To Chat with me click here

Monday, December 3, 2012

SIRI ZA CHADEMA ZAWEKWA HADHARANI *NAPE ADAI VIGOGO WENGI WANA KADI ZA CCM *ASEMA HADI SASA WANAZILIPIA OFISI ZA CHAMA

Nape Nnauye
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Bw. Nape Nnauye, amefichua siri nzito ndani ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Amesema vigogo wengi wa chama hicho wameendelea kuwa na kadi za CCM pamoja na kuzilipia jambo linalothibitisha unafiki walionao viongozi wengi wa upinzani nchini.

Bw. Nnauye aliyasema hayo jijini Mwanza jana wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, wenye lengo la kupokea maazimio ya Mkutano
Mkuu wa nane wa chama hicho.

Maazimio hayo yalifikiwa katika mkutano uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni ambao ulifungwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete ambapo wajumbe wa mkutano huo wilayani humo pia watatumia fursa hiyo kuijadili hotuba yake.

Bw. Nnauye alidai kuwa, hivi sasa siasa imevamiwa na watu aliowaita “makanjanja” ambao kazi yao ni kuganga njaa hivyo huishi kinafiki na kuwadanganya Watanzania.

Amekitaka chama tawala CCM kuhakikisha kinatoa uongozi mzuri ili kudhibiti uvamizi wa makanjanja katika suala zima siasa nchini.

“Siasa za leo zimevamiwa na makanjanja waganga njaa ambao kwa kweli, wanachokisema na kukitenda ni vitu viwili tofauti, wapo viongozi wengi wa CHADEMA ambao kucha kutwa wanaipiga vijembe CCM lakini tunawaona wakija kulipia kadi zao.

“Kama nasema uwongo, Babu Dkt. Slaa (Katibu Mkuu wa CHADEMA), ajitokeze na kuueleza umma kadi yake ya CCM aliirudisha lini na kukmabidhi nani,” alisema Bw. Nnauye.

Bw. Nnauye alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, anayo orodha ya vigogo wa CHADEMA ambao wamekuwa wakienda katika ofisi za CCM kulipia kadi zao mara kwa mara hivyo wanapokaa majukwaani na kukipiga vijembe chama tawala ni unafiki mtupu,” alisema.

“Kauli ya Dk. Slaa kudai anataka kukisafisha CHADEMA akidai baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi za chini ni mamluki ambao wamepandikizwa na CCM ni kuweweseka.

“Wenye kadi za CCM ndani ya CHADEMA si viongozi wadogo tu, hata vigogo wa juu kabisa wana kadi za chama tawala hivyo awe makini asije kujikuta anajifukuza na yeye,” alisema.

Akizungumzia tuhuma mbalimbali zilizotolewa na Dkt. Slaa kwa sekretarieti mpya ya CCM, Bw. Nnauye alimshangaa kiongozi huyo kushughulika na uongozi ndani ya chama tawala badala ya kukijenga chama chake ambako kinamfia mikononi mwake kila kukicha.

“Mimi namshangaa Dkt. Slaa, badala ya kukijenga chama chake ambacho kinamfia mikononi mwake kila siku, anaweweseka na sekretariete mpya ya CCM, nani kampa kazi ya kuitathmini
safu ya uongozi ndani ya chama chetu,” alihoji Bw. Nnauye.

Aliwapongeza viongozi wa CCM wilayani humo kwa kuitisha mkutano huo ili kuyajadili na kuyaendeleza yale yaliyoamuliwa
na Mkutano Mkuu wa nane uliofanyika hivi karibuni.

“Palianza kujengeka utamaduni ambao haukuwa mzuri sana, baada ya kufanyika maamuzi kwenye vikao, hakukuwa na utaratibu wa ngazi za chini kuyachukua maamuzi na kuweka mkakati wa kuyatekeleza hivyo nyie mmefungua ukurasa mpya.

“Nawapongeza kwa kufanya uamuzi sahihi wenye tija kwa chama chetu, nachukua fursa hii kuziagiza wilaya zote nchini na ngazi zingine za chama kuiga mfano wetu,” alisema.

Alisisitiza kuwa, agizo la Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana kuwa lazima CCM itoke ofisini na kwenda kwa wananchi kama njia ya kuwa karibu zaidi na watu, kujua matatizo yao na kuyapatia ufumbuzi wa haraka.

“Nasisitiza viongozi wa kukaa ofisini hatuwataki kwa sasa, lazima agizo la Katibu Mkuu litekelezwe kwa vitendo ili tuipeleke CCM kwa wananchi, mtaani ili kusikiliza, kujua matatizo yao na kuyafanyia kazi ipasavyo,” alisema Bw. Nnauye.

No comments:

Post a Comment