto huyo alizikwa ndani ya
chumba cha duka, bali pia kitendo hicho kilifanywa usiku wa manane bila jamii
ya eneo husika kushirikishwa.
“Nilipigiwa
simu na mwenzetu mmoja kutoka Magu akaniambia kwamba baada ya Witness kufariki
dunia, alizikwa ndani ya chumba cha duka, na kweli tulipokwenda kuitembelea
familia yake, tuliingizwa ndani ya chumba hicho kuonyeshwa kaburi lake,”alisema
Kapole.
Aliongeza
kwamba taarifa zaidi walizozipata zinasema kuwa mwili wa mtoto huyo
ulichukuliwa na wazazi wake kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya
Wilaya ya Magu Desemba 16, mwaka huu majira ya usiku kwa ajili ya kwenda
kuuzika.
Ofisa
Uhusiano wa Tas taifa, Josephat Toner, alisema wao kama jamii ya albino,
hawakubaliani na kitendo hicho kwa sababu kinakiuka misingi ya ubinadamu na pia
kinaweza kuchochea mauaji dhidi yao.
Alisema
katika jamii nyingi za Watanzania, wanaamini kuwa albino hawafi kifo cha kawaida
bali hupotea, hali ambayo imekuwa ikichochea mauaji dhidi yao kwa baadhi ya
watu kudhani kuwa viungo vyao si vya kawaida na vinaweza kusababisha utajiri.
Kwa
msingi huo, alisema kitendo cha familia ya Witness kumzika mtoto wao ndani ya
chumba cha biashara tena usiku wa manane pasipo kuishirikisha jamii, kinaweza
kuchochea imani hiyo potofu kwamba albino hawafi bali hupotea.
“Albino
ni binadamu kama binadamu wengine, tunazaliwa na kufa, hivyo mazishi yetu
yanapaswa kufanyika hadharani kama vile mazishi ya watu wengine yanavyofanyika,
lazima `wananzengo’ (wanajamii) washiriki kwa taratibu zilizozoeleka ili
kuondoa kabisa dhana potofu kwamba hatufi bali tunapotea,” alisema.
Kwa
upande wake, Katibu wa Tas Mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju, alisema kitendo kilichofanywa
na familia ya Witness, kimewatia simanzi kiasi cha kuwafanya wawe na hisia
mbaya dhidi ya familia hiyo.
Alifafanua
kwamba ingawa Witness alikufa kifo cha kawaida baada ya kuugua kwa muda mfupi,
lakini namna ambavyo mwili wake umezikwa ndiko kunakowatia shaka na kuhisi kuwa
huenda kuna jambo limejificha.
Alisema
kama lengo la familia hiyo lilikuwa kuepusha uwezekano wa watu wenye imani
potofu kufukua kaburi la mtoto wao, ni bora wangemzika katika makaburi ya
jamii na kujengea zege lakini sio kumzika ndani ya chumba cha biashara tena kwa
siri.
“Kutokana
na mazingira ya tukio lenyewe, kama chama tumeamua kufungua jalada la shaka na
kuiomba mahakama itoe kibali kwa Jeshi la Polisi kufukua kaburi la Witness ili
tujiridhishe iwapo kweli mwili wake una viungo kamili kwa sababu hata mahali
penyewe tulipoonyeshwa kuwa ndipo alipozikwa, hapaonyeshi dalili hizo,”
alisema.
Alipoulizwa
kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu,
alisema hajapata taarifa.
Hata
hivyo, alisema kama tukio hilo lipo ni vema viongozi wa Tas wakamuona Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Magu ili alishughulikie.
“Mimi
sina taarifa pengine Tas walikuja ofisini wakati nimetoka, lakini nitafuatilia
kujua kama walizungumza na wasaidizi wangu ili tumwelekeze OCD alishughulikie
ingawa suala la kufukua kaburi linahitaji kwanza kibali cha mahakama,” alisema
Kamanda Mangu.
No comments:
Post a Comment