Uwazi katika
mikataba ya ardhi utawezesha kuondoa migogoro kati ya wawekezaji na wamiliki
zikiwemo serikali za vijiji.
Hayo
yameibuliwa wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea wilaya za Kilwa na Rufiji kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa
matumizi ya ardhi, hususan katika uwekezaji katika kuzalisha nishati mimea.
Ziara
hiyo iliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (Jet),
ilifanyika katika vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti (Kilwa) na
Rungungu, Mangwi na Chumbi C wilayani Rufiji.
Mwenyekiti
wa Jet, Johnson Mbwambo, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana kuwa wimbi la uwekezaji mkubwa katika nishati mimea, limewaacha wanavijiji
hao bila ardhi iliyotumika awali kwa kilimo na shughuli za maendeleo.
“Wanavijiji
wengi hawana ardhi baada ya serikali kuingia mikataba na wawekezaji kukodisha
ardhi kwa miaka mingi bila kujua masharti wala kuelimishwa na halmashauri za
wilaya husika,” alisema.
Mbwambo
alisema katika vijiji vya Mavuji, Migeregere, Nainokwe na Liwiti, wanavijiji
walidai kushinikizwa na viongozi wa wilaya na mkoa, kukodisha jumla ya ekari
160,000 kwa mwekezaji mmoja ambaye hata hivyo hivi sasa hajulikani alipo.
“Wanavijiji
hao walidai kuwa mwanasheria wa mkoa, alisimamia mikataba hiyo kati ya mwaka
2006 na 2007 iliyoandikwa kwa Kiingereza pasipo kufafanulia haki na wajibu
wao,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mbwambo, madai ya wanavijiji hao yaliungwa mkono na viongozi wao
waliothibitisha kutokuwa na nakala za mikataba husika.
Pia
walisema jitihada za kuzifuatilia nakala hizo ofisi za halmashauri ya wilaya na
Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) jijini Dar es Salaam, hazijafanikiwa.
Mbwambo
alimnukuu Mwanasheria wa Wilaya ya Kilwa, Godfrey Jafar, akithibitisha ofisi
yake kutokuwa na nakala ya mkataba wa ukodishwaji wa ardhi hiyo.
Ilielezwa
kuwa kutoonekana kwa mikataba hiyo kumejenga hisia ya kuwapo mabadiliko, hasa
yanayohusu muda wa umiliki. Mbwambo
alisema uchunguzi uliofanywa na Jet ulibaini kuwa eneo hilo lililokodishwa kwa
ajili ya kilimo cha miboni, halikutumika ilivyokusudiwa badala yake wawekezaji
walikata miti, kutengeneza mbao na kuzisafirisha nje ya nchi.
“Baadaye
alisitisha shughuli zote na maofisa wake kuondoka wilayani Kilwa kwa sababu ya
kile kilichoelezwa iliishiwa fedha kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi duniani,
alisema.
Aliongeza:
“Kwa maana hiyo eneo hilo halijaendelezwa na vijiji havina haki kisheria ya
kulitumia.”
Mbwambo
alisema wanavijiji hao walipendekeza mambo kadhaa, ikiwamo kuitaka halmashauri
za wilaya kuwajibika katika kuwaelimisha kuhusu masuala ya ardhi na mipata
yake.
Pia
walipendekeza kuondolewa kwa sheria inayowaruhusu wawekezaji kukodishwa ardhi
kwa miaka 99, badala yake (ardhi) itumike kwa ubia na wamiliki (kijiji) kwa
kipindi kisichozidi miaka 15.
No comments:
Post a Comment