Mtu
mwenye silaha alimpiga risasi na kumjeruhi vibaya padri wa Kikatoliki Mjini
Zanzibar siku ya Jumanne (tarehe 25 Disemba), liliripoti shirika la habari la
AFP.
Padri
Ambrose Mkenda, mkuu wa Kanisa la Kikatoliki la Tomondo, alipigwa risasi
alipokuwa akirudi nyumbani kutoka kanisa lake kiasi cha saa 1:45 magharibi,
alisema msemaji wa polisi wa Zanzibar Aziz Juma. Mkenda alipigwa risasi mkononi
na kifuani kwa kutumia bastola.
Juma
alisema haikufahamika mara moja ikiwa mashambulizi hayo yamechochewa na dini.
"Uchunguzi unaendelea, lakini inawezakana pia kwamba washambuliaji
walidhani padri huyo alikuwa na fedha," alisema.
Huku
madaktari wakipigania kunusuru maisha yake, waumini wa Kikristo walikusanyika
kwenye Hospitali ya Mnazi-Mmoja iliyo mji mkongwe wa Zanzibar. Wakristo ni
asilimia 3 ya Wazanzibari milioni 1.2, wengi wao wakiwa ni Waislamu.
Hii
ni mara ya pili kwa kiongozi wa kidini kushambuliwa ndani ya kipindi cha miezi
miwili. Katibu Mkuu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga
alijeruhiwa mnamo tarehe 6 Novemba pale alipomwagiwa maji yanaoaminika kuwa ni
tindikali usoni na mwilini.
No comments:
Post a Comment