To Chat with me click here

Sunday, December 23, 2012

WAHAMIAJI HARAMU WAVAMIA TEMBO


USALAMA wa Tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi uko mashakani kufuatia kuwepo kwa vitendo vya uwindaji wa wanyama hao unaofanywa na watu wanaoaminika kuwa ni wahamiaji haramu.

Wawindaji hao husafirisha pembe hizo za Tembo na kuzipeleka nchi jirani ya Rwanda kwa ajili ya kuziuza.

Uchunguzi uliofanywa na vyanzo vya habari hii Jumapili na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Constantine Kanyasu, umebaini kushamiri kwa wahamiaji haramu wanaojihusisha na ufugaji na wamekuwa wakiingia kinyemela nchini na kuendesha shughuli za ufugaji katika ardhi ya Tanzania na baadhi yao kuendesha vitendo vya uhalifu.

Baadhi ya wananchi katika vijiji vya Kasulo na Ngoma wilayani Ngara walisema wahamiaji hao wamekuwa wakifika na mifugo yao na kujifanya wafugaji lakini wamekuwa wakishughulika na uwindaji haramu ikiwa ni pamoja na uuwaji wa Tembo na kisha kuuza pembe nchini Rwanda.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kasulo, (Ramadhani Luzuba) alisema wahamiaji hao ambao wamekuwa wakiendesha shughuli za ufugaji, wamekuwa wakifanya uharamia huo kwa msaada wa maofisa wa Idara ya wanyamapori.

“Hawa wafugaji wa Rwanda wamekuwa wakipanga na askari wanyamapori, wanapotaka kuuwa Tembo ni lazima wawasiline na askari wa Pori, wanapokubaliana basi ni lazima utoe fedha na kila Tembo mmoja anayeuawa wauaji hulipia kiasi cha Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni,” alieleza mmoja wa wafugaji.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, wafugaji wengi wanaojihusisha na uwindaji wa Tembo wamekuwa wakiuza pembe za ndovu na kununua Ng’ombe ambao wamekuwa wakiwafuga porini, na kisha ng’ombe hao wanapofika zaidi ya 500 au 1000 wamekuwa wakiuzwa na kupeleka  fedha kwao.

Mauaji ya Tembo
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasulo, wilayani Ngara, Yusuf Katura  alisema kwamba kwa takwimu walizonazo hadi sasa jumla ya Tembo 19 wameuawa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na wafugaji hao.

Idadi hiyo inafanya idadi ya jumla ya Tembo 37 ambao watakuwa wameuawa na majangili katika Pori la Hifadhi ya Burigi iliyopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

“Tatizo kubwa ni hawa wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia porini kwa kisingizio cha ufugaji, wengi ni raia kutoka nchi za Rwanda na Burudi. Hawa wafugaji wageni wanaua sana Tembo, na ikitokea wakati wa kuua Tembo akawapo mwana kijiji akawaona, basi kinachotokea aliyewaona uuawa na kama ni mwanamke hubakwa ama kupigwa,” alieleza Katura.

Taarifa za ndani kutoka katika Hifadhi ya Burigi, zilidai kwamba jumla ya Tembo kumi waliuawa mwezi Julai mwaka huu katika maeneo ya Kulushasha na ndani ya hifadhi hiyo na kuongeza kati ya Tembo hao, watatu waliuawa katika eneo la Kulushasha na saba ndani ya hifadhi ya Burigi ambapo kati ya mwezi Septemba na Agosti Tembo wengine waliuawa katika maeneo ya Bwawani, eneo la Gerezani.

“Wastani wa Tembo kuuwawa kwa siku ni kati ya mmoja hadi wawili, hawa ni wale ambao tunawaona huku kijijini kwetu, lakini kule ndani ya hifadhi wapo pia wanauawa,hiyo hesabu yake  hatuijui ila siku akifa Tembo huko utaona tu magari ya maliasili yakifika porini kwa wafugaji na kuwakamata, lakini baada ya muda wanaokamatwa huachiwa,” alieleza mwanakijiji cha Ngoma wilayani Ngara.

No comments:

Post a Comment