KILA
mwaka katika kipindi kama hiki cha Majirio, yaani kuelekea siku ya kuzaliwa
Kristo Masihi, Yesu Kristo (Krismas), kote duniani huwa kuna furaha kubwa
mitaani na makanisani, majumba yakiwa yamepambwa kwa miti ya Krismas
inayonukia, maua na vikorombwezo anuai kuikaribisha siku hiyo muhimu kwa
wanadamu wote.
Zawadi
mbalimbali huandaliwa kwa ajili ya kuwapatia ndugu na jamaa, Father Christmas naye akiwaandalia watoto zawadi, huku muziki mwororo
ukitawala anga zote kupitia kwenye redio au televisheni.
Ni
wakati huu ambapo muziki unaotawala huwa ni wa yule mkongwe wa muziki laini,
marehemu Jim Reeves wa Marekani, ambaye vibao vyake 12 kikiwemo cha Jingle Bells pamoja na
kundi la Boney M vibao
vyao vinatamba duniani kote ikiwa ni pamoja na hapa Tanzania, ambako pia
hukolezwa na kibao cha Komandoo Hamza Kalala kisemacho Noel-Krimas.
Lakini
mbali na vibao hivyo, kwa ukanda mzima wa Afrika kibao ambacho hutamba zaidi na
kuchukua chati ya juu ni kile kinachojulikana kama Kakoele, ama Viva Christmas au Noel Krismas, kwa vyovyote utakavyokiita.
Nasi
kwa kuwatakia heri na baraka za kusherehekea sikukuu hiyo ya Krismas pamoja na
Mwaka Mpya, kwa nia njema kabisa, leo tumeamua kuwaletea kibao hicho ambacho
kimeimbwa kwa lugha ya Kilingala.
Wimbo
huo umetungwa na kuimbwa na marehemu Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda Gaston
Omer maarufu Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, mwanamuziki kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire) ambaye alikuwa maarufu katika
ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kibao
hicho kilichomo kwenye albam yake ijulikanayo kwa majina niliyoyasema hapo juu
kilifyatuliwa takriban miaka 35 iliyopita nchini Kenya, lakini bado kinaendelea
kutamba na kitaendelea kutamba kwa mashabiki na wafuasi wote wa dini ya
Kikristo kutokana na ujumbe uliomo ndani.
Wimbo
huo unaosikika kila ikaribiapo sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya uliweza
kumjengea jina na sifa kubwa mkongwe huyo ingawa hakuwa mashuhuri kama
walivyokuwa akina Joseph Kabasele ‘Le Grand Kalle’, Dk. Nico Kassanda ‘Kassanda
Nicalay’, L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi (Francis Makiadi) ama
Franco na wengineo kutoka Zaire.
Aliifyatua
albam hiyo kwa ajili ya nyimbo za Krismas tu kama alivyofanya Jimmy Reeves,
ambapo ina jumla ya nyimbo tano ukiwemo huo wa Kakoele au Krismas. Nyingine ni Nakumbuka Krismas, Bewela Krismas,
Super Krismas na Topele
Krismas.
Kwa
hiyo anamtaka ajaribu kujivua uchoyo wake na kuwa mkarimu siku hiyo kisha
amwonyeshe angalau pendo linalotakiwa kwa binadamu badala ya lile la ‘Chuna
Buzi’.
Hali
kadhalika, katika ushauri huo kwa Kakoele, anatukumbusha wanadamu wote kuwa
tunawajibika wakati huu kushinda udhaifu wetu na kudhihirisha pendo la kweli
ambalo limeletwa na Bwana Yesu Kristo.
Ni
kibao kilichopambwa na maneno ya kumweleza muhibu wako, lakini kikiwa kimelenga
hasa kuwataka wanadamu wote wapendane kama lilivyokuwa kusudi la Bwana Yesu,
ambaye wanadamu wote tunaamini kwamba hata wakati anapaa aliwaambia wanafunzi
wake kuwa, Wapendane, kama Mungu alivyowapenda wanadamu na kumtuma Yeye ili
auokoe ulimwengu na vilivyomo!
Baba
Gaston alizaliwa Julai 5, 1936 mjini Lubumbashi kusini-mashariki mwa Zaire na
kujipatia elimu yake ya msingi katika shule ya St. Gabriel, Kapolowe katika
Jimbo la Shaba na baadaye akafanikiwa kuendelea na masomo ya juu katika shule
ya Benedict Catholic Fathers ya mjini Likasi.
Alijitosa
katika ulimwengu wa muziki akiwa na miaka 20 katika Jiji la Kinshasa kwa kuanza
kuimba kwaya kanisani kabla ya kuingia kwenye muziki wa Jazz akiwa na bendi
yake mpya ya Orchestra Baba
Nationale na wimo wake wa kwanza ukiwa ‘Barua kwa Mpenzi Gaston’.
Mwaka
1972 gwiji huyo aliamua kuja Tanzania ambapo onyesho lake la kwanza lilikuwa
katika ukumbi maarufu wakati huo wa White House, Kimara jijini Dar es Salaam,
ambako pia ndiko kulikuwa maskani ya bendi ya Marquiz du Zaire (OMACO), bendi
ambayo sasa ni marehemu!
Miaka
mitatu baadaye mwanamuziki huyo akiwa na mkewe na watoto wake kadhaa aliamua
kuchanja mbuga na kwenda Kenya ambako aliendelea kuimba kabla ya kwenda Arusha
alikozindua kibao chake kingine maarufu cha Talaka Mpakani Yanitoa Jasho na
kuongeza raha pale alipozingua na kibao kingine cha Mapendo Kizunguzungu.
Baadaye
mwaka 1994 akiwa na familia yake alihamishia maskani yake mjini Arusha akitokea
Nairobi, Kenya, ambapo alikuwa ameachana na muziki na alitegemea zaidi biashara
zake za duka la kuuza vyakula mbalimbali katika eneo la Majengo katika barabara
ya Sokoine.
Mwanamuziki
huyo alifariki dunai Jumamosi Machi 18, 1997 katika Hospitali ya KCMC mjini
Moshi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Alifariki akiwa anakaribia
kabisa kufikisha miaka 61. Akaenda kuzikwa katika makaburi ya Lang’ata jijini
Nairobi.
No comments:
Post a Comment