To Chat with me click here

Tuesday, December 18, 2012

UONGOZI CHADEMA KARATU WASIMAMISHWA



Kamati  Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeusimamisha uongozi wa chama hicho Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, baada ya kubaini kasoro za utendaji wa viongozi wake.

Kufuatia uamuzi huo, shughuli za utendaji wa chama wilayani humo sasa zitakuwa chini ya uangalizi wa Kamati Kuu mpaka hapo itakapotolewa maagizo mengine.

Ofisa Mwandamizi wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kwamba uamuzi huo ulichukuliwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha kawaida cha siku mbili, kilichofikia tamati juzi usiku, jijini Dar es Salaam.

“Kamati Kuu ilichukua uamuzi wa kusimamisha uongozi mzima wa Wilaya ya Karatu na kuweka shughuli za utendaji wa chama chini ya uangalizi wa Kamati Kuu mpaka hapo itakapotolewa maagizo mengine baadaye” alisema Makene.

Alisema uamuzi huo ni sehemu ya maazimio ya kikao hicho na kwamba, maazimio yote yatatolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari leo.

Makene alisema wamelazimika kutoa ufafanuzi wa awali kutokana na kuwapo kwa taarifa zinazowakanganya wanachama na Watanzania kwa jumla zilizoandikwa juzi na jana katika baadhi ya vyombo vya habari.

Alisema katika kikao hicho, Kamati Kuu ilijadili masuala mbalimbali, ikiwamo kupokea taarifa ya hatua kadhaa za utekelezaji wa maazimio yatokanayo na vikao viwili vilivyotangulia.

Pia ilijadili hali ya siasa nchini, mchakato wa Katiba Mpya na Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na pia ilipokea taarifa ya mwenendo wa chama kutoka maeneo mbalimbali nchini na kujadili pia kasoro za utendaji wa viongozi wa chama katika wilayani humo.

Vilevile, ilipokea na kujadili mwenendo wa utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa taasisi za kiserikali wanaotokana na Chadema, hasa katika masuala ya ardhi na maji Wilayani Karatu.

Makene alisema kikao hicho pia kilibaini kuwa taarifa zinazohusu masuala hayo ya maji na ardhi ni tofauti na namna zilivyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment