MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(CHADEMA), amesema atamshawishi mbunge mwenzake wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe, ili ampatie majina ya vigogo walioficha fedha Uswisi awataje bungeni.
Zitto ndiye aliibua hoja hiyo bungeni
na kuwasilisha hoja binafsi akitaka Bunge liazimie kwa kauli moja na kuunda
kamati teule ya kuchunguza tuhuma hizo na kuwachukulia hatua, vinginevyo
serikali ikishindwa atawataja.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
mjini Kahama mkoani Shinyanga, alipopata mapokezi ya kifalme akiwa na
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche na kada mwingine, James Ole Millya,
alisema kuwa atataja majina hayo bungeni.
Lema alisema kuwa Watanzania wamekuwa
na shauku ya kuwafahamu viongozi wao mafisadi waliopora fedha zao na kwenda
kuzificha katika nchi za ughaibuni kama Uswisi, Mauritania, Dubai na Morocco.
Alisema tangu hoja hiyo ifikishwe
bungeni na serikali kuahidi kufuatilia, hadi sasa kumekuwa na ukimya ambao
unazua maswali juu ya ukweli wa suala hilo kutoka kwa wananchi.
“Nitamuomba Kamanda Zitto anipatie
majina hayo nami Bunge lijalo niyaanike ili kukata kiu ya Watanzania walio na
haja kubwa ya kuwafahamu, hata kama hatua hiyo itanisababishia kifo, mimi
siogopi kufa,” alisema Lema.
Aliwataka wakazi wa Kahama kuondokana
na woga pindi linapofikia suala la kupigania haki zao na akasema wasiwaachie
viongozi na wanachama wa CHADEMA pekee.
Lema aliishutumu Serikali ya CCM akidai
imeshindwa kuwajengea miundombinu mizuri na kuwakopesha mitaji mikubwa
wachimbaji wadogowadogo pindi wanapovumbua maeneo yenye madini.
Alisema kuwatimua wachimbaji hao ni
kupanua wigo wa watu wasiokuwa na ajira, ombwe ambalo linaweza kuigharimu nchi
hata kuingia katika machafuko.
Wakati huo huo, kada mashuhuri wa CCM,
Frank Mwaisumbe, aliyeitikisa ngome ya upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2010 akiwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini, amehamia CHADEMA.
Mwaisumbe aliyewahi kuwa Mhadhiri
Msaidizi wa Kitivo cha Uchumi na Biashara katika Chuo Kikuu cha Tumaini-Iringa,
kabla ya kuachana na kazi hiyo, ametangaza kujiunga na CHADEMA juzi.
Alisema CCM imeshindwa kushughulikia
kero na matatizo ya wananchi ikiwemo rushwa na makundi yanayowania madaraka.
Jimbo hilo la Mbeya Mjini kwa sasa
linaongozwa na Mbunge wa CHADEMA, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu baada
kumshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Benson Mpesya.
Katika hatua nyingine, vijana
wametakiwa kutokuwa na fikra mgando katika kupambana na matumizi mabovu ya
rasilimali yanayofanywa na baadhi ya watu wachache ili kuliokoa taifa linaloangamia.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti
wa BAVICHA Mkoa wa Iringa, Joseph Lyata katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Kijiji cha Luganga wilayani Kilolo.
Lyata alisema ili taifa liweze kusonga
mbele, lazima liwe na watu wenye uchungu na rasilimali zilizopo na kujali
matumizi ya pamoja.
No comments:
Post a Comment